22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Nnayikaa: Mrembo wa Jux aliyefanya oparesheni kibao kutengeneza umbo, sura

BANGKOK-THAILAND

MIEZI mitatu iliyopita tovuti ya Pattaya Today ya nchini Thailand iliandika habari kubwa iliyobeba kichwa cha habari, ‘Mwanamke wa Ki-Thailand aliyekuwa ‘addicted’ na operesheni za urembo, amefanya nyingine sita kwa mara moja.

Habari hiyo ilikuwa inamzungumzia mrembo mpya anayeonekana na  staa wa RnB, Juma Musa ‘Jux’, Nnayikaa ambaye katika tovuti hiyo ametajwa kwa jina la Nayika Thongom mwenye umri wa miaka 25.

Nnayikaa, amekuwa gumzo hivi karibuni hapa Bongo baada ya Jux kuweka picha zao hadharani zikiwaonyesha wakijiachia maeneo mbalimbali nchini kama vile uwanja wa ndege, hifadhi ya Serengeti na kwenye fukwe za Nungwi huko Zanzibar, ikiwa ni muda mfupi baada ya Vanessa Mdee kuthibitisha kuwa aliachana na Jux miezi tisa iliyopita.

Taarifa mbalimbali za kwenye mitandao nchini nyumbani kwao nchini Thailand na China anakoishi hivi sasa  zinamtaja Nnayikaa kama msichana ambaye aliyewahi kuteswa na mwonekano wake wa awali hivyo kulazimika kuingia kwenye upasuaji mara kadhaa akitumia mamilioni ya fedha kutafuta mwonekano alionao sasa.

Mtandao wa habari wa nchini Thailand ambao ulipata kufanya mahojiano na Nnayikaa wa Pattaya Today, uliandika kuwa mrembo huyo aliingia kwenye operesheni nyingine sita za mara moja miezi mitatu iliyopita ili kuondoa mafuta au unene kwenye ngozi katika maeneo ya kiuno, tumbo, mapaja na eneo lililo karibu na viungo vya uzazi yaani chini ya kitovu pembeni kwa pande zote mbili.

Pia alifanya ukarabati wa pua na kuondoa ‘silicone’ (kifaa kinachokuwa na majimaji ndani) kwenye kidevu.

Picha zake akiwa kitandani hospitalini baada ya kumaliza upasuaji  huo zinamuonyesha akiwa na bandeji nyingi katika mwili wake.

Pattaya Today, imeandika kuwa; leo hii baada ya operesheni nyingi zikiwemo pia za kurekebisha uso, makalio, matiti na rangi ya ngozi  Nnayikaa ana furaha juu ya mwonekano wake mpya.

Kwa maneno yake mwenyewe amekaririwa na Pattaya Today akisema ameongeza makalio kwa sababu  mazoezi peke yake hayakuweza kumpa mwili mzuri.

 “Nilishauriana na daktari wangu na kuamua kuondoa mafuta ilikuwa ni njia sahihi kwangu kwa sababu siku zote nilitaka mwili wangu uonekane imara na unaovutia,

“Wakati mwingine lazima ukiri kwamba mazoezi hayawezi kukupa kila kitu unachotaka kwa ajili ya mwili wako.’’

Nnayikaa, ambaye kwa sasa anaishi Shenzhen, China, anasema kupenda kwake upasuaji wa plastiki  kulianza wakati akiwa mdogo.

Anasema mara nyingi alikuwa anaitwa mbaya hali iliyokuwa inamfanya apoteze raha na kujiamini.

Nnayikaa anasema tangu wakati huo amekwenda kufanyiwa upasuaji mwingi wa kurekebisha umbo la uso wake na  matiti.

Nnayikaa mwenye asili ya Surin, nchini  Thailand ambaye Pattaya Today inamtaja kama Mfanyakazi wa Chuo Kikuu  na mitandao mingine ikimtaja kama mwanamitindo anasema; “Nilikuwa mnene sana na ngozi nyeusi ambapo kila mtu alikuwa ananiita nguruwe mweusi. Wakati mmoja niliachwa na mwanaume kwa sababu tu alisema nilikuwa mbaya.’’

Nnayikaa, ambaye amesomea shahada ya udaktari wa binadamu na upasuaji katika Chuo Kikuu cha Southern Medical huko Guangzhou China, baada ya kupitia changamoto hizo anasema  ndipo alipoanza kufanya upasuaji wa plastiki kwenye pua yake na kidevu, kufanya mazoezi na kula mlo bora.

Hata hivyo alibaini kuwa vyote hivyo bado vilikuwa havimridhishi hadi pale alipoamua kufanya upasuaji wa gharama zaidi wa kuondoa mafuta ili kuupa mwili mwonekano wa bikini na unaong’aa.

Nnayikaa mwenyewe akielezea hilo anasema: “Ni vigumu mno kupata shepu nzuri kama ambayo niliitaka. Sasa nimechoka na nimetumia fedha nyingi mno katika hilo.

“Ni vigumu mno pia kubaki katika shepu hii hii. Lakini baada ya operesheni ya kuondoa mafuta, lazima niwe na nidhamu, kufanya mazoezi sana na kula vizuri, vinginevyo nitakuwa kama nilivyokuwa mwanzo.’’

UHUSIANO WAKE NA JUX

Ingawa Nnayikaa na Jux hawajaeleza lolote kuhusu uhusiano wao zaidi ya kuutambulisha kupitia picha na kuweka maelezo “No calls, texts Only..!vacation#sumaku. Vacation #sumaku#thelovealbum,” 

Pamoja na kwamba hawajaeleza lolote lakini kuna uwezekano mkubwa wawili hao walikutana China ambako mwanamuziki huyo alikuwa akisomea masuala ya sayansi ya kompyuta na wakati huo huo akifanya ubia na moja ya kiwanda nchini huo kwaajili ya kuzalisha mavazi yenye chapa, African Boy.

Nnayikaa na Jux

Mbali na wawili hao kuonekana wakila bata sehemu mbalimbali nchini, mwishoni mwa wiki iliyopita katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, walikuwa kivutio kwa wengi waliohudhulia ‘707 The Great Gatsby’, hafla ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa mama mzazi wa Diamond Platnumz na mpenzi wake Tanasha Donna.

Jux ameaonekano kujiachia zaidi na mrembo huyo tofauti na ilivyokuwa kwa Vanessa jambo ambalo limekuwa gumzo zaidi katika mitandao ya kijamii.

VANESSA ATAKA WANAOMSEMA WAACHE

Ingawa Vanessa amesikika na kuonekana katika video mpya ya Jux, Sumaku, mrembo huyo hivi karibuni kupitia ukurasa wake wa Instagram, aliwataka watu wanaomsema vibaya baada ya kuachana kwao kuacha kufanya hivyo.

 “Mimi ningependa kusema kitu kimoja hasa kwa wale wanaonitukana kwenye mitandao ya kijamii, mimi ni mtu ambaye najiheshimu, naheshimu kazi yangu na heshimu sanaa,

“Naheshimu ‘brand’ yangu ambayo nimeijenga kwa muda mrefu sana, wale wanaoanza kunitukana mimi, kusema ooh mimi malaya, mimi ni tasa, ooh nimekataa kuolewa, ooh nilikuwa namdharau Juma, msinisemee, msiusemee moyo wangu, msiusemee moyo wake,” alisema Vanessa ambaye alikuwa akijibu maswali ya mashabiki zake waliotaka kufahamu juu ya uhusiano wake na Jux.

Vannessa alisisitiza kwa sasa baada ya kuachana wamebaki kama marafiki wa kawaida.

Vanessa Mdee na Jux

Kama njia ya kuthitibisha kuwa bado ni marafiki wazuri, Ijumaa wiki iliyopita waliachia kibao walichofanya pamoja (Jux Ft Vanessa Mdee) kinachokwenda kwa jina la Sumaku ambapo video yake ilitoka Alhamisi wiki hii.

Hata hivyo Sumaku ilirekodiwa muda mrefu kabla ya kutibitisha kuachana kwao.

Hii si mara ya kwanza kwa Vanessa na Jux  kutoka hadharani na kusema wameachana.

Mwaka 2017, miezi kupita bila wawili hao kusemeshana baadaye walirudiana wakiwa kwenye jukwaa la Fiesta Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles