NEW YORK, MAREKANI
RAIS wa Marekani, Barack Obama na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, wametoa hotuba zao za mwisho katika umoja huo wakiitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi kukabiliana na mizozo ya kimataifa.
Waliitaja mizozo hiyo kama kuanzia vita nchini Syria hadi mgogoro wa  wakimbizi na mpango wa kinyuklia wa Korea Kaskazini.
Aidha, Ki-moon ambaye alihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mara ya mwisho katika kipindi chake cha uongozi cha miaka 10, aliwashutumu viongozi wa dunia kwa kushindwa kwao kutatua  mzozo wa Syria.
Akizungumzia kuhusu kuvunjika kwa mazungumzo ya amani katika Mashariki ya Kati, Ban alisema matumaini ya suluhisho la mataifa mawili kati ya Israel na Palestina yanapungua siku hadi siku kutokana na misimamo mikali hasa ya upande wa Israel.
Wakati huo huo, Rais Obama alitarajia kutangaza msamaha wa madeni na ahadi ya misaada kutoka mashirika ya Serikali ya Marekani na wawekezaji binafsi, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake kulipatia bara la Afrika nishati.