24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Nyuma ya kifo cha Rais Nkurunziza mtikisiko, gumzo kuhusu mafao yake

MWANDISHI WETU Na MASHIRIKA

KUSHINDWA kupata mtu wa kushika wadhfa wa urais kwa wakati baada ya kifo cha Rais Pierre Nkurunziza ni dalili mojawapo kwamba, kuondoka kwa kiongozi huyo aliyetawala Burundi kwa miaka 15 kumeacha mtikisiko.

Wakati kukiwa na hali hiyo ya sintofahamu, juzi siku takribani tatu baada ya kifo chake, Baraza la Mawaziri nchini Burundi lilimesema litaongoza nchi hiyo hadi rais mpya atakapoapishwa.

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya kufanyika kwa mkutano siku ya Alhamisi chini ya uongozi wa Makamu wa Rais wa kwanza Gaston Sindimwo.

Bado haijabainika ni lini kiongozi mpya ataapishwa, japo katiba iko wazi kuwa Spika wa Bunge la kitaifa, Pascal Nyabenda alitakiwa kuapishwa kushikilia wadhifa wa Rais kwa kipindi cha mpito hadi Rais Mteule atakapoapishwa rasmi kuchukua hatamu ya uongozi.

Wakati hali ikiwa hivyo ziliibuka taarifa ambazo hazikuwa zimethibitishwa zikieleza kwamba Rais Mteule, Jenerali Évariste Ndayishimiye, pia ni mgonjwa.

Hadi sasa baada ya kifo cha Rais Nkurunziza ni mke tu wa rais huyo mteule ndiye aliyepigwa picha akitia saini kitabu cha maombolezo na Ndayishimiye mwenyewe hajaonekana hadharani.

Chama cha mawakili nchini Burundi tayari kimetoa wito wa kuapishwa mara moja kwa rais mteule.

Tovuti ya binafsi pamoja na vyombo vingine vya habari vimesema kuwa mawaziri waliifahamisha mahakama hiyo kuhusu nafasi iliyo wazi katika ofisi ya rais.

Mahakama ya Katiba sasa inasubiriwa kutoa uamuzi ni nani anastahili kuapishwa kuwa rais.

Kwa mujibu wa katiba, Spika wa Bunge, Pascal Nyabenda, anatakiwa kuapishwa kama kiongozi wa mpito.

Hata hivyo, Evariste Ndayishimiye wa chama tawala cha CNDD-FDD aliyechaguliwa Mei 20 anatakiwa kuapishwa mwezi Agosti.

Rais wa zamani, Sylvestre Ntibantunganya, ametoa wito Ndayishimiye aapishwe mara moja kama rais wa Burundi.

Wakati huo huo kundi la upinzani linataka uchaguzi ufanywe upya.

 Wapinzani wamekuja na hoja hiyo katika wakati ambao bado kuna mshtuko mkubwa wa kifo cha Nkurunziza.

Tayari Serikali ya nchi hiyo imetangaza siku saba mfululizo za maombolezo kwa ajili ya kumuenzi kiongozi huyo aliyeliongoza taifa hilo la Afrika Masharkiki kwa miaka 15 akitokea kupigana msituni.

Ni wazi kwamba mshtuko huo unatokana na ukweli kwamba Rais huyo amefariki akiwa madarakani, akimalizia muda wa mwisho wauongozi wake, baada ya kupata mrithi wa kiti hicho kutokana na uchauzi uliofanyoika Mei 20 mwaka huu.

Katika uchaguzi huo, Domicien Ndayizeye kutoka chama tawala cha CNDD-FDD aliibuka mshindi na kwa mujibu wa katiba ya Burundi, alitakwia kuapishwa rasmi Agosti mwaka huu na kuchukua rasmi madaraka ya urais kutoka kwa Nkurunziza.

Kifo cha Nkurunziza kinatokea wakati nchi hiyo ikiendelea kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona, lakini kukiwa hakuna hatua zozote maalumu zinazochukuliwa baada ya utawala wa Nkurunziza kuwataka wananchi wake waendelee na shughuli zao bila hofu kwa kuwa Mungu ndiye mlinzi wao.

AACHA KITITA CHA BIL 11

Nkurunziza amefariki dunia huku akiacha kitita kizito ambacho kiliidhinishwa na bunge la nchi hiyo kama marupurupu yake atakapostaafu, pamoja na cheo cha juu kabisa cha “Kiongozi Mkuu” ambacho kilishaandaliwa kwa ajili yake.

Februari mwaka huu, Bunge la Burundi liliidhinisha sheria inatakayompa rais mstaafu kitita cha faranga bilioni za Burundi sawa na Dola laki 5 za Marekani (ambazo ni karibu Sh bilioni 11.5 za kitanzania). Upinzani ulilalamika ukisema fedha hizo ni nyingi mno.

Muswada huo wa sheria pia ulimwezesha kulipwa mshahara wake katika kipindi chote cha maisha yake, kupata marupurupu yote anayopewa makamu wa rais aliyeko madarakani  na kupewa nyumba ya kifahari, anayopewa kila rais wa Burundi aliyechaguliwa kidemokrasia.

Katika marupurupu na ulinzi kwa rais huyo, Bunge la Burundi lilipitisha pia azimio la kuhakikisha kuwa kwa kipindi cha miaka saba atachukuliwa kama mwenye cheo cha Makamu wa Rais na baada ya miaka hiyo atakuwa na cheo cha mbunge kwa miaka yake yote atakayoishi duniani.

Kiongozi wa upinzani Agathon Rwasa alijitokeza na kusema fedha hizo ni nyingi lakini kulikuwa na umuhimu ili asiwe na nia ya kurudi kugombea. 

MARUPURUPU MENGINE KWA RAIS MSTAAFU

Chini ya utaratibu huo, Nkurunziza alipewa haki ya kupatiwa magari sita na madereva saba huku yeye na familia yake, yaani mkewe na watoto watapewa hati za kusafiria za kidiplomasia.

Muda mfupi baada ya Bunge kupitisha utaratibu huo Februari mwaka huu, Waziri wa Sheria wa Burundi, Aime Laurentine Kanyana alisema kuwa sheria hiyo itamuhusu rais aliyepo na watangulizi wake walioingia madarakani bila njia ya mapinduzi ya kijeshi.

“Tumesema sheria hiyo haiwahusu walioingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi. Tangu 1962 sera iliyoanzishwa na Mwanamfalme Rwagasore, ilikuwa ya uchaguzi. Hivyo hapangekuwepo na wanaokwenda kinyume isipokuwa kwa maslahi yao,” alisema Laurentine

Kiongozi wa upinzani, Agathon Rwasa ambaye pia alikuwa Naibu Spika wa Bunge alisema huenda chama tawala chenye wingi wa wabunge kilikusudia kuepusha kumpa maisha mazuri rais baada ya kustaafu ili asiwe na nia ya kugombea tena.

Rwasa, mwanasiasa wa upinzani aliongeza kuwa usalama wa nchi ni muhimu kuliko marupurupu.

Muda mfupi baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo, Baraza la Mawaziri la Serikali liliibuka na kutangaza Rais Nkurunziza kama kiongozi kinara wa uzalendo.

Ni rais Melchior Ndadaye, aliyeuawa mwaka 1993 na Pierre Nkurunziza wenye vigezo vya kupewa marupurupu hayo.

HALI YA FAMILIA YA NKURUNZIZA

Kumekuwa na taarifa za kutatanisha katika mitandao ya kijamii kuhusu hali ya afya ya familia ya Rais Nkurunziza.

Mkewe, Denise Bucumi Nkurunziza (50) ambaye alisafirishwa kwa ndege kutoka Bujumbura hadi Nairobi Mei 28 kutibiwa ugonjwa ambao mpaka sasa haujawekwa wazi tayari ameripotiwa kuondoka hospitalii jijini Nairobi saa chache baada ya kifo cha mumewe siku ya Jumanne.

Maofisa katika ofisi ya rais nchini Burundi walipinga ripoti kwamba Denise Nkurunziza alipelekwa Nairobi kutibiwa virusi vya corona.

Denise ambaye ni mama wa watoto watano na ofisa wa zamani wa uhamiaji, alipata umaarufu nchini Burundi kutokana na wakfu wake wa ‘Buntu’ pamoja na miradi ya kusaidia wanawake.

Serikali ya Burundi pia imekanusha madai kuwa mama mzazi wa Rais Pierre Nkurunziza amefariki.

NKURUNZIZA

Pierre Nkurunziza amekuwa mwanasiasa wa Burundi na kuwa madarakani tangu mwaka 2005.

Nkurunziza, kijana wa aliyekuwa mbunge, alinusurika mauaji 1993 ya wanafunzi wa Kihutu katika Chuo Kiuu cha Burundi ambapo alikuwa mhadhiri na kujiunga na waasi wa FDD kundi ambalo baadae lilibadilika na kuwa chama tawala cha CNDD-FDD ambacho alikuja akawa kiongozi.

Alikuwa mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD-FDD, hadi alipochaguliwa kama rais wa Burundi.

Baada ya makubaliano ya Amani ya Arusha kati ya serikali na waasi, Nkurunziza alitajwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kabla ya Bunge kumchagua kama rais Agosti 2005.

Mwaka 2015, Nkurunziza alichaguliwa katika uchaguzi uliokuwa na utata na chama chake kwa muhula wa tatu madarakani.

Wafuasi wake na wanaompinga Nkurunziza walishindwa kukubaliana ikiwa ilikuwa halali kwake kugombea tena na maandamano yakafuata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles