29.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

NMB yakabidhi Serikalini gawio la Sh bilioni 30.7

Na Mwanandishi Wetu, Dodoma

BENKI ya NMB jana walikabidhi Sh bilioni 30.7 kwa Serikali huku Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango akisema benki hiyo imefanya siku yake na Serikali nzima kuwa yenye furaha.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 15, 2022 jijini Dodoma, kufuatia agizo lake kwa beki hiyo mwaka jana kipindi kama hiki alipopokea gawio la Sh bilioni 20.8 ikiwa ni faida ya mwaka 2020 na kutaka waongeze nguvu na ubunifu ili waje na gawio nono.

Gawio hilo limetolewa ikiwa ni faida ya NMB kwa mwaka wa fedha ulioishia 2021 ambapo jumla ya Sh bilioni 97 zilipitishwa na mkutano mkuu wa wana hisa wa Benki ya NMB kutolewa kwa wanahisa kama gawio. Serikali ikiwa inayomiliki hisa asilimia 31.8, imepokea Sh bilioni 30.7 kama gawio lake kutoka benki ya NMB ikiwa ni ongezeko la asilimia 40 ukilinganisha na mwaka jana.

Kwa gawio hilo, Benki ya NMB ndani ya kipindi cha miaka mitano kuwa wametoa jumla ya Sh bilioni 80.544 kwa serikali.

Akipokea mfano wa hundi ya kiasi hicho, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk, Philip Mpango alisema benki hiyo imeendelea kuiheshimisha Serikali kwa kuonyesha namna gani inavyokuwa kimtaji na kuwajali wateja wake.

Hata hivyo, Dk Mpango aliagiza kwa benki hiyo kuongeza ubunifu ili iweze kuwafikia watu wengi vijijini,kuwa benki bora na kusaidia ajira kwa vijana ikiwemo utunzaji mazingira.

“Hata nitakapokwenda kumpokea Mheshimiwa Rais, hili litakuwa ni jambo la kwanza kumuambia, moyo wangu umeburudika sana, mmenifurahisha sana nasema hongereni sana,” amesema Dk. Mpango.

Akitoa taarifa yake kwa Makamu wa Rais, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema faida ya Benki baada ya kodi katika kipindi cha 2021 iliongezeka kwa asilimia 41 hadi kufikia Sh bilioni 290.

Kiasi hicho ni kikubwa ukilinganisha na Sh bilioni 206 ya mwaka 2020 ambapo idadi ya idadi ya akaunti za wateja iliongezeka hadi kufikia milioni tano ikilinganishwa na milioni nne za 2020.

“Katika kuhakikisha Benki inaendelea kuwa na maendeleo endelevu,tumeweza kuongeza mtaji wa Benki hadi Sh trilioni 1.3 na Benki iliendelea kuwa na ufanisi, na kuweka rekodi ya uwiano wa gharama za uendeshaji na mapato, kufikia asilimia 46,” amesema Zaipuna.

Afisa huyo alisema kwa mwaka 2021, Benki ilipata Tuzo saba za kimataifa, ikiwemo ya benki bora nchini kwa mwaka wa tisa mfululizo ambayo iliyotolewa na Jarida la Kimataifa la Euromoney. Kwa mujibu wa Mtendaji huyo, hadi mwishoni mwa 2021, jumla ya mikopo ya Sh trlioni 4.3 ilikuwa imetolewa kwa wakulima, wafanyabiashara wadogowadogo na wa Kati na watu binafsi.

Akizungumzia mafanikio ya benki, alisema yalitokana na uwekezaji katika mifumo ya kidijitali, huduma za wakala, ambazo ziliongezeka na kufikia mawakala 10,194 ukilinganisha na 8,410 waliokuwepo 2020.

Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya NMB, Dk. Edwin Mhede alisema ongezeko la faida kwa benki hiyo linatokana na uimara na umadhubuti wa uongozi na kwamba wanajivunia kuwa na Mtendaji Mkuu Ruth Zaipuna.

Alitaja mafanikio kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo kuwa yamekuwa yakipanda kila mwaka ambapo 2020 walitoa gawio la Sh bilioni 20.8, huku 2019 zikiwa Sh bilioni 15.6.

Dk Mhede amesema gawio kwa mwaka wa 2022 wanatarajia kuwa na gawio nono zaidi kwani kwa kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wamepata faida kubwa inayolingana na faida ya mwaka mzima katika kipindi cha miaka ya nyuma kutokana na ubunifu uliofanywa na watumishi wa benki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles