25 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Odion Ighalo Anavyosukumwa na kivuli cha marehemu dada yake

BADI MCHOMOLO

BAADHI ya mafanikio kwa wachezaji yanatokana na familia wanayotokea, wengine wafanya vizuri viwanjani kutokana na kuwa na kipaji cha mchezo husika, wengine kutokana na kuupenda, lakini wapo ambao wanapambana kwa ajili ya kuyaka kuikwamua familia kutokana na hali mbaya ya kiuchumi.

Wachezaji wengi ambao wanatoka Amerika ya Kusini wanadaiwa kutokea kwenye familia ya hali ya kawaida, hivyo wanautumia mchezo kama sehemu ya kuziokoa familia zao, hivyo wanapambana sana ndani ya uwanja.

Hii sio tu kwa wachezaji wa Amerika ya Kusini, hata bara ya Afrika wapo wachezaji ambao wanafanya vizuri viwanjani kutokana na kuzipigania familia zao kwa kuwa michezo ni ajira kubwa duniani.

Miongoni mwa wachezaji wa kiafrika ambao wametokea katika familia za hali ya chini na baadae kwenda kuzikomboa ni pamoja na Michael Essien raia wa nchini Ghana ambaye akaja kupata nafasi ya kucheza klabu kubwa duniani kama vile Real Madrid, Chelsea na zingine nyingi, lakini mbali na mchezaji huyo kuna wachezaji wengine wengi ambao wametokea kwenye mazingira magumu ambayo yamewasababisha kupambana kwenye michezo na kufika mbali.

Odion Ighalo, mshambuliaji wa timu ya Shanghai Greenland Shenhua FC ya nchini China, lakini kwa sasa anakipiga katika klabu ya Manchester United kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu huu.

Hiyo ni kama ndoto kwake kupata nafasi ya kucheza moja ya klabu kubwa nchini England na kuwa mchezaji wa kwanza kutoka nchini Nigeria kucheza soka katika klabu hiyo.

Thamani ya jina lake ilianza kuonekana mwaka jana kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika huku Algeria wakiibuka mabingwa huko nchini Misri, wakati huo mchezaji huyo akiibuka kinara wa mabao.

Klabu mbalimbali zilionesha nia ya kuitaka saini yake mwishoni mwa msimu uliopita wakati huo anaitumikia klabu ya Changchun Yatai FC ya huko nchini China, lakini Shanghai Greenland Shenhua FC walionesha jeuri ya fedha na kuinasa saini yake.

Wakati wa tetesi za uhamisho wa dirisha dogo la usajili Januari mwaka huu mchezaji huyo alikuwa anahusishwa na klabu mbalimbali ikiwa pamoja na Manchester United, ambao walikuwa wanahitaji mshambuliaji kwa ajili ya kuboresha kikosi chao.

United walituma ofa kwa uongozi wa klabu ya Shanghai Greenland Shenhua FC kwa kuhitaji saini ya mchezaji huyo kwa mkopo, huku mazungumzo yakiendelea kati ya klabu na klabu, mchezaji huyo alitengeneza majadiliano na dada yake ambaye alikuwa anajulikana kwa jina Mary, aliyepoteza maisha wiki sita kabla ya Ighalo kujiunga na Man United.

Inasemekana kuwa Mary alikuwa na ushawishi mkubwa kwa Ighalo kuweza kuhamia United kwa mkopo, lakini alipoteza maisha kabla ya kumuona kaka yake akitimiza ndoto hizo za kucheza soka kwenye viwanja vya Old Trafford.

Usajili wa Ighalo ulionekana hauna maana ndani ya kikosi hicho, hapakuwa na mashabiki wengi ambao walikubaliana na uwezo wake, hivyo alijiunga United akiwa na machungu ya kumpoteza dada yake, lakini wakati huo huo alikuwa hakubaliki na mashabiki wengi, jambo hilo lilimfanya ajitume sana mazoezini ili kumshawishi kocha aweze kumpa nafasi kwenye kikosi chake na kuwatuliza mashabiki.

Alianza kufungua ukurasa wake wa mabao ndani ya klabu hiyo katika mchezo wa Kombe la Europa hatua ya 32 bora huku United ikishinda mabao 5-0 dhidi ya Club Brugge.

Kwenye mchezo huo Ighalo alionekana kumtafutia dada yake zawadi ya bao ambapo baada ya kufunga alifunua jezi na kuionesha picha ya dada yake huyo enzi za uhai wake, huku baadae kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii aliweka wazi kuwa, kila bao ambalo atalifunga akiwa na Man United ni zawadi kwa dada yake ambaye hajayaona mafanikio yake akiwa na klabu hiyo.

Juzi mchezaji huyo aliwaziba tena baadhi ya mashabiki wa Manchester United ambao walikuwa hawana imani naye, akiwafungia mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Derby County kwenye michuano hiyo ya Kombe la FA.

Baada ya ushindi huo bado aliendelea kumtaja dada yake huku akisema, muda mwingi amekuwa akimfikiria kwa kuwa ndio mmoja kati ya watu waliomshawishi kukubali kujiunga na United wakati wa Januari mwaka huu, hivyo alitamani awe anaona akiwa na mafanikio hayo.

Juzi kwenye ukurasa wake wa Instagram, Ighalo aliposti picha kubwa akiwa na dada yake huyo enzi za uhai wake na kudai kuwa, anachokifanya uwanjani akiwa na Manchester United ni kutokana na kumuwaza yeye na ndio maana anapata nguvu ya kuipigania timu na anadhani kwa kufanya hivyo anampa furaha dada yake japokuwa hayupo duniani.

Mary Atole alipoteza maisha ghafla akiwa nyumbani kwake huko nchini Canada, Desemba mwaka jana baada ya kuanguka.

Kutokana na kile ambacho anakifanya mchezaji huyo kuna uwezekano mkubwa wa kumshawishi kocha wa Manchester United kumsajili moja kwa moja mara baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa mkopo mwishoni mwa msimu huu na hilo ndio lengo la Ighalo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,538FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles