Na Nora Damian, Mtanzania Digital Dodoma
Rais Samia Suluhu Hassan amehitimisha Sikukuu ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) kwa mwaka 2024 akisema serikali imepiga hatua kubwa ambazo zimeanza kuleta matokeo mazuri huku dhamira yake ikiwa ni kujenga uchumi jumuishi katika sekta hizo muhimu.
Akihutubia Agosti 8,2024 wakati wa kilele cha sikukuu hiyo kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Rais Samia ameeleza mageuzi yaliyofanywa katika sekta hizo, miradi inayoendelea pamoja na kutoa maelekezo kwa watendaji na kuitafsiri kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu.
Amesema walitoa ahadi na wameonyesha nia ya kuzitekeleza kwa vitendo kwa kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi ni kipaumbele kwa Serikali ambayo inatumia sekta hizo kutengeneza ajira kwa vijana.
Amesema kutokana na ongezeko la bajeti katika Wizara ya Kilimo na ile ya Mifugo na Uvuvi sasa wanajielekeza kukuza tafiti kwenye maeneo yote ya kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuongeza tija ya uzalishaji na kupata masoko ya kimataifa.
NAMBA ZINAONGEA
Rais Samia amesema mwaka 2023 sekta ya kilimo imekua kwa asilimia 4.2 na kuchangia asilimia 26.5 katika Pato la Taifa, kutoa ajira kwa wananchi kwa asilimia 65.6, kuchangia upatikanaji wa malighafi za viwandani kwa asilimia 65, kuongeza mauzo ya nje kwa asilimia 30 na kuhakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa chakula kwa zaidi ya asilimia 100.
Amesema kiwango cha uzalishaji wa mazao ya chakula kimeongezeka kutoka tani milioni 17.1 (2021/2022) hadi kufikia tani milioni 20.4 (2023/2024) sawa na asilimia 19.
Amesema tija ya zao la mpunga imeongezeka kutoka tani 1.25 kwa hekta hadi tani 4 malengo yakiwa ni kufikia tani 7 wakati kwa mahindi imeongezeka kutoka tani 2 kwa hekta hadi tani 4.5 malengo yakiwa ni kufikia tani 5.
“Miaka minne iliyopita zao la mbaazi halikuwa na thamani kabisa, walikuwa wananunua mbaazi kilo Sh 200 lakini leo ni Sh 4,000, zao la kokoa walikuwa wanauza kilo Sh 7,000 hadi 8,000 lakini bei imepanda na sasa inauzwa Sh 30,000…serikali tumetafuta mbinu na kutafuta masoko na tutaendelea kufanya hivyo kwa mazao mengine ili bei iwe nzuri wakulima waweze kujitegemea,” amesema Rais Samia.
Kuhusu sekta ya mifugo amesema uzalishaji wa mifugo na mbegu za malisho katika mashamba ya serikali umeongezeka kutoka tani 22.7 (2022/2023) hadi kufikia tani 127.8 (2023/2024) huku uzalishaji wa vyakula vya mifugo vilivyosindikwa ukiongezeka kutoka tani 1.6 (2020/2023) hadi kufikia tani 1.9 (2023/2024).
Amesema uzalishaji wa mazao ya samaki umeongezeka kutoka tani 506,549 (2020/20221) hadi kufikia tani 517,896 (2022/2023) zenye thamani ya Sh trilioni 3.34 ambapo miundombinu ya uvuvi inaendelea kuimarishwa kwa ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa Masoko mkoani Lindi.
Amesema masoko saba ya mazao ya uvuvi yamejengwa, vituo vya ukuzaji viumbe maji, mashamba darasa na mialo ambayo itaimarishwa kwa kujengwa mitambo ya kuhifadhia mazao kama vile vyumba vya ubaridi na mitambo ya kuzalisha barafu.
“Tumeanzisha Programu ya BBT kama ilivyo kwenye kilimo cha mazao na kwenye uvuvi tumetoa mkopo wa Sh bilioni 1.1 kwa vikundi 25 vya vijana walioiva katika sekta hii ili wakawekeze zaidi,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema kutokana na mageuzi hayo makubwa wameongeza maeneo ya umwagiliaji maji, matumizi ya mbolea, uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora, kuanzisha vituo jumuishi vya zana za kilimo, kuzindua kiwanda cha kuunganisha matrekta nchini na kukabidhi zaidi ya matrekta 500 na zana kadhaa za kilimo.
