23.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 20, 2021

Nyerere, Magufuli hata vikwazo walivyopitia vimeshabihiana

 KATIKA awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, kuna mambo mengi yamejiri ikiwamo dhana kwamba kiongozi huyo anafanana na Rais wa awamu ya kwanza, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Mfanano unaoaminika kujikita kwenye uwajibikaji wao kwa lengo la kuliletea taifa mapinduzi ya kiuchumi.

Wahenga walisema, “Ndege wafananao huruka pamoja” Hata Mwandishi Joseph M. Rugashoborola, katika kitabu alichoandika kiitwacho Kongozi Wetu mwaka 2020, anaelezea mengi kuhusu uongozi, kiongozi na jinsi ilivyo muhimu kwa jamii kutoa uzito stahiki kwa mchakato wa kupata kiongozi.

Tafiti zinaonesha kuwa, mafanikio ya taasisi ama taifa yanategemea kwa kiasi kikubwa tabia za mtu mwenye dhamana ya kufanya uamuzi unaohusu taasisi ama taifa husika. Kiongozi akikosa sifa ni vigumu walio chini yake kutekeleza wajibu wao.

Makala ya leo, inaangazia namna ambavyo viongozi katika vyakati tofauti na zama tofauti wamepitia vikwazo ambavyo kwa kiasi kikubwa vinafanana, uzoefu unaonesha kuwa, viongozi wenye sifa zinazofanana hata kama wangepishana kwa nyakati za miaka mia moja, lakini vikwazo ambavyo hupitia katika kutoa uongozi hufanana kwa kiasi kikubwa kulingana na nyakati za wakati huo.

Kwa sasa, si jambo la ajabu kusikia ama kuona wananchi wakimfanananisha Rais wa awamu ya tano, Dk. Magufuli na Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, katika nyanja za kiuchumi hasa ndoto za ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwamo mradi wa stiegglers Gorge uliopewa jina la mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, ambalo lilikuwa kwenye ndoto za Mwalimu na sasa katika awamu ya tano inatekelezwa.

Licha ya hilo, pia ndoto mbalimbali za Mwalimu zimeendelea kutekelezwa katika awamu hii, ikiwamo mpango wa kuhamia Dodoma, ambapo ilishapangwa tangu mwaka 1973. Pia hata kauli mbiu ya sasa ya Hapa Kazi Tu, ni mwendelezo wa hotuba za Mwalimu ikiwamo, Uhuru ni kazi ya Mei 01, 1974 katika sikukuu ya wafanyakazi, kila mtu afanye kazi ya Juni 25, 1976 kwa viongozi wa chama na serikali Mkoa wa Dar es Salaam katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Heshima ya mtu ni kazi mwaka Julai 27, 1967, kwenye mkutano mkuu wa NUTA. Hivyo, kutokana na kufafana huko kwa viongozi hawa wawili wa zama tofauti ni wazi kabisa kuwa hata changamoto wanazopitia pia zinafanana.

Mathalani, kipindi cha Azimio la Arusha mwaka 1967, katika kitabu cha Azimio la Arusha Maswali na Majibu chini ya Kavazi la Mwalimu Nyerere mwaka 2017, kinafafanua changamoto kadhaa ambazo Mwalimu alizipitia katika utekelezaji wa Azimio hilo, ambapo kuna swali moja ambalo kila alipozungumza na viongozi wenzie, wafanyabiashara na watu aliyewaita wenye nafuu ya maisha, alikutana nalo.

Swali hilo ni: “Maazimio haya ya Arusha kwa ujumla ni mazuri lakini je, kutimizwa kwake hakufanywi haraka mno, tena bila fikra na mipango ya kutosha?”

Mwalimu alijibu hivi; Swali hili linaweza kuwa na ukweli kidogo ndani yake. Inawezekana kweli hatukufanya au hatufanyi mipango ya matayarisho ya kutosha ili kuwezesha shabaha zote za azimio la Arusha kutimizwa.ila huo ndio wajibu wa viongozi katika chama chetu na serikalini. Ni wajibu wao kuona mipango inafanywa kuwezesha kutekelezwa vyema maazimio ya Arusha.

Mwalimu anaendelea, lakini ubaya wa swali la namna hii ni kwamba linaweza kutumiwa na mara nyingi limetumiwa, kama kisingizio cha kutotimiza Azimio la Arusha. Wenye mabenki ni miongoni mwa wale wanaotumia hila hii. Hutuuliza, “kwa nini hamkutuonya mapema ili tuanze kujitayarisha?” Mtu anaposema kuwa maazimio ya Arusha yanatimizwa kwa haraka mno maana yake nini?

