Hadija Omary, Lindi
Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), mkoani Lindi, limezindua kampeni ya ‘Zamu Yako’ inayolenga kuwafikia watu wasio kwenye sekta isiyo rasmi.
Akizindua kampeni hiyo, katika semina ya namna ya kujiunga na mfuko huo, iliyowakutanisha viongozi wa vikundi vya wajasiriamali na vyama ushirika, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shahibu Ndemanga akizindua kampeni hiyo wilayani humo jana, amesema hatu hiyo imekuja baada ya Bunge kupitisha Sheria Mpya Namba 2 ya mwaka 2018 inayoboresha hifadhi za jamii nchini, ambapo sheria hiyo imeacha mifuko miwili ya PSSSF na NSSF.
Amesema katika mambo muhimu yaliyo katika sheria hiyo ni pamoja na msisitizo uliowekwa wa kupanua wigo wa hifadhi ya jamii kwa kuwafikia Watanzania wote wakiwemo na wale waliojiajiri wenyewe ambapo jukumu hilo limepewa NSSF.
“Kampeni ya zamu yangu inawalenga hasa watu wasio kwenye ajira rasmi, kama wajasiliamari, mama lishe waendesha bodaboda, wavuvi na wote walio kwenye kundi hilo lengo likiwa ni kuwahamasisha ili na wao waweze kunufaika na mafao yanayotolewa na mfuko huo,” amesema.
Kwa upande wake Meneja wa NSSF, Mkoa wa Lindi, Robert Kadege, amesema kampeni hiyo ni ya kitaifa ambapo kwa mkoani hapa ndiyo imezinduliwa rasmi.
“Mtu atakapojiunga na kuwa mwananchama wa hiari na kuchangia kiasi kilichopangwa cha Sh 20,000 kila mwezi atapata matibabu ya bure yeye na mwenza wake na watoto hadi wanne walio chini ya umri wa miaka 18 au 21 iwapo yupo shule,” amesema.
Alitaja manufaa mengine ambayo atayapata mwanachama huyo ni pamoja na pensheni atakapofikia wakati wa kustaafu pamoja na stahiki zote ambazo anazipata mwanachama ambaye yupo kwenye ajira rasmi huku wanachama walio kwenye vikundi vilivyosajiliwa rasmi kama SACCOS wanaweza kukopeshwa kupitia usimamizi wa Benki ya Azania kwa riba nafuu.