“Tumenunua magari ya watendaji mikoa na wilaya ili waweze kwenda kusimamia kazi vizuri, ni fahari yangu kwamba tumeweza kuzindua matrekta 600 kwenda kwa wakulima katika maeneo mbalimbali, kiwanda cha kuunganisha matrekta sasa kipo Dodoma na hatutaagiza tena matrekta,” amesema.
Amesema huduma za ugani zimeimarishwa kote nchini kwa kutoa usafiri kwa maofisa ugani kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza idadi ya maghala ya kisasa ya kuhifadhi chakula, kujenga maabara za kisasa na za mfano Afrika ambapo chunguzi zote za kilimo zitafanywa nchini.
“Hatutapeleka tena sampuli za vitu vyetu nje na kusubiri matokeo, kuanzia mwaka 2026 mambo yote yatafanyika Tanzania, kwa wanafunzi wanaosoma Kilimo Sua tumezindua jengo la maabara mtambuka ambayo itakuwa inafanya uchunguzi wa mambo mengi ya kilimo, afya ya binadamu na wanyama…mwanafunzi akitoka pale ameiva na akija eneo la kazi vitendea kazi vipo,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema serikali inaendelea na miradi ya umwagiliaji maji 780 ambapo katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 miradi 231 itatekelezwa na ikikamilika itaongeza eneo la umwagiliaji kwa hekta 256,185 na kufanya eneo linalomwagiliwa kufikia hekta 983,466 sawa na asilimia 81.95 ya lengo la kuwa na hekta milioni 1.2 ifikapo mwaka 2025.
MATUMIZI YA MBOLEA
Rais Samia amesema wastani wa matumizi ya mbolea nchini ni kati ya kilo 19 hadi 21 kwa hekta wakati barani Afrika ni kilo 18 kwa hekta na malengo ni kuongeza kiwango kulingana na maelekezo ya Umoja wa Afrika kwa kuendelea kutoa ruzuku kwa wakulima na kuvutia viwanda kuja kuwekeza nchini.
Amesema kwa msimu ujao wataanza kutoa ruzuku ya mbegu ili kuleta nafuu kwa wakulima na kusisitiza uadilifu kwa wakulima wanaotaka mbolea au mbegu za ruzuku kufuata utaratibu kwa kujisajili kwenye mifumo.
UPATIKANAJI MIKOPO
Amesema katika kukuza sekta ya kilimo na mtaji wa kukopesha wakulima kutakuwa na bondi ya usalama wa chakula na kwamba tayari wamezungumza na benki ambazo zimeunga mkono mpango huo.
“Tutapata fedha ambazo zitawawezesha NFRA (Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula) kujijenga kiteknolojia, vifaa na ukubwa maghala ya kuhifadhi chakula, iweze kununua chakula kwa wingi kwa wakulima na kuhifadhi tujihakikishie usalama wa chakula,” amesema Rais Samia.
MAELEKEZO KWA MAWAZIRI
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ameelekezwa kuunda mamlaka ya usimamizi wa maendeleo ya ugani ili iwasimamie kwa karibu maofisa hao na kupunguza mzigo wizarani huku akiahidi kukutana na makundi ya maofisa ugani kuwaeleza maono na mipango aliyonayo katika kilimo.
Pia amemtaka Waziri Bashe kuhakikisha ahadi ya kupeleka kwa wakulima matrekta 10,000 na ‘powertillers’ 10,000 kabla ya mwaka 2030 inatekelezwa.
Kuhusu ushirika amesema; “Ili mageuzi makubwa tunayoyafanya kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi yalete matokeo ya uchumi endelevu ni lazima tujenge vyama vya ushirika vilivyo imara, naitaka Wizara ya Kilimo itupie jicho sekta hii ili kurejesha hadhi na mchango wa ushirika nchini…natafuta siku nikutane na maofisa ushirika nikae nao tuelewane kwa karibu zaidi.
Amemuelekeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, kuhakikisha kunakuwa na matumizi mazuri ya ranchi za taifa na kuziendeleza ili wafugaji waweze kujifunza na kuzitumia kwa unenepeshaji na kuleta tija.
Amesema dhamira ya serikali ni kupunguza uchungaji mifugo wa kizamani ili wawe wafugaji wa kisasa na kupata tija zaidi kwenye maeneo madogo waliyonayo.
Amesema pia katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 serikali itafanya kampeni maalumu ya utoaji chanjo kwa njia za ruzuku na kusisitiza chanjo za kuku zitakazotolewa bure si kwa kampuni zinazofuga kuku bali zielekezwe kwa wafugaji wadogo.
“Sitaki nisikie Interchick au nani kapewa chanjo bure, wale wanalipa, wafugaji wadogo wadogo kinamama ndiyo wapate chanjo bure,” amesema Rais Samia.
Amesema anatiwa moyo kuona Watanzania wanafanya biashara za mazao ya mifugo kwa viwango vya kimataifa na kumuelekeza Waziri Ulega kushughulikia changamoto za urasimu hasa katika utoaji vibali vya kusafirisha mazao.
Amesema akiwa ziarani katika Mkoa wa Morogoro alizindua mpango wa ‘Tutunzane’ wenye lengo la kuwafanya wakulima na wafugaji kuishi kwa amani ili kila mmoja aendeshe shughuli zake kwa ufanisi na kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kufikiria mipango ya aina hiyo katika maeneo yao ili kuleta utulivu nchini.
Pia amemuelekeza Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, kutoa kipaumbele kwa sekta za uzalishaji kwa kuwa ni muhimu nchini.
KAULIMBIU YA MAADHIMISHO
Akizungumzia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ‘Chagua viongozi bora wa serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu kilimo, mifugo na uvuvi’ amewataka Watanzania kuchagua watu madhubuti watakaosimamia maendeleo yao na wasikubali kupangiwa viongozi.
“Kaulimbiu hii ni sahihi kabisa kwa sababu shughuli zinafanywa kule wananchi waliko, chagueni viongozi wanaopenda maendeleo, msichague viongozi wanaopenda matumbo yao au nafsi zao…msikubali kupangiwa viongozi, kataeni wekeni wale mnaowajua watasimama na kufanya kazi kwa maendeleo yenu,” amesema Rais Samia.
WAZIRI WA MIFUGO, UVUVI
Waziri Ulega amesema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 shughuli kubwa zitakazofanyika ni kampeni ya chanjo ya mifugo na kutambua mifugo yote nchini ambapo chanjo za ruzuku zitapelekwa kwa wafugaji na kupunguza bei za chanjo.
Amesema wanaendelea na programu ya kutoa mikopo nafuu kwa wavuvi ambapo watatoa boti 450 na vizimba vya kufugia samaki 900.
“Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha kushirikiana na sekta binafsi, tunao mradi mkubwa wa kuhakikisha tunaboresha ufugaji wetu, ng’ombe bora 17,200 watasambazwa na mabanda ya kisasa 5,000, mfumo wa biogesi utatengenezwa kwa wafugaji ili kuunga mkono falasafa ya nishati safi,” amesema Ulega.
Amesema ongezeko kubwa la bajeti kutoka Sh bilioni 66 hadi Sh bilioni 465 itatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji na wavuvi nchini.
WAZIRI WA KILIMO
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema wanaiwezesha NFRA iwe kituo kikuu cha kukusanya mazao ya wakulima ambapo wameanza kununua mpunga kwa Sh 900.
Amesema pia vituo jumuishi vya matrekta 500 na pawatila 800 zinapelekwa vijini kwa ajili ya wakulima ambapo watahudumiwa kwa njia ya ruzuku.
Waziri huyo amesema mkandarasi uwanja wa Mwakangale Mbeya ameshapatikana na kwamba utabomolewa kwa ajili ya kujengwa na kuwataka waliovamiwa maeneo ya Tari waondoke haraka.
Amezishukuru benki kwa kuanza kuielewa sekta ya kilimo na kwamba katika mpango wa 2050 watatengeneza sera kuhakikisha riba zinapunguzwa zaidi.