NA WAANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
NYUMBA ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT – Wazalendo), iliyopo eneo la Mwandiga mkoani Kigoma, imeteketea kwa moto.
Picha za kuungua kwa nyumba ya mbunge huyo ambaye pia ni kiongozi wa ACT-Wazalendo, zilianza kusambaa jana jioni katika mitandao ya kijamii.
Mbali na picha hizo, muda mfupi baadaye, Ofisa Habari wa chama hicho, Abdallah Hamisi, alisambaza taarifa ya tukio hilo kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.
“Taarifa tulizozipokea ni kuwa nyumba ya kiongozi wa chama, ndugu Zitto Kabwe ya Mwandiga, Kigoma imeungua moto muda huu,” ulisomeka ujumbe huo.
Pia ofisa huyo alisema Kamati ya Amani (Ulinzi na Usalama) ya chama hicho chini ya Mwenyekiti wake, Mohammed Babu, inafuatilia tukio hilo na kuahidi kuendelea kutoa taarifa.
MTANZANIA Jumapili lilipomtafuta ofisa huyo kupata ufafanuzi zaidi, alisema tukio hilo limetokea wakati Zitto akiwa safarini kutoka mkoani humo.
“Bado naendelea kuwasiliana na watu wa uko, sijapata taarifa zaidi. Lakini hata Zitto mwenyewe hakuwepo, yupo safarini anaenda mkoa mwingine,” alisema.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frednand Mtui, alisema kuwa moto huo umetetekeza vitu vyote isipokuwa jenereta lililookolewa na watu waliokuwamo.
Alisema tayari maofisa wa polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wamekwenda eneo la tukio na kuanza uchunguzi ili kujua chanzo cha moto huo.
“Taarifa ya awali ni hiyo, nyumba imeteketea yote na vitu vilivyokuwemo, lakini hakuna taarifa ya kujeruhiwa au kuungua kwa mtu, tunafanya uchunguzi kujua chanzo,” alisema Kamanda Mtui.
Pia alisema Zitto ana nyumba mbili zilizopo katika eneo moja na kwamba iliyoungua ni ndogo wakati kubwa imesalimika.
Alisema Zitto aliondoka jana nyumbani kwake na kumwacha mlinzi anayetambulika kwa jina la Norbert Joseph ambaye saa 10 jioni alianza kuona moshi ukifuka.
Kamanda Mtui alisema baada ya kuona moshi huo unazidi, mlinzi huyo aliita zimamoto kutoka Kigoma iliyofika na kukuta nyumba na samani vyote vimeteketea.
Malumbano ya Zitto na Ndugai
Awali kabla taarifa ya tukio hilo, Zitto alisema Spika wa Bunge, Job Ndugai, amemwadhibu kabla ya kusikilizwa na Kamati ya Maadili.
Pia alisema hataki malumbano na Ndugai kwa sababu ameshatoa maoni yake.
Zitto alitoa kauli hiyo jana baada ya gazeti hili kutaka ufafanuzi wa baada ya Ndugai kukaririwa na Kituo cha Televisheni cha Azam akisema kwamba hata kama hakuna kanuni iliyoandikwa, lakini akiwa kama kiongozi wa Bunge anao uwezo wa kumnyamazisha Zitto kwa muda wote bungeni.
Katika maelezo yake kwa gazeti hili, Zitto, alisema hana maoni mengine dhidi ya kauli ya Ndugai kwa sababu ameishapelekwa katika Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
“Mimi sitaki malumbano na Spika. Nimeishatoa maoni yangu na ameishaamua kunipeleka Kamati ya Maadili na wakati huo huo kashaamua adhabu kabla hata sijasikilizwa. Sasa nimjibu nini tena? Nitatoa maelezo yangu Kamati ya Maadili,” alisema Zitto.
Wakati akihojiwa na Azam Tv kuhusu tathmini ya kikao cha nane cha Bunge la 11, Ndugai, aliulizwa na mwandishi kuhusu kanuni zinazompa nafasi ya kumnyamazisha Zitto.
Katika maelezo yake, Ndugai, alisema si kila kitu huandikwa katika masuala ya kikazi kwa sababu kiongozi wa kazi ana mamlaka makubwa na madaraka makubwa kuliko yaliyoandikwa.
“Sio kila jambo lazima iwe kanuni, narudia tena nimesikia watu wakibishabisha, ninao uwezo, ninao uwezo, ninao uwezo kama Spika. Ukisoma kanuni za Bunge kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho ni Spika, Spika, Spika na zipo kanuni ambazo zinamruhusu Spika kwa kadiri anavyoona inafaa, kwa busara yake namna gani aongoze Bunge.
“Huwezi kuwa unatukana Bunge, unamtukana huyo Spika halafu huyo huyo anakupa nafasi uzungumze, kwani yeye ni malaika? Mimi ni binadamu wa nyama kama binadamu mwingine. Kwa kadiri ambavyo unaninyanyasa na kunidhalilisha mbele ya watu na mimi nitatumia madaraka yangu na mamlaka niliyonayo ambayo nimepewa na nchi na nimepewa na Mungu kuona nini nifanye katika mamlaka niliyonayo,” alisema.
Malumbano kati ya Ndugai na Zitto yalianza mapema wiki hii baada ya kiongozi huyo wa ACT–Wazalendo kudai kuwa Bunge limewekwa mfukoni na Serikali wakati alipotoa maoni kuhusu ripoti mbili za Kamati ya Bunge kuhusu biashara ya madini ya almasi na tanzanite.
Kutokana na kauli hizo, Ndugai, aliagiza Zitto ahojiwe na Kamati ya Maadili huku akimshtaki kwa wapigakura wake kuwa licha ya mbunge wao kuwapo nchini, lakini hajafika bungeni kuwawakilisha na yeye (Spika) hana taarifa.
Ndugai alisema bungeni kuwa ana uwezo wa kumpiga marufuku Zitto kuzungumza hadi miaka yote mitano iishe na hana pa kwenda, hawezi kuuliza swali la nyongeza wala kuzungumza na hakuna atakachoweza kumfanya.
Lakini Zitto alimjibu kupitia ujumbe alioutuma katika akaunti yake ya Twitter akisema: “Nimegundua Spika Ndugai ameibua mashtaka yangu ili kufunika ufuatiliaji wa wananchi kuhusu (Tundu) Lissu kupigwa risasi. Nimeamua sitawapa hilo.”
Septemba 27, mwaka huu, Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alipigwa risasi kati ya 28 hadi 32, mjini Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge na sasa uko Nairobi nchini Kenya akitibiwa.
Taarifa hii imeandikwa na Evans Magege na Aziza Masoud
Pole sana kwa mkasa uliokukuta
Normally I don’t learn article on blogs, however I wish to say that this write-up very forced me to take a look at and do it!
Your writing taste has been amazed me. Thanks, quite nice article.