31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

Nyerere alituachia silaha, ikipotea tutavuna aibu

nyerere

Na Lameck Kumbuka, Uswisi

AWALI ya yote natoa pongezi kwa uamuzi wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Rwanda chini ya Rais Paul Kagame kupitisha uamuzi wa kurasimisha Lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha nne rasmi zinazotumika nchini humo.

Hakika uamuzi wa Rwanda umekuwa chachu ya njia nyepesi kabisa kwa wanajumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwa na utambulisho wetu wenyewe (Our own Identity) yaani Lugha ya Kiswahili. Binafsi hili jambo limekuwa ndoto yangu ya siku nyingi.

Ninawiwa kuongea machache juu ya hili hasa muda huu tunaoadhimisha miaka 17 ya kumbukumbu ya kututoka baba  wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Ikumbukwe kuwa moja ya silaha ambayo Mwalimu alituachia ni umoja, utaifa na ile kuwa Watanzania kwanza kabla ya kabila, dini, itakadi  au tofauti yoyote. Hili limetupatia sifa nyingi sana, kwa kuwa nchi ambayo imeweza kuilinda amani na utulivu kwa ajili ya ustawi wa taifa letu.

Hata jengo la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lililozinduliwa hivi karibu nchini Ethiopia na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, limepewa jina la Julius Nyerere. Ni jambo la heshima kwaTanzania.

Katika safari zangu iwe kikazi, kusaka elimu au matembezi, nimekuwa nikiumia kuona kinachotuunganisha waafrika ni ‘lugha za kikoloni’ ninlazimika kuongea kiingereza, Kifaransa au Kiispaniola ili niweze kuwasiliana na mtu kutoka Ghana, Jamhuri ya Congo ama Jamhuri ya Guinea ya Ikweta.

Nakumbuka mwaka 2013 hapa mjini Geneva nilipotakiwa kuwaelekeza wageni sehemu unapofanyika Mkutano kwenye jumba la Umoja wa Mtaifa, ndugu mmoja kutoka Guinea-Ikweta, hakuelewa vizuri kiingereza, nami Kihispania changu hakikuwa kizuri.

Basi nikalazimika kumpeleka hadi ulipo mkutano kwa kuwa nisingeweza kumuelekeza. Njiani tulitembea kama bubu. Wajua namna inavyouma kukutana na mtu ughaibuni mwenye historia na utamaduni kama wa kwako lakini hamuwezi kuongea.

Leo hii kila mwenye pesa anatamani mtoto wake aongee lugha ya kiingereza, hakika ni maajabu. Naomba nieleweke; Ni muhimu na inasaidiakuongea lugha za kigeni, unafiki tupa kule. Mimi binafsi imenisaidia sana mbali na Kihangaza lugha Mama, Kiswahili ni lugha ya Taifa, lakini naongea lugha nyingine pia kama vile kiingereza, Kifaransa na kiispaniola.

Pia nimeanza kusoma lugha za Kijerumani na Kiarabu. Lakini hizi lugha zote ni ziada tu. Ninacho jaribu kuongea ni kuwa tuzalishe Taifa ambalo linajua umuhimu wa kuongea lugha nyingine lakini waringie zaidi inayowapa utambulisho. Hata uwe mahiri vipi katika kiingereza, hutakuja kamwe kuwa mwingereza.

Hata waliozaliwa Uingereza bado wanakanwa- maadamu wana muonekano wa kiafrika, Kiarabu ama Ki-Asia. Kuna mifano mingi hata ya watu maarufu wenye asili ya Afrika wanaosakata kambumbu huku Ulaya, potelea mbali mchango wao katika nchi hizo, walizozaliwa na kulelewa huko lakini jamii husika inakuwa na kigugumzi kuwatambua, kisa wana rangi nyeusi (hawana asili ya nchi hizo).

Kwa sasa namalizia utafiti ambao umehusishawatu 50 wenye Hati za Kusafiria za hapa Uswisi lakini asili yao ni Afrika na Asia na pamoja na Ulaya Mashariki na walifika Uswisi kama wakimbizi miaka mingi iliyopita.

Aidha, napenda kuwashirikisha watanzania wenzangu kuwa  matokeo utafiti huo Mungu akipenda utakamilika ifikapo mwezi Februari mwakani na utachapishwa. Je wajua kuwa kuna Wafaransa, Waswisi, Wajerumani, Wabelgiji wengi wanaoongea lugha ya Kiingereza vizuri sana lakini ukihitaji huduma yao na unaongea lugha hiyo imekula kwako.

Aidha utalazimika kuongea lugha yao ya Kifaransa ama Kijerumani ili usinyimwe huduma zao. Kama unauliza chochote katu hutaelekezwa. Yaweza kuonekana kama ukatili lakini wamefundishwa tangu utotoni kuwa lugha yao ndio bora na mgeni lazima autambue huo uthamani wa lugha yao.

Ninaandika mengi haya ndugu zangu Watanzania kwa uchungu. Tutakapozalisha taifa la watu wanaoongea hata lugha 10 za kigeni lakini wakajivunia zaidi kuongea lugha ya Kiswahili, ndio utakuwa mwanzo wa kupiga hatua.

Tuone vijana wa kike na kiume wakijivunia kuandika Kiswahili fasaha, na inapotokea wanaongea maneno mawili ya Kiswahili na kuchanganya lugha ya kiingereza basi waone aibu na nafsi yao iwasute. Lugha ya Kiswahili ni almasi kwa nchi hizi zetu na isichezewe kuanzia Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda , Burundi, Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ni vema viongozi wetu wakafahamu kuwa lugha ya Kiswahili ni ngao yetu ya kwanza kabla ya kuwaza kuunganisha sarafu wala hati ya kusafiria. Tulipotea baada ya kukubali kuvua vazi letu wenyewe, na kuazi mavazi la jirani, kila mtu anaona sio vazi letu kwani linatubana na mbaya zaidi tunaliringia bila hata aibu.

Mwandishi wa makala haya ni Mtaalamu wa Diplomasia, amewahi kuwa mshauri  wa Masuala ya sheria za Biashara wa Umoja wa Mtaifa mjini Geneva. Kwa sasa anasoma shahada ya Uzamili ya Sheria za Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Fribourg. Baruapepe; [email protected], simu; +41 76 651 6758

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles