Na Mwandishi Wetu
BENKI yaNMB imezindua akaunti ya dhamana ya muda mrefu inayoambatana na bima ya maisha bure inayoitwa Wekeza.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi wa NMB, Filbert Mponzi amesema akaunti ya Wekeza itavutia kwa maana ina kiwango cha riba hadi kufikia asilimia 12 kwa ambao watakuwa na uwekezaji wa muda mrefu.
Amesema kiwangi hicho cha riba kitakwenda na idadi ya miaka ambayo mteja anataka kuwekeza.
“Tumeamua kuja na ubunifu huu kama ilivyo kawaida yetu lengo ni kuwafundisha Watanzania utamaduni wa kuweka akiba, ndiyo maana tumeruhusu kutoa fedha kwenye akaunti hiyo mara mbili kwa mwaka, Juni na Desemba kwa sababu tunafahamu huenda ikatokea dharura au kulipia ada za watoto.
“Mtakumbuka hivi karibuni benki yetu ilipata tuzo sita za kimataifa mmojawapo kutoka jarida la ‘International Banker’ Benki ya NMB imekuwa benki bora kwa ubunifu wa bidhaa kwa wateja binafsi.
“Tunafurahia kumudu kuwapa wateja wetu njia nyingine salama na ya muda mrefu kuhifadhi fedha, ikumbukwe tunatoa huduma katika mazingira shindani zaidi, lakini kwa mara nyingine tunathibitisha kuwa tunaweza kuendelea kuleta bidhaa mpya zinazoongeza thamani kwa wateja.
“Tunajivunia zaidi huduma yetu ya Wekeza, tumejipanga kuhakikisha tunaongeza fursa kwa wateja wetu wakati tunaendelea kuwatia moyo kujizoesha utaratibu mzuri wa matumizi ya fedha,” amesema Mponzi.
Mkuu wa Idara ya Bidhaa Benki ya NMB, Aloyce Maro amesema akaunti hiyo inatoa fursa kwa mteja kuanza kwa kuweka kiasi cha sh 250,000 ambapo ataanza kwa kupata riba ya asilimia mbili kila baada ya miezi sita.
“Mteja atapata nafasi ya kuendelea kuweka akiba katika akaunti yake kadiri awezavyo, ambapo riba itaongezeka kulingana na kiasi alichonacho. Vilevile kutakuwa na huduma ya bima ya maisha bure itakayotolewa kulingana na kiasi cha akiba iliyopo hadi kufikia sh milioni 50, itawahusu wateja waliopata kilema cha maisha au kifo,” amesema Maro.