Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Shirika la Sauti ya Jamii Kipunguni kwa kushirikiana na Shirika la Kaya wameanza kampeni ya kuelimisha wananchi kujiandikisha kwenye sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu.
Akizungumza wakati wa kampeni hiyo inayofanyika nyumba hadi nyumba, Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Seleman Bishagazi, amesema sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa wapinga ukatili wote kwa sababu zinahitajika takwimu mbalimbali ili kujenga hoja.
“Sauti ya jamii Kipunguni tumeunganisha nguvu na shirika la kaya kwa kujitolea bila malipo kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba, kuhamasisha wanajamii kuwa tayari kuhesabiwa,” amesema Bishagazi.
Amesema kwa Kata ya Kipunguni sensa ina umuhimu wa kipekee kwa sababu iliyofanyika mwaka 2012 kata hiyo haikuwepo ilikuwa mtaa kwenye Kata ya Kivule kabla ya kugawanywa.
“Kwa takwimu za sensa ya mwisho Kipunguni inasomeka kivule, sensa ya mwaka huu itatusaidia kupata taarifa kamili za Kata ya Kipunguni peke yake,” amesema.
Bishagazi amesema lengo la kampeni hiyo ni kufikia nyumba 350 na kuitaka jamii kuzingatia elimu inayotolewa ili waweze kushiriki vema kwenye zoezi hilo.