23.7 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

Obasanjo achana kadi ya chama tawala

ObasanjoMwandishi Wetu na Mashirika ya Habari
RAIS wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, juzi alichana kadi yake ya uanachama wa chama tawala cha Peoples Democratic (PDP) na kutangaza kuachana na siasa.
Obasanjo aliichana kadi yake hiyo katika makazi yake ya Hilltop huko Abeokuta Kaskazini wakati akizungumza na viongozi wa PDP kutoka kata 11.
Viongozi wa chama hicho katika kata hizo walienda kumwona Obasanjo ili kusafisha hali ya hewa baada ya kuibuka minong’ono kwamba ametimuliwa kutoka chama hicho kutokana na mlolongo wa matamshi yake ya kukikosoa katika vyombo vya habari.
Obasanjo alisema alifahamu uwapo wa minong’ono hiyo, lakini alitania kuwa aliamua kujiondoa mwenyewe, akiahidi kutojiunga na chama kingine cha siasa.
“Walisema wanataka kunitimua kutoka PDP, japokuwa sijaambiwa. Tumekuwa tukijaribu kumkimbia mtu, lakini ameomba tumsubiri upande mwingine wa mto.
“Niliwahi kuwaambia kuwa nilikuwa rais kwa jukwaa la PDP, kwa heshima yake, nikiondoka, sitajiunga na chama kingine. Nitabakia Mnigeria wa kawaida; niko tayari kufanya kazi na yeyote bila kujali itikadi yake ya kisiasa. Kwanini baadhi ya watu wanataka kunitimua? Hawana haja ya kusumbuka. Basi isiwe tabu, hii hapa kadi yenu ya uanachama, ichukueni,” alisema.
Kabla ya kuichana kadi hiyo, Obasanjo aliorodhesha mlolongo wa udhaifu wa Serikali ya Rais Goodluck Jonathan kuanzia ukosefu wa usalama, ajira hadi mfumuko wa bei na ufisadi.
Lakini mwenyekiti wa PDP katika Jimbo la Ogun, alisema Obasanjo alishatimuliwa kutoka chama hicho baada ya kuichana kadi yake ya uanachama hadharani.
Mgogoro huo mpya uliibuka baada ya tukio la kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu kutoka Februari 14 hadi Machi mwaka huu.
Obasanjo alihusisha uamuzi huo wa Tume Huru ya Uchaguzi na mpango wa kumnufaisha Jonathan ambaye anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha All Progressives Congress (APC), Muhammadu Buhari.
Muda mchache kabla ya kutimuliwa katika chama, Obasanjo aliwaambia waandishi wa habari kwamba alikuwa akitarajia kutimuliwa japo ujumbe ulimfikia mapema kabla ya tangazo.
Rais Jonathan amekuwa akimlaumu Obasanjo kwa kumpigia debe mpinzani wake, Buhari.
Katika mahojiano na jarida la Financial Times wiki iliyopita, Obasanjo alimpitisha Buhari, mtawala wa zamani wa kijeshi katika miaka ya 1980 anayeonekana kuwa na msimamo mkali katika masuala ya usalama na rushwa.
Mwaka 2013, Obasanjo aliandika barua ya wazi akimtaka Jonathan asiwanie muhula wa pili wa urais akiufananisha urais wake na ule wa Jenerali Sani Abacha, ambaye utawala wake wa kijeshi wa miaka mitano katika miaka ya 1990 ulitawaliwa na ukiukaji wa haki za binadamu na uporaji fedha katika taifa hilo mzalishaji mkubwa wa mafuta barani Afrika.
Obasanjo, ambaye pia aliwahi kuwa jenerali wa jeshi, aliwaudhi wengi serikalini na jeshini alipodai kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ilikuwa ni njama ya Jonathan kutumia jeshi kujiongezea muda wake ofisini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,701FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles