24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

NSSF yaleta neema kwa wanachama sekta isiyo rasmi

Mwandishi wetu – Mwanza

WANACHAMA kutoka sekta binafsi na sekta isiyokuwa rasmi ambao watajiunga na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) watanufaika na fursa mbalimbali zitakazowasaidia kukuza vipato na kujiondoa katika umasikini.

Miongoni mwa fursa zinazopatikana katika mfumo huo ni mafao ya uzeeni, matibabu na msaada wa mikopo kwa wajasiriamali.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Meneja wa Idara ya Sekta Isiyo rasmi ya NSSF, John Mwalisu, wakati wa semina kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza, iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari mkoani humo (MPC) kutambulisha kampeni ya ‘NSSF na Marafiki’.

Mwalisu alisema kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2018, ukurasa wa 50, shirika hilo limepewa mamlaka ya kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi.

Alisema tayari NSSF imesajili mfumo wa taifa wa sekta isiyo rasmi, ambao wanachama wote katika sekta isiyo rasmi wataandikishwa.

Mwalisu alitaja faida zilizomo katika mfumo huo ni mafao ambayo yamegawanywa katika awamu tatu. Mafao hayo ni fao la uzeeni, matibabu na msaada wa mikopo kwa wajasiriamali.

Alifafanua kuwa mafao ya uzeeni ni lazima mwanachama achangie katika kipindi cha miaka 15 na afikishe umri wa kustaafu wa miaka 55 kwa hiyari, na miaka 60 kwa lazima.

Kuhusu fao la matibabu, alisema shirika lipo katika mazungumzo na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ili wanachama wapya wapate matibabu kupitia bima ya afya wakati utakapofika.

Akizungumzia mikopo, alieleza kuwa wameiweka kwenye makundi matatu, na kwamba mkopo wa elimu kama mwanachama anataka kujiendeleza kielimu, anaweza kukopa kupitia benki ya Azania, lakini kwa sasa wapo kwenye mazungumzo.

Alisema kama mwanachama anataka kumsomesha mtoto wake, anaweza kukopa kupitia benki ambazo watazitangaza kwa umma muda ukifika.

“NSSF tunataka kujiondoa kwenye huduma ambazo hatuzifanyi, zikiwemo za mikopo na badala yake tubaki na shughuli za hifadhi ya jamii. Mikopo na matibabu zibaki kwenye taasisi husika,” alisema.

Alifafanua zaidi kuwa mikopo hiyo ni ya muda mfupi, lakini mwanachama atarudisha katika kipindi cha miaka minne.

Pia, alisema kutakuwa na mkopo wa kukuza mitaji ambao utakuwa unatolewa na benki ya Azania, kwamba mwanachama anatakiwa kuchangia kwa muda wa mwaka mmoja ili apate mkopo huo.

Alisema lengo la kufanya hivyo wanataka kuona shughuli za wanaojiunga na NSSF ziwe endelevu na waendelee kuchangia.

Meneja wa NSSF Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Kahensa, alisema sasa shirika hilo linakuja na kampeni ya kutekeleza sheria ya mwaka 2018 toleo namba 50 kwa kupita kwa waajiri wote.

Kahensa alisema wamepata orodha kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kampuni ambazo waajiri wake hawachangii katika shirika hilo.

Alisema kitika mkoa huo tayari wameanza kupita kwa waajiri wote kuhakikisha wafanyakazi wao wanaandikishwa na kuchangia NSSF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles