30 C
Dar es Salaam
Saturday, June 10, 2023

Contact us: [email protected]

NYONGEZA MISHAHARA YATINGA BUNGENI

Na GABRIEL MUSHI – DODOMA


WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sixtus Mapunda (Mbinga Mjini) na Musa Sima (Singida Mjini), wameitaka Serikali kutoa kauli juu ya lini mishahara kwa watumishi itapandishwa.

Kauli za wabunge hao zimekuja siku moja baada ya Rais John Magufuli, kusema Serikali yake itapandisha mishahara kabla muda wake wa kukaa madarakani haujaisha.

Magufuli alitoa kauli hiyo kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa Iringa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), kumwomba kupandisha mishahara kwa watumishi.

Jana bungeni, baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, wabunge hao walisimama na kuomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Change, aliyekuwa akiongoza kikao cha asubuhi.

Wabunge hao, waliomba mwongozo huo wakipitia majibu yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, kuhusu mipango ya Serikali kupunguza umasikini aliyoyatoa wakati wa kipindi cha maswali na majibu.

Akiomba mwongozo wake, Mapunda, alisema katika swali lililoulizwa na Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko (CCM), majibu ya Serikali kwa ujumla wake yalijikita kwenye kuondoa umasikini wa kipato.

Alisema umasikini wa kipato una uhusiano wa moja kwa moja na ongezeko la mishahara ya watumishi wa Serikali wa kada zote.

“Kwa kuwa jana Rais ‘aliji-commit’ kuwa ongezeko la mishahara pamoja na mambo mengine litazingatia hali halisi ya uchumi, uwezo wa Serikali kulipa na mahitaji halisi ya Serikali, na kwa kuwa Rais ‘ameshaji-commit’ kuwa kutakuwa na ongezeko la mishahara litakalozingatia mahitaji ya msingi, Serikali inatoa kauli gani, lini mishahara hiyo itapanda maana hili suala ni kama lipo hewani na limeacha sintofahamu nyingi kwa wananchi?” aliuliza Mapunda.

Kwa upande wake, Sima, aliomba mwongozo kwa mwenyekiti huyo kwa kueleza kuwa Dk. Kijaji anatoa majibu kuhusu miongoni mwa hatua za kuondoa umasikini Tanzania, lakini hakuweza kuonyesha nyongeza ya mishahara kwa watumishi.

“Sasa nimpongeze Rais kwa hotuba yake ya Mei Mosi, lakini ni vizuri kama Bunge tukahitaji kusikia ‘commitment’ ya Serikali kwa ajili ya watumishi, ni lini Serikali itahakikisha inapandisha mishahara ya watumishi hawa kama hatua mojawapo ya kuondoa umasikini?” aliuliza Sima.

Akijibu miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Chenge, aliitaka Serikali kujipatia nafasi nzuri ya kujielezea na kuwapa matumaini wananchi.

 

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,409FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles