NONDO APATA DHAMANA, AWASHUKURU WATANZANIA KWA KUMUOMBEA

0
701

Na Francis Godwin, Iringa

Dhamana ya Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP), Abdul Nondo imekubaliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, baada ya kutimiza masharti kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh milioni tano.

Mahakama hiyo imetoa uamuzi huo leo baada ya Nondo kutimiza masharti hayo yaliyomtaka kuwa na wadhamini wawili ambao ni wakazi wa Iringa, mmoja kutoka serikalini na mwingine sekta binafsi watakaosaini bondi ya Sh milioni tano.

Baada ya kuachiwa huru na mahakama hiyo, Nondo amesema “Nawashukuru Watanzania kwa kuniombea na waandishi wa habari kwa kutoa taarifa zangu, naamini nitawahi kufanya mitihani itakayoanza chuoni kesho”.

Aidha, mawakili wake Jebra Kambole na Charles Luoga, wameishukuru mahakama imetenda haki kwa kutoa dhamana kwa mteja wao na kuahidi kuendelea kumpigania.

Nondo alifikishwa mahakamani hapo Machi 21, na kusomewa makosa mawili ya kutoa taarifa za uongo mitandaoni na kudanganya kuwa alitekwa ambapo Wakili wake Luoga, alimuomba hakimu kumpatia dhamana mteja wake kwa kuwa makosa hayo yanadhaminika lakini Wakili wa Serikali, Abel Mwandalamo aliiomba mahakama kukataa maombi hayo na Hakimu John Mpitanjia akaazimia kutoa uamuzi wa dhamana hiyo leo.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here