23.2 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

NMB yatoa msaada wa Sh milioni 68 kusaidia Elimu, Afya Musoma

Na Mwandishi Wetu, Rorya

Benki ya NMB imetoa msaada wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 68 kwa ajili ya kusaidia sekta za elimu na afya  mkoani Mara msaada ambao utazinufaisha shule 11 za Msingi na Sekondari pamoja na Hospitali ya kumbukumbu ya mwalimu Nyerere maarufu Kwangwa.

Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB Juma Kimori(kushoto) akimkabidhi viti na meza 157 kwa Meya wa Manispaa ya Musoma Kapteni William Gumbo, kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya msingi Buhare, ambapo NMB imetoa mabati 750, madawati 157 kwa ajili ya shule za mkoa wa Mara na vitanda 8 vya kujifungulia kwa ajili ya Hospitali ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere. Benki ya NMB imekabidhi madawati, viti na meza kwa shule msingi na sekondari, na hospitali vyenye thamani jumla ya zaidi ya Shilingi 68 Milioni mkoani Mara ikiwa ni sehemu uwajibikaji wake kwa jamii.

Msaada huo umetolewa kwa wilaya za  Musoma na Rorya mkoani humu ambapo unahusisha madawati, vifaa vya kuezekea kwa sekta ya elimu pamoja na vitanda maalum  kwa sekta ya afya.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kukabidhi misaada hiyo katika wilaya hizo, Afisa mkuu wa fedha wa benki hiyo Juma Kimori alisema kuwa benki yake  itaendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha miundombinu ya Elimu na Afya kwa kutoa misaada ya vifaa kutokana na faida iipatayo kila mwaka.

Kimori aliongeza changamoto za sekta za elimu na afya nchini ni jambo la kipaombele kwa benki kutookana na umuhimu wa sekta hizo katika ustawi wa jamii na kwamba ingawa serikali imekuwa ikijitahidi kwa kiwango kikubwa kuboresha sekta hizo lakini bado ipo haja ya jitihada hizo kuungwa mkono.

“Sisi kama wa wadau tunao wajibu wa kuunga mkono juhudi hizi za maendeleo  kwa kusaidia jamii kwani jamii hii ndio imeifanya benki ya NMB kuwa hapa ilipo kwani ni benki kubwa kuliko yoyote hapa nchini na na tutaendelea  na kuunga mkono jituhada hizi ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na mafanikio ya hali ya juu katika sekta hizi ili ziweze kuwa mfano ndani na nje ya nchi,” alisema.


Kimori alisema kuwa kuwa benki  hiyo kwa kutambua changamoto zinazozikabili sekta za afya na elimu nchini tayari imekwishatumia zaidi ya Sh 1.88 bilioni kuanzia mwezi Januari mwaka huu  hadi sasa kuzisaidia sekta hizo ambapo kwa mikoa ya kanda ya ziwa msaada huo umezinufaisha shule na vituo vya kutolea huduma za afya 129 huku mkoa wa Mara ukiwa umepokea jumla ya madawati 587, mabati 2,580 na vitanda 8 katika kipindi hicho.

Aliwataka wananchi kutumia bidhaa mbali mbali za benki hiyo ili waweze kunufaika nazo huku Meneja wa benki hiyo kanda ya ziwa, Baraka Ladislaus akisistiza kuwa benki hiyo itaendelea kutoa misaada ya hali na mali kwa jamii ili kuboresha maisha. 

Akizungumza bada ya kupokea msaada huo mkuu wa mkoa wa Mara,  Ally Hapi aliishukuru  kwa msaada huo huku akizitaka mamlaka husika mkoani humo kuhakilisha kuwa zinaboresha taaluma ili kuongeza ufaulu.

Alisema kuwa mkoa wa Mara hauna mpango wa kuwa na makambi kwaajili ya kuwaandaa wanafunzi walio kwenye madarasa ya mitihani kutokana na ukweli kuwa hivi sasa hakuna uhitaji wa makambi hayo kwani serikali imejitahidi kupambana na changamoto za elimu ikiwemo kuajiri walimu wengi siku za hivi karibuni.

Alisema kuwa mkoa wa Mara umejiwekea malengo ili kuhakikisha kuwa taaluma inaboreshwa hasa ikizangatiwa kuwa kumekuwepo na matokeo yasiyoridhisha katika mitihani ya kitaifa kwa matokeo ya darsa la saba, kidato cha pili na cha nne.

Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara, Dk. Joachim Eyembe alisema kuwa msaada huo utasaidia kuboresha huduma zitolewazo hospitalini hapo hasa ikingatiwa kuwa mwezi ujao hospitali hiyo iliyoanza kutoa  huduma mwezi Novemba  mwa mwaka jana inapanua huduma zake kutoka huduma za mama na mtoto za sasa na kuongeza huduma za kibingwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,250FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles