Na ASHA BANI,
BENKI ya NMB (National Microfinance Bank ) yaja kivingine kwa kuanzisha huduma ya NMB Wakala ambayo inamfuata mwananchi hadi sehemu anayoishi.
Kwa kufanya hivyo itawarahisishia wateja wake kupata huduma katika maeneo yao hasa yale ambayo kulikuwa na ugumu kufikiwa na benki hiyo.
Ubunifu kwa benki hiyo umekuwa na mwendelezo wa kuhakikisha inawasaidia wateja wake kwa kuwaondolea usumbufu wa kutoka katika maeneo ya vijijini kutafuta huduma hiyo ya kifedha.
Mkuu wa Huduma za Wakala za Dharura wa NMB, George Kivaria, anasema huduma hiyo itamsaidia mwananchi kuweza kuokoa muda na kurahisisha maisha popote alipo.
Anasema huduma hiyo inamwezesha mteja kuweka, kutoa fedha na kulipa malipo yoyote eneo lolote atakalokuwapo kwa muda huo.
Anasema ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia watu wote, wamewaandaa mawakala ili kuwafikishia wananchi huduma hiyo kwa wakati.
“Hadi sasa tuna mawakala 2200 wa kutoa huduma kwa kushirikiana na Maxcom na Selcom ambapo hadi kufikia mwisho wa mwaka huu tunatarajia kuwa na zaidi ya mawakala 3000,” anasema.
Pia anasema kuwepo na mawakala wengi kutasaidia kuongeza wigo wa ufanyaji wa biashara zao katika maeneo mbalimbali.
Aliitaja mikoa inyoongoza nchini kuwa na mawakala wengi kutokana na kujikita katika biashara, kuwa inaongozwa na Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya.
Hata hivyo, anasema benki hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kufikia matawi 189 na ATM 700 nchini.
Banki ya NMB imeingia makubaliano na Kampuni ya Maxcom kupitia mtandao wa mawakala wanaojulikana kama Max Malipo kwa ajili ya kuanza kutoa huduma za kibenki.
Kuingia kwa MaxCom kwenye Benki ya NMB kunamaanisha kuwa NMB itazidi kupanua zaidi mtandao wao kwa kuingia hadi vijijini, ikiwa ni tofauti na benki nyingine.
Kupitia mawakala wa MaxCom, wateja wa NMB wanaweza kutoa na kuweka fedha kwenye akaunti zao za NMB, kuangalia salio, kulipia huduma mbalimbali na hata kutuma fedha.
Mbali na MaxCom pia wateja wao kutoka katika maeneo mbalimbali wanatumia huduma nyingine kama Mpesa, Tigo Pesa, NMB Mobile, Pesa Fasta na nyinginezo nyingi zinazolenga kusogeza huduma karibu zaidi na wateja wao.
Benki hiyo pia ilishazindua huduma za fedha kwa kushirikiana na Kampuni ya mawasiliano ya Halotel katika ushirikiano unaoendelea kuwezesha mamilioni ya Watanzania kunufaika na huduma za kifedha nchi nzima.
Katika kufanikisha azma ya kupanua wigo wa huduma za kifedha kwa wananchi wenye vipato tofauti, Halotel na Benki ya NMB ziliingia katika ushirikiano utakaowawezesha mamilioni ya Watanzania kunufaika na huduma za kifedha nchi nzima.
Hatua hii itawawezesha Watanzania wengi zaidi kufikiwa na huduma za kifedha kwa njia ya mtandao, ikiwa ni sehemu ya kufanikisha azma ya Serikali ambayo inazitaka taasisi mbalimbali za kifedha kuwafikia wananchi na huduma zao hasa kwa maeneo ya vijijini.
Mpaka hivi sasa Halotel ina mawakala zaidi ya 30,000 walioenea nchi nzima. Hii itawawezesha wakazi wa maeneo ambayo hayakuwahi kuwa na mawasiliano kabisa au huduma za kibenki sasa kuweza kupata huduma za kifedha kupitia simu zao za mkononi.
Wafanyabiashara mbalimbali waliopo katika klabu za biashara za benki hiyo mwishoni mwa wiki waliweza kuzungumzia huduma zinazotolewa na NMB kwa kuridhika nazo, kwani zinawafikia kokote kwenye biashara zao.