29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Nyota Chelsea atumia dakika 9 kuiua Stars

pICHANA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
NYOTA wa Chelsea anayecheza kwa mkopo Fiorentina, Mohamed Salah, alitumia dakika tisa juzi usiku kuiongoza timu yake ya Taifa ya Misri kuiua Taifa Stars mabao 3-0.
Stars iliweza kuhimili vishindo vya Misri kwa takribani dakika 60 za mwanzo za mchezo huo wa Kundi G, kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2017 nchini Gabon.
Lakini Salah, aliyekuwa nyota wa mchezo huo, aliweza kupiga kona safi dakika ya 60 iliyozaa bao la kwanza lililofungwa na beki wa Sporting Lisbon, Rami Rabia, aliyetumia uzembe wa kipa Deogratius Munishi ‘Dida’.
Dida alitokea vibaya mpira huo wa kona na Rabia alikwenda juu hewani na kupiga kichwa kilichojaa wavuni.
Makali ya Salah yalizidi kuitesa Stars, hasa upande wa kushoto wa beki, Oscar Joshua, ambaye dakika ya 65 alifanya uzembe wa kumpasia adui.
Misri ilitumia vema nafasi hiyo na kuandika bao la pili lililofungwa kwa kichwa na mshambuliaji wa Zamalek, Basem Morsi, kufuatia pasi safi ya juu ya Salah.
Bao la tatu la Misri lilifungwa na Salah dakika ya 69, baada ya kugongeana vizuri na Mohamed Elneny na winga huyo kuunyanyua mpira juu (chipping) uliopishana na Dida na kujaa wavuni.
Kipigo hicho kinaifanya Stars kuburuta mkia Kundi G, linaloongozwa na Misri, Nigeria ikifuatia baada ya kuifunga Chad mabao 2-0, inayokamata nafasi ya tatu.
Stars inakabiliwa na mechi ngumu Jumamosi hii ya kufuzu Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) dhidi ya Uganda ‘The Cranes’, itakayofanyika kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar.

Makocha watema cheche
Kocha mkongwe nchini, Abdallah Kibadeni ‘King’, aliliambia MTANZANIA jana kuwa hakuna kocha mgeni atakayeweza kuisaidia Stars kutoka kwenye mfumo huu wa soka uliopo nchini.
“Mimi tokea inaondoka nchini hapa nilijua haiwezi kuifunga Misria kwao, kama ingetokea ingekuwa ni maajabu ya Mungu.
“Kocha wa Stars, Mart Nooij, hawezi kutusaidia chochote, anastahili kufukuzwa kutokana na mwenendo mbaya wa timu na kocha siku zote anahukumiwa kutokana na matokeo ya uwanjani,” alisema.
Kocha huyo wa zamani wa Simba alisema kitakachoiokoa Stars kwa sasa ni makocha takribani watatu wazawa kuwekwa pamoja na kufanya kazi ili kuiokoa Stars.
Akizungumzia mechi ijayo dhidi ya Uganda, alisema: “Tunaweza tukafanya vizuri kwenye mechi, cha muhimu ni kujipanga tu kwani Uganda ni timu ambayo hatujazidiana sana.”
Naye kocha Fred Minziro hakutaka kuzungumza sana na kusema kwa ufupi kuwa: “Misri ni timu ya kiwango cha juu, tulistahili kufungwa, cha msingi kilichobakia ni kujipanga kwa mechi zinazokuja, kwani bado mechi zipo nyingi.”

DRFA nao wapasuka
Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), nao wamepokea kwa masikitiko matokeo hayo, huku wakibainisha kuwa benchi la ufundi la timu hiyo lazima liangaliwe upya.
Mwenyekiti wa DRFA, Almasi Kasongo, alisema jana: “Naamini kuwa kikosi hicho kina wachezaji wazuri na wenye uwezo, lakini wamekuwa wakikosa mbinu za kufanya vizuri kwenye timu ya Taifa, hasa kwenye safu ya ushambuliaji, ikilinganishwa na uwezo wanaouonyesha kwenye michuano ya ligi wakiwa na klabu zao.”

Hata hivyo, Kasongo amesema licha ya Stars kuanza vibaya, bado nafasi ipo ya kujipanga upya na kwa kuanzia lazima uwezo wa benchi la ufundi uangaliwe upya.
“DRFA inaamini kuwa TFF ina uwezo wa kutafuta mwarobaini wa kutibu tatizo la matokeo mabaya kwa Starz, bila kumuonea mtu aibu,” alimalizia Kasongo.

Kocha wa Stars, Mart Nooij, mpaka sasa ameiongoza Stars kwenye mechi 17, imefungwa mechi nane, sare sita na ushindi mechi tatu, yakiwa ni matokeo mabaya sana kwenye rekodi yake, tofauti na watangulizi wake, Jan Poulsen na Kim Poulsen (wote raia wa Denmark) na Mbrazil Marcio Maximo.
Wakati huo huo, Stars inatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam leo ikitokea Misri.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, kikosi cha Stars kitawasili jijini saa 7 mchana kwa Shirika la Ndege la Ethiopia.

Baada ya kuwasili, timu hiyo inatarajiwa kuelekea visiwani Zanzibar kati ya Alhamisi na Ijumaa tayari kwa mchezo wao dhidi ya Uganda wa kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), uliopangwa kufanyika Juni 20, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles