27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

NMB yatoa msaada kwa vituo vya watoto yatima kufurahia Eid El Fitri

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Katika kuhakikisha watu wenye hali mbalimbali wanatoa tabasamu katika kipindi cha Sikukuu ya Eid El Fitri, Benki ya NMB imetoa msaada katika vituo vya watoto yatima kanda zote za benki hiyo nchini ambapo zaidi ya watoto 1000 katika vituo 12 nchini wamefikiwa na msaada huo.

Akizungumza katika Kituo cha Watoto Yatima Ijango Zaidia kilichopo Sinza jijini Dar es Salaam, baada ya kukabidhi msaada huo Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu Benki ya NMB -Emmanuel Akonaay alisema Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umewakumbusha watu umuhimu wa kutoa kwa wanaomzunguka hasa wasiojiweza kwa kipato.

“Sisi Benki ya NMB tunatambua  Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaowagusa zaidi ya Waislamu bilioni 1.5 ulimwenguni ambao miongoni mwao kuna wafanyakazi wenzetu, wateja wetu, wabia, wawekezaji na wanahisa. Mwaka huu tumeona vyema zaidi kujumuika na watoto wa vituo vya Yatima  nchini kutoa sadaka hii ya mkono wa Eid,” alisema Akonaay na kuongeza:

“Dini zote, Waislamu kwa Wakristo tuna imani kuwa Mola humsaidia mtu anayemsaidia ndugu yake. Kwa maneno mengine ni kwamba, tumeumbwa ili tuwasaidie wengine na hili ndilo kusudi la uwepo wetu hapa kwenye kituo hiki cha watoto Yatima cha Ijango Zaidia cha Sinza Madukani jijini Dar es Salaam,”amesema.

Aidha, afisa huyo alibainisha kuwa sadaka hiyo ya mkono wa Eid itafanywa pia na wafanyakazi wengine wa benki ya NMB kwenye kanda zote nchini kutoa vyakula mbalimbali vikiwemo Mbuzi, mchele, mafuta ya kupikia, sukari, majani ya Chai, pamoja na vifaa vingine vya kupikia kwa ajili ya watoto kupata mlo wa Sikukuu.

“Tunatarajia kufikia vituo 12 vya watoto yatima kanda zote vikiwa na jumla ya watoto zaidi ya 1,000 na kuwapa faraja ya kusherehekea Sikukuu kama watoto wengine. Matukio haya yote ni kudhihirisha kuwa Benki ya NMB  ni sehemu ya jamii. Kwa hapa kituo cha Ijango Zaidia tunafurahia kuwa zawadi hii itaweka tabasamu kwa watoto 125.  Mwenyezi Mungu awabariki sana na niwatakie Idd Mubarak!,” alisema Akonaay.

Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Watoto Yatima, Ijango Zaidia, Zaidia Nuru alisema: “Mlichofanya ni kitu kikubwa kwa watoto hawa. Hawan wazazi sisi na nyinyi ndio wazazi wao. Hakika Mungu atawalipa kwa kila mlichotoa mkafanikiwe zaidi kwenyw shughuli mnazofanya.”

Nuru alibainisha kuwa kutoa ni moyo, zipo taasisi na mashirika mengi nchini, lakini NMB imeamua kutoa ili kuwapa tabasamu watoto yatima nchi nzima.

Kwa kuwa tukio hilo la utoaji msaada wa mkono wa Eid katika vituo vya watoto Yatima lilifanyika katika kanda zote nane za Benko ya NMB nchini, Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam na Zanzibar, Donatus Richard alisema kuwapa tabasamu wanajamii ni sehemu ya utamaduni wa benki hiyo.

“NMB ina kanda nane nchi nzima, tumetoa msaada huu wa chakula na vinywaji katika vituo 12 kwenye kanda nane nchini, hui ni utamaduni wetu. Hivyo kwa niaba ya mameneja wa kanda zote ambao leo wamekabidhi misaada kwa watoto yatima, tunawaambia tupo pamona nanyi kuhakikisha mnatabasamu,” alisema Richard.

Msaada uliokabidhiwa katika kanda zote nane katika kila kitup kati ya vituo 12 ni pamoja na Mbuzi, mafuta ya kupikia, Mchele, Juisi, Maharage, Sukari, Chumvi na Sabuni.

Sheikh wa Wilaya ya Tabora, Ramadhani Juma ambaye alishiriki hafla ya makabishiano kwa Kanda ya Magharibi alisema: “NMB mmeonyesha mfano wa kuigwa, mashirika,taasisi na watu binafsi wanatakiwa kuguswa kusaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu wakati wote.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles