Na FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM
KATIKA tathmini iliyofanywa na mwandishi wa makala haya katika maeneo mbalimbali ya Sinza jijini Dar es Salaam, imebainika kuwa wamiliki wa baa, nyumba za kulala wageni na ‘supermarket’ kuwa katika kipindi kigumu cha biashara wakati huu wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Imeonekana wazi kuwa biashara imekuwa ngumu kwa wafanyabiashara ukilinganisha na ilivyokuwa hapo awali.
Wamiliki wa biashara hizo wanalalama kukosa wateja na kutokutoka kwa bidhaa zao kutokana na hali ya maisha kuwa juu zaidi ukilinganisha na ilivyokuwa hapo awali.
Hali hiyo imetokana na ukata kuzidi kushika kasi katika nyanja mbalimbali za kibiashara, hivyo kusababisha wamiliki kulazimika kufunga biashara zao na wengine kuuza majengo kwa bei ya hasara. Waziri wa Fedha ameainisha kufungwa kwa biashara kwa baadhi ya wafanyabiashara, lakini anashindwa kuelewa sababu ya kutokea hayo kwani haijafanya mabadiliko ya kodi kwa kupandisha au kuongeza uwigo wa hiyo kodi.
Sasa nyumba za wageni hususani za jijini Dar es Salaam mara nyingi huaminika kwa kulala wazawa (wenyeji pekee) badala ya wageni, kutokana na ongezeko la wingi wa nyumba za wageni kuzidi kujengwa kila siku.
Lakini kwa sasa hali imekuwa ndivyo sivyo na matarajio, kwani hata wenyeji pia imekuwa ni vigumu kuingia na kupata huduma kutokana na mkwamo wa maisha.
Gharama ya chumba cha kulala kwa siku katika baadhi ya nyumba mara nyingi hutofautiana kutokana na hadhi ya mahali na mazingira husika.
Kuna baadhi ya hoteli na nyumba zina hadhi ya juu ambapo chumba kimoja kwa siku hupatikana kwa Sh 100,000 na kuendelea na zile nyumba nyingine huwa ni Sh 12,000, 15,000 , 20,000, 30,000 na kushuka chini, lakini kwa kipindi hiki imekuwa ni tofauti kiasi kwamba bei imeanguka chumba cha nyumba ya wageni Sh 12,000 hukodishwa kwa Sh 10,000 hadi 8,000 na cha Sh 20,000 kinapungia hadi kufikia Sh 18,000.
Mara nyingi kwa kipindi hiki nyumba hizo huweza kuingia wateja wawili tu, biashara ikiwa mbaya zaidi inaweza kupita siku nzima mmiliki asiingize hata mteja mmoja.
Mbali na nyumba hizo kutokupata wateja, vilevile hata katika upande wa utokaji wa vinywaji katika baa umekuwa ni shida kwani mauzo yamedorora na kuathiri zaidi biashara.
Mmiliki mmoja wa Baa ya Home Town iliyopo katika eneo la Sinza Mori ambaye hakutaka jina lake kuandikwa, aliliambia MTANZANIA kuwa mara nyingi biashara huwa ni mbaya, lakini kwa muda wa kipindi hiki cha bajeti ya mwaka mambo yamezidi kuwa magumu zaidi tofauti na matarajio.
Hali hiyo hubadilika hasa kwa kipindi hiki ikichangia kuwa na mabadiliko ya soko la biashara hiyo kusababisha kudorora siku hadi siku.
Pia changamoto nyingine ni mabadiliko ya hali ya hewa kama vile mvua ambazo zinaendelea kunyesha hivi karibuni ambayo mara nyingi endapo zikizidi huathiri mwenendo mzima wa uendeshaji wa biashara kwa wafanyabiashara wengi.
Hivyo, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mfululizo jijini Dar es Salaam na maeneo mengine mbalimbali ya mikoa ya Tanzania, wafanyabiashara wamekuwa wakilia kupungua kwa kipato katika mauzo, hata hivyo kushindwa kufikia malengo stahiki na kwa wakati mwafaka, hivyo kusababisha wananchi kuzidi kulalamikia Serikali kila siku.
Anasema unaweza kufungua biashara asubuhi lakini matokeo yake hadi kufika jioni ukashindwa kuuza chochote, kwani kuna uwezekano wa kupita siku nzima usiuze hata kidogo, hivyo mmiliki kushindwa kuiendeleza biashara hiyo.
Biashara ya ‘supermarket’
Supermarket pia zimekuwa zikikabiliwa na adha ya kutotoka kwa bidhaa na hivyo kushuka kwa mauzo ya kibiashara hususani kwa kipindi cha bajeti ya mwaka wa fedha ilipokuwa inaendelea kule Dodoma.
Mmoja wa wamiliki wa biashara ya ‘supermarket’ au duka kubwa katika maeneo ya Sinza jijini Dar es Salaam, anaielezea hali hiyo kuwa katika biashara kuna vipindi viwili vya Serikali katika biashara ambayo ni Juni mosi na Julai 30 ambavyo huwa katika mwaka wa bajeti.
Anasema kwa kipindi hicho biashara mara nyingi huwa si nzuri ukilinganisha na vipindi vilivyopita vya mwaka 2015 hadi 2016, kwani ilikuwa ni afadhali katika ufanyaji wa biashara mbalimbali nchini na hata kwa mamalishe pia.
Lakini imekuwa ni tofauti kwa mwaka huu wa 2017 tangu uanze, kwani kila kitu kimekuwa ni ghali sana na tofauti na hapo awali.
Anasema katika kipindi cha nyuma cha bajeti ya Serikali, bajeti ilikuwa nzuri watu wengi walikuwa wakifanya biashara inatoka na kuona matunda ya faida inayotokana na biashara hiyo.
“Kwa ujumla pesa ilikuwa inapatikana kwa urahisi katika nyanja mbalimbali hata kwa wapiga dili, hii ni kutokana na mzunguko mzuri wa fedha katika Serikali iliyopita,” anasema mfanyabiashara huyo.
Anasema katika biashara ya kuuza bidhaa za vyakula (supermarket), imeshuka kimapato ukilinganisha na hapo awali mteja mmoja alikuwa akinunua bidhaa hata 10 kwa siku, lakini imekuwa ni tofauti kwani kwa siku sasa mteja mmoja hununua wastani wa bidhaa 2 hadi 3 pekee.
Hali hiyo ni kutokana na watu kukosa fedha za kutosha kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa wanazohitaji kununua kwa wakati huo.
Hata hivyo, ameongeza kuwa kwa kipindi hiki hauzi mzigo kwa wakati mwafaka, kwani anaweza kununua mzigo wa wiki ukakaa mwezi mzima bila kuisha, hivyo ni tofauti na kipindi cha nyuma ilivyokuwa katika mauzo.
Anasema: “Hapo awali nilikuwa nauza bidhaa za aina mbili ambazo ni za vyakula na za watoto kama vile pampas, wipers, taulo za watoto, nguo na vitu mbalimbali vya watoto ambapo bidhaa za watoto zilikuwa ni ghali sana na ndio maana zilikuwa hazitoki kibiashara.
Katika mabadiliko ya kibiashara kwa mfanyabiashara huyo, yapo pia ya kawaida, kwani kwa siku yaweza kutokea biashara kuwa mbaya zaidi ya jana.
Anaongeza kuwa hata katika maandiko matakatifu yanasema kuwa ‘vitaumbwa vipya na vizuri vitaaga’, kauli hii yenye maana kwamba huu ndio wakati wake kwani nao utapita na utakuja mwingine.
Hali hii ni kutokana na kipindi cha mpito wa biashara ngumu kwani katika biashara kuna vipindi viwili, navyo ni kipindi cha mafanikio na kipindi cha kukosa.
Anaongeza kuwa baada ya kuona biashara ya bidhaa za watoto hazitoki, ikabidi ahamishe na kuhamia sehemu nyingine na kuweka bidhaa za watoto pekee bila kuchanganya na bidhaa za vyakula.
Anasema hali hii imekuwa ngumu hata kwa wapiga dili za hapa na pale mtaani, kukosa chochote na hatimaye juhudi zao kupiga mwamba siku hadi siku, ambapo hapo awali katika Serikali ya Awamu ya Nne, mambo yalikuwa ni rahisi kwao.
Ametoa rai kwa wapiga dili wote kwamba, kwa kipindi hiki ni wakati wa kujishughulisha na si kubweteka kusuburi mambo ya mteremko kwa hali ya sasa ilivyo na inakoelekea ni mbaya kuliko jana.
Ameongeza kuwa kwa hali iliyopo sasa hakuna fedha isiyo halali ambayo hukuitolea jasho, kwani lazima ufanye kazi kwa bidii ndipo matunda utayaona.
Kitu cha msingi hasa ni kufanya kazi kwa bidii na kwa uhalali kwa kipindi hiki ili kutokuwa tegemezi ili kufanikisha jambo husika ulilokusudia kufanya kwa wakati mwafaka.
“Kupitia njia hiyo, watu wanaofanya dili za hapa na pale watapungua kwa kiasi fulani, hatimaye tutawapata wananchi watenda kazi na wanaofanya kazi kihalali kwa kuitolea jasho,” alishauri.