29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

NMB yatoa misaada ya milioni 20 Dar

NA MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB, kupitia Program ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), imetoa msaada wa viti na meza 150 kwa shule za sekondari za Saranga ya Kimara na Mashujaa ya Sinza, pamoja na mabati 175 kwa shule ya msingi Mianzini, iliyopo Magomeni Makurumla, zote wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam, vyote vikiwa na thamani ya sh. 20 milioni.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika jana Alhamisi ya Agosti 5, 2021 katika shule ya sekondari Saranga, ambako Mkuu wa Kitengo cha Biashara za Serikali wa NMB, Vicky Bishubo, alimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Heri James, mbele ya Mbunge wa Ubungo na Waziri wa Viwanda na Biashara, Kitila Mkumbo.

Akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa hivyo, Bishubo amesema msaada huo ni sehemu ya utaratibu wao wa kila mwaka, ambako hutumia asilimia moja ya faida yao kwa mwaka uliotangulia, kurejesha kwa jamii kwa kusaidia utatuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta za Elimu na Afya, pamoja na majanga. 

Bishubo amebainisha kuwa, NMB inatambua, kuthamini na kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya vijana na watoto wa Kitanzania kupata elimu bora, hivyo wao kama wadau, wanao wajibu wa kusapoti jitihada hizo kwa kusaidia kila penye uhitaji.

“Benki yetu inatambua namna Serikali inavyopambana kuhakikisha inasukuma mbele sekta ya elimu na afya nchini, nasi NMB kila mwaka tunatenga asilimia moja ya faida yetu ili kuunga mkono jitihada hizo, ambako kwa mwaka huu benki imetenga sh. bilioni 2. 

“Hadi sasa NMB imetumia sh. bilioni 1.3 kutoa misaada kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu, ambapo kwa mkoa wa Dar es Salaam peke yake, benki imetoa misaada yenye thamani ya sh. milioni 207.9, kati ya hizo  milioni 144.5 katika elimu na milioni 93 sekta ya afya,” amesema Bishubo.

Kwa upande wake, DC James, ameishukuru NMB, aliyoitaja kama sehemu ya familia ya maendeleo wilayani mwake kutokana na ushiriki wao wa mara kwa mara wa utatuzi wa changamoto katika elimu na afya, huku akiwataka walimu na wanafunzi kutunza misaada hiyo, ili idumu kwa muda mrefu.

“NMB wamekuwa wanafamilia wa maendeleo Ubungo, tangu siku naapishwa walikuwa na sisi, naanza kazi NMB ilikuwa pamoja na sisi, tuliposimama kuhangaika na changamoto za sekta ya elimu na afya, NMB iko pamoja nasi. Wao wako na sisi katika raha na shida.

“Mahusiano yaliyojengwa na NMB pamoja na sisi wilaya ya Ubungo, ni hamasa kwa wadau wengine wa maendeleo. Kwa sasa NMB imechagua kuwa pamoja na sisi, kwani kila tunapowaza kuhusu miradi ya maendeleo ama utatuzi wa changamoto, NMB imesimama na sisi,” amesema James.

Naye Waziri Mkumbo, ameishukuru NMB kwa namna inavyomsaidia kutekeleza ilani ya chama iliyomuingiza madarakani na kwamba heshima ya wabunge wengi nchini imejengwa na kuendelea kujengwa na benki hiyo, kadri inavyojitoa kufanya utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii.

Ameongeza kuwa, Jimbo la Ubungo lina jumla ya shule za msingi 35 na sekondari 10, ambako kumekuwa na changamoto nyingi, ikiwamo upungufu wa vyumba vya madarasa na kwamba miundombinu ya shule mbalimbali wilayani mwake, zinahitaji kumalizwa kwa  sh. bilioni 14.65.

“Wito wangu kwa wadau wa elimu na maendeleo ni kuiga mfano wa NMB kwa kuikumbuka elimu wilaya ya Ubungo, kila wanapokaa na kupanga mikakati yao ya kila maka.

“Serikali pekee haiwezi kuzimaliza changamoto zinazoikabili miundombinu ya sekta ya elimu na afya,” amesema Mkumbo.

Amefafanua kuwa, katika shule hizo 35, miundombinu ni changamoto kuu, ambako kuna upungufu wa madarasa 340 yanayohitaji sh. bilioni 6.8, matundu ya vyoo 1,173 ya sh. bilioni 2.4, madawati 3,312 yenye thamani ya sh. mil. 331 na Ofisi za Walimu 36, zinazoigharimu Serikali sh. bilioni 1.8.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles