23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

ODINGA, KENYATTA WAINGIA MITINI

NA MWANDISHI WETU,

RAIS Uhuru Kenyatta na mgombea urais kwa tiketi ya Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA), Raila Odinga, hawatashiriki mdahalo utakaowakutanisha wagombea urais Julai 10 na 24, kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 8, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari nchini Kenya, wagombea wote wawili wamesema hakukuwa na makubaliano yoyote baina ya waandaaji na kambi za wanasiasa hao.

Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee, Raphael Tuju, aliviambia vyombo vya habari nchini Kenya wiki hii kuwa, waandaaji wa mdahalo huo ambao ni Debate Media, hawakuwasiliana na chama chao ili kupata baraka na kuthibitisha kushiriki midahalo miwili ambayo imepangwa kufanyika tarehe tofauti, Julai 10 na mwingine Julai 24.

“Tumeona matangazo ya mdahalo huo kwenye vyombo vya habari tu na hakika hatuwafahamu wanaoandaa. Walipanga tarehe za midahalo bila kutushirikisha wala kumweleza Rais mwenyewe,” alisema Tuju.

“Waandaaji hawakuwasiliana na Ikulu wala chama cha Jubilee. Hatufahamu kanuni na taratibu zinazoendesha midahalo hiyo na hatutashiriki kabisa,” aliongeza.

Akizungumzia suala hilo, mshauri mkuu wa Nasa, Salim Lone, alisema Raila Odinga hatashiriki mdahalo wowote kwa wakati huu, licha ya kuwa tayari.

“Hata hivyo nisisitize, sekretarieti ya kampeni za urais ya Nasa, inamshauri Rais Uhuru Kenyatta kuwa wazi kushiriki mdahalo na Odinga kuhusu masuala mbalimbali yanayogusa jamii kwa kipindi hiki,” alisema Salim Lone.

Midahalo hiyo imeandaliwa na Kampuni ya Debate Media Limited, ambayo tayari imeshatinga kortini na mgombea mwingine wa urais kwa tiketi ya chama cha Alliance for Real Change, Abduba Dida.

Chama cha Alliance for Real Change kimeishtaki kampuni ya Debate Media Limited kwa madai ya kutoandaa mdahalo unaowahusisha wagombea wawili maarufu, Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, ambao tayari wametawala kwenye kura za maoni.

Chama hicho kinadai kuwa, kampuni hiyo iache mara moja kuendesha mdahalo unaozihusisha pande mbili tu; Odinga na Kenyatta.

Aidha, chama hicho kimesema ni kampuni ya hiyo hiyo ndiyo ilitoa matokeo ya kura za maoni na kuwapa nafasi Odinga na Kenyatta zaidi, huku wengine wakiambulia aslimia 5 ya kura za maoni.

Dida amepinga utaratibu wa kuwaweka kwenye makundi wagombea wa nafasi mbalimbali kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, mwaka huu.

Kutokana na uamuzi huo, Kampuni ya Debate Media imebainisha kupata hasara ya Sh milioni 200 za Kenya kwenye matangazo waliyolipia.

MGAWANYO WA MIDAHALO

Taarifa ya kuandaliwa midahalo hiyo ilitolewa na Wachira Waruru, ambaye ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati.

Kwa mujibu wa Waruru, Kamati hiyo ilipanga midahalo mitatu ambapo yote ingefanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, kilichopo nchini humo.

Aidha, mwenyekiti huyo alibainisha kuwa, midahalo hiyo ingerushwa moja kwa moja na televisheni kuanzia saa moja na nusu usiku kupitia redio na televisheni mbalimbali, hatua ambayo ingewasaidia wapigakura kuchambua kwa kina sera na mikakati ya maendeleo ya wagombea hao kabla ya kuamua nani wamchague kuwa rais wao.

Utaratibu wa midahalo hiyo ni kwamba, awamu ya kwanza ungehusisha wagombea urais peke yao, ambao ulipangwa kufanyika Julai 10, mwaka huu.

Aidha, kwa upande wa wagombea wenza, wangelikuwa na mdahalo wao Julai 17, mwaka huu, yaani siku 7 baada ya mdahalo wa wagombea wa urais.

Duru la tatu la mdahalo wa mwisho litafanyika Julai 24, mwaka huu, likiwakutanisha tena wagombea wote 18 wa urais, ikiwa ni siku 7 kabla ya zoezi la uchaguzi mkuu.

WAGOMBEA WA VYAMA VYA SIASA NA BINAFSI

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi nchini humo, kuna wagombea 18 wa urais, ambao ni Uhuru Kenyatta (Jubilee), Raila Odinga (ODM-Nasa), Peter Ondeng (Restore and Build Kenya), Abduba Dida (Tunza Coalition), Kennedy Mongare (Federal Party of Kenya), Ekuru Aukot (Thirdway Alliance Party)  na Cyrus Jirongo (UDP).

Wagombea binafsi ni Profesa Michael Wainaina, Joe Nyagah, Nazlin Omar, David Munga, Stephen Oweke Oganga, Robert Mukwana Juma, Joseph Ngacha, Japheth Kavinga, Nixon Kukubah, Joseph Musyoka, Edwin Wambua, Erastus Nyamera na Amram Musungu (39), mwenye uraia wa nchi mbili (Marekani na Kenya) ambaye anaishi Marekani.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kinyang’anyiro cha mwaka huu kitaendelea kwa wagombea wawili; Uhuru Kenyatta kutoka chama tawala cha Jubilee na Raila Odinga wa Muungano wa upinzani wa NASA.

Ushindani mkubwa ni kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, kutokana na kuchuana vilivyo kwenye uchaguzi uliopita wa mwaka 2013.

Kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi nchini humo, wagombea wanatakiwa kupata saini za wadhamini 1,000 katika nafasi ya bunge, wakati wagombea wa useneta wanatakiwa kupata saini 2,000.

Aidha, kwa wagombea binafsi wanatakiwa kukusanya saini 500 kutoka kata zao, kabla ya kuwasilisha maombi ya kugombea kwa Tume ya Uchaguzi.

MDAHALO WA MWAKA 2013

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2013 wagombea walioshiriki mdahalo walikuwa Raila Odinga, Uhuru Kenyatta, Musalia Mudavadi, Peter Kenneth, James Kiyiapi na Martha Karua.

Mdahalo huo ulifanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Brookhouse, jijini Nairobi, nchini humo, ukiwa na mada kuu za usalama, huduma za jamii na usimamizi wa rasilimali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles