29.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Nyoka huwa waoga kwa binadamu, wapo wanaozaliwa na ulemavu

MWANDISHI WETU

KWA kawaida nyoka hutazamwa kwa hatari kubwa, werevu na mara nyingine hata kuhusishwa na imani potofu za kichawi katika baadhi ya jamii za Kiafrika.

Kwa kawaida, nyoka anakuwa juu ya orodha ya mambo ambayo huogopwa na watu wengi maishani.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kila mwaka maelfu ya watu duniani hufariki dunia kutokana na kuumwa na nyoka wenye sumu kali.

Ukosefu wa matibabu na hata matibabu mabaya hufanya vifo hivyo kutokingika.

Kuumwa na nyoka huenda kusionekane kuwa janga baya la kiafya, lakini katika maeneo mengine duniani ni hatari kila siku na huenda kukasababisha maafa ama hata kubadilisha maisha ya mtu.

Pengine ndio sababu ya kuwapo dhana tofuati, baadhi potofu, kuhusu wanyama hawa.

Ukweli kuhusu kutambaa katika mawe na kamba

Ukweli ni kwamba, nyoka wanaweza kutambaa juu na hata chini ya mawe, kwenye miti na majengo. Nyoka hupenda kujificha ardhini.

Ni rahisi kwao kujificha chini ya vichaka, na vigumu kutambaa chini ya mawe madogo katika bustani.

Ili kuzuia uwapo wa nyoka katika eneo unaloishi, ni vema kuzikata nyasi ziwe ndogo na kuondoa masalio yoyote ya nyasi zilizokatwa au majani makavu yalioanguka na kujikusanya.

Kadhalika, ni kuondoa sehemu za mti zilizoanguka juu ya paa au zinazoning’inia katika nyumba yako.

Akizaa hutelekeza mtoto

Nyoka anapozaa au kutaga mayai, huwa na kawaida ya kuwatelekeza watoto na kuwaacha kivyao.

Nyoka huwa na tabia ya kuondoka mahali mara anapozaa, ikitokea umewaona pamoja nyoka mtoto na mkubwa, basi hiyo ni kwa bahati mbaya.

Hivyo, wale wanaoona mtoto wa nyoka katika maeneo wanayoishi, wasidhani kwamba mama mtu yupo karibu, la hasha! ni kwamba amezaliwa akatelekezwa na hivyo kujikuta akitangatanga bila wazazi.

Ngozi zao ni nyororo

Kawaida, watu ambao hawajawahi kumgusa nyoka hudhani kwamba wanyama hawa huteleza ukiwagusa. Ngozi ya nyoka huonekana kuwa kavu, lakini ukiigusa huwa ni nyororo.

Waoga

Nyoka wanatabia ya kuogopa binadamu zaidi ya binadamu wanavyowaogopa wao. Wameumbwa na haya au aibu, ndio maana huwa na tabia ya kujificha wasionekane.

Ikitokea ameshindwa kujificha au ametishiwa, kama ilivyo kwa kiumbe chochote, hushambulia kwa lengo la kujilinda.

Lakini mara nyingi baadhi yao huona afadhali kutoroka kuliko kushambulia.

Kutaga mayai

Licha ya kwamba reptilia wengi hutaga mayai, si nyoka wote wanaotaga. Baadhi yao kama wawale wa Oriental Vine, huzaa nyoka wadogo.

Sumu ya yake ni dawa

Nyoka mwenye sumu kali zaidi duniani anatajwa kuwa suluhisho la kupatikana kwa dawa ya kupunguza uchungu.

Wanasayansi wanamtaja nyika anayejulikana kwa jina la ‘Blue Coral’ ndiye mwenye sumu kali zaidi na hupatikana zaidi Kusini Mashariki mwa Bara la Asia. Utafiti uliochapishwa katika Jarida la Afya la Toxin, unasema nyoka huyo huwalenga maadui wake ambao husababisha uchungu kwa binadamu.

Wanasayansi wanasema huenda sumu hii ikatumika kutengeneza dawa ya uchungu. Baadhi ya wanyama ambao sumu yao imetumika kutengeneza dawa ni pamoja na konokono wa baharini na buibui wenye sumu.

Wanasayansi sasa wanataka nyoka huyo kuhifadhiwa hususan baada ya maeneo mengi anakopatikana kugeuzwa kuwa mashamba ya michikichi. Wanasayansi hao walifanya utafiti wao katika nchi za China, Singapore na Marekani.

Wanasema japo kwa mwanadamu nyoka huwa adui, lakini huyu huenda akawa suluhu la matatizo mengi ya kiafya.

Nyoka mwenye macho matatu

Hivi majuzi, maafisa wa wanyamapori nchini Australia walisambaza picha za nyoka mwenye macho matatu, aliyepatikana katikati ya barabara, kaskazini mwa nchi hiyo.

Shirika la huduma kwa wanyamapori na bustani za wanyama, Northern Territory Parks and Wildlife Service, wanaeleza kwamba nyoka huyo ambaye picha zake zilisambaa katika mitando ya kijamii ni wa kustaajabisha.

Amepewa jina la Monty Python, ambapo nyoka huyo aina ya chatu, alifariki wiki kadhaa tu baada ya kugunduliwa Machi, mwaka huu.

Nyoka aliyezaliwa na ulemavu, akiwa na macho matatu

Wataalamu wanasema jicho la tatu la nyoka huyo lililo juu ya kichwa chake limeonekana kuwa ni mabadiliko ya asili.

Maafisa walimgundua nyoka huyo katika mji wa Humpty Doo, kilomita 40 Kusini Mashariki mwa Darwin.

Wakizungumza na BBC, maafisa hao walisema kuwa nyoka huyo alikuwa na urefu wa inchi 15 na alikuwa akipata tabu kula chakula kutokana na ulemavu wake.

Shirika hilo la huduma kwa wanyamapori limesema picha za X-ray zimeonyesha kwamba hakuwa na vichwa viwili kwa pamoja.

“Badala yake alionekana kuwa na fuvu moja la kichwa na jicho la ziada hivyo, alikuwa na macho matatu yanayofanya kazi sawasawa,” wanasema maafisa hao.

Mtaalamu wa nyoka, Profesa Bryan Fry, anasema mabadiliko ya maumbile ni sehemu ya kawaida ya kuumbwa.

“Kila mtoto hupitia mabadiliko ya kiwango fulani – huyu alishuhudia mabadiliko yasiyo ya kawaida,” anasema Profesa Fry, kutoka Chuo Kikuu cha Queensland.

Anaongeza: “Sijaona nyoka mwenye macho matatu awali, lakini tumeona chatu mwenye vichwa viwili katika maabara yetu, ni aina tofuati ya mabadiliko kama tunavyoona kwa pacha wachanga wanaozaliwa wakiwa wameungana.”

Anaashiria kwamba huenda jicho hilo la tatu likawa sehemu ya mwisho ya pacha wa nyoka huyo aliyefyonzwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles