29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

NMB, NHIF kuwawezesha wakulima nchini kujiunga na bima ya afya

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Benki ya NMB na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wameingia makubaliano rasmi ya kuwawezesha wakulima walioko ndani ya vyama vya ushirika nchini kunufaika na huduma za matibabu kupitia mpango wa bima ya afya kwa wakulima unaojulikana kama Ushirika Afya.

Afisa Mkuu wa Wateja binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (kushoto)  na  Mkurugenzi na Mkuu wa Mfuko wa Taifa  wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga wakipongezana baada ya kutiliana saini ya mpango wa Bima ya Afya kwa wakulima wa vyama vya Ushirika kwa uhakika wa huduma za matibaubu wakati wote na popote wakati wa hafla iliyofanyika.jijini Dar es Salaam. Katikati ni Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Udhibiti na Usimamizi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDS), Collins Nyakunga.

Katika makubaliano hayo yaliyofikiwa juzi, Benki ya NMB itamlipia Mkulima gharama za bima ya afya kwa wakati na mkulima huyu atarejesha mkopo huo bila riba wakati wa msimu wa mavuno na baada ya mauzo ya mazao husika.

Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema lengo lao ni kuwafikia wakulima zaidi 300,000 ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

Amesema wanufaika wa mpango huu watakua wateja na wasiyo wateja wa benki hiyo na mwanzoni walengwