31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

NYONGO ‘AITUMBUA’ KAMPUNI YA KUCHAKATA MADINI BATI ISIYO NA LESENI

Na Veronica Simba, Kagera

Serikali imeifungia Kampuni ya kuchakata Madini Bati ya African Top Minerals, iliyopo Kyerwa mkoani Kagera kwa kutokuwa na leseni ya kufanya shuguli hizo.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amemwagiza mmiliki wa kampuni hiyo, Hassan Ibar kutoendelea na kazi hiyo hadi pale atakapofuata taratibu za kuomba na kupatiwa leseni halali ya Serikali.

Nyongo ametoa agizo hilo jana akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kagera ambapo pamoja na mambo mengine alikagua kampuni hiyo na kutembelea maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kyerwa zinakofanyika shughuli za uchimbaji madini ya bati na viwanda kadhaa vya uchakataji madini hayo vikiwamo vya TanzaPlus Minerals na Hamad Mine Scale.

“Serikali inapenda wawekezaji wawepo ili pamoja na mambo mengine wasaidie upatikanaji wa ajira kwa wananchi lakini kamwe haitaridhia mtu yeyote kufanya uwekezaji bila kuwa na leseni halali ya kutambuliwa na Serikali na kulipa kodi zote stahiki.

“Naomba utambue kuwa unafanya shughuli hii kinyume cha sheria, hivyo naagiza, kuanzia sasa usiendelee na kazi hadi pale utakapokuwa na leseni,” amesema Nyongo.

Akizungumza na wana kikundi wa Umoja wa Wachimbaji Kyerwa, Nyongo amewasihi wawe wavumilivu wakati Serikali ikishughulikia suala la kujisajili na mikataba ya kimataifa itakayowezesha kutambulika kwa Madini ya Bati yanayochimbwa nchini ili yaweze kuuzwa popote duniani.

“Natambua mnapitia kipindi kigumu kutokana na zuio tuliloweka la kutouza madini ghafi nje ya nchi. Serikali inashughulikia suala hilo haraka ili kama nchi nasi tuweze kuingia katika mikataba hiyo ya kimataifa ambayo itatuwezesha kuleta wawekezaji kununua madini yetu kwa ushindani na tuuze kwa bei nzuri zaidi tofauti na ilivyo sasa,” amesema.

Hata hivyo, Naibu Waziri aliwataka wachimbaji hao kuachana na suala la utoroshaji wa madini na kuyauza kwa njia za magendo huku akionya kwamba, yeyote atakayekamatwa, atawajibika kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles