LONDON, ENGLAND
KINDA wa Real Madrid, Marin Odegaard, juzi alikiri kufunikwa na kiwango cha kinda wa Manchester United, Marcus Rashford.
Kauli ya Odegaard ilitokana na kiwango cha Rashford ambaye anacheza katika timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 21 nchini England, kufunga ‘hat trick’ katika ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Norway mchezo uliochezwa juzi uwanja wa Community England.
Odegaard hakuwa katika kiwango kizuri kwenye mchezo huo ambao alishuhudia timu yake ikishindwa kuzuia kasi ya Rashford ambaye alionekana kuwa katika kiwango bora zaidi.
Kiwango hicho kilifanya Odegaard ambaye alikuwa mara yake ya kwanza kucheza katika ardhi ya England amsifu Rashford kutokana na uwezo wake uwanjani.
“Ni miongoni mwa wachezaji wa kiwango bora niliowahi kuwaona katika soka pia Rashford aliwahi kuonesha kiwango hicho akiwa Ligi Kuu England,” alisema Odegaard.
Odegaard alisema angependa siku moja acheze pamoja na nyota huyo kati ya Manchester United au Real Madrid.
“Ni vizuri kucheza na mchezaji anaye kuvutia uwanjani,” alisema Odegaard.
Akizungumzia kiwango chake Madrid alisema anajitahidi kuhakikisha anacheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
“Natarajia nitapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza hivyo najituma kuhakikisha lengo langu linatimia,” alisema Odegaard.
Nyota huyo aliongeza kwamba, bado umri wake wa miaka 17 unaruhusu kujifunza zaidi.