Mwalimu anakazia kuwa, katika hisoria ya mwanadamu, hila hii imetumiwa mara nyingi sana kupinga mabadiliko ya maana kwa kusema; “ni mazuri, lakini……” na ni hila ambayo hutumiwa na wale ambao hawajambo na ndio wasiopenda mabadiliko. Kwa hiyo, utawasikia watu hao wakisema; “Usawa wa mwandamu ni jambo jema….lakini…”, “kutokuwa na ubaguzi wa rangi ni jambo jema……lakini…….”, “kujali hali ya masikini ni jambo jema……lakini….”. Na hatma yake ile “lakini” ndio hufaulu ila ile sehemu ya “jambo jema” huendelea kuwa jambo jema lakini haitimizwi kamwe.

Mwalimu anamalizia kwa kusema; kosa kubwa linalofanywa na nchi nyingi za Afrika ni la kutofanya mema ya dhahiri, katika kutimiza jambo ambalo limeafikiwa kwa pamoja kuwa ni jema.

Hali hiyo ya vikwazo inafanana kwa kiasi kikubwa na hali ilivyo sasa anayokumbana nayo Dk. Magufuli katika kuipeleka Tanzania kuelekea uchumi wa kati na kubana baadhi 

 ya maeneo ambapo baadhi ya watu wachache wa ndani na nje walikuwa wanufaika wakubwa, ikiwamo mikataba ya madini, kudhibiti watumishi hewa na mambo mengine mengi.

Hali hii imejidhihirisha wazi katika hotuba ya mkutano maalum wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) mkoani Mwanza Desemba 12, 2019, pale ambapo Rais alisema wazi vikwazo anavyotokumbana navyo ikiwa ni pamoja na: “…..kumekuwa na changangamoto ambazo tumekuwa tukikabiliana nazo kama Serikali katika jitihada zetu za kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi. Kusema kweli, mimi huwa sipendi sana kuzungumzia changamoto; huwa napenda kuzikabili moja moja, head on. Lakini kwa minajili ya hadhara hii, nitazitaja mbili tu.

Anaendelea, moja kubwa ni kukosekana kwa utayari, miongoni mwa baadhi ya wananchi na viongozi pia, kukubali na kuendana na mabadiliko, yaani resistance to change. Bado watu wanashindwa au wanachelewa kuelewa kuwa tupo kwenye zama mpya ambapo nia yetu kubwa ni kujenga taifa linalojitegemea kiuchumi. Hawajaelewa kwamba ni lazima tujenge nidhamu na uadilifu katika kazi na kuelekeza rasilimali zetu kwenye mikakati ya maendeleo inayolenga kuleta ukombozi kiuchumi.

Ninachokiona bado kuna uzembe, kushindwa kuchukua uamuzi na kupenda fedha za dezo ambazo hazipo. Haya yote yanatokana na mazoea ya utegemezi na kushindwa kutambua kuwa tunapojenga misingi ya kujitegemea, hatuna budi kufunga mikanda na wakati mwingine, kupata shida kwa muda ili tujitegemee.

 Hiyo ni changamoto ya kwanza kubwa. Lakini ya pili ambayo ni kubwa pia ni hujuma dhidi ya jitihada za Serikali zinazofanywa na baadhi ya watu wasioitakia mema nchi yetu. Hujuma hizi zinalenga kufifisha jitihada zetu za kujikomboa kiuchumi kwa maslahi yao binafsi. Watu hawa kamwe hawataki kuona tunadhibiti rasilimali zetu ambazo walikuwa wakizivuna na kusafirisha wanavyotaka, bila kuulizwa na mtu. Zaidi ya hapo, watu hawa hawatakubali tutekeleze miradi mikubwa ya kimapinduzi itakayoharakisha maendeleo nchini, ikiwemo Bwawa la Nyerere, SGR au Kufufua Shirika la ATCL. Wangependa tuendelee kuwategemea wao, ilihali wao wanaishi kwa kwa kutegemea rasilimali zetu.”

Katika hotuba hiyo, nia njema ya Rais imejieleza kwa uwazi na mahala ambapo anataka kuipelekea Tanzania, ila vikwazo ni vile vile kama ambavyo alikuwa akikabiliana navyo Mwalimu, “ni jambo jema … lakini…..,” lakini hii ndio imekuwa ikitumiwa na watu wasiopenda maendeleo ya nchi na wakati mwingine hata kuwavunja moyo viongozi wetu.

Mwandishi ni Said Said Nguya

Mchambuzi wa Masuala ya Siasa na Maendeleo nchini.

Anapatikana Dodoma, 0742102913.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,961FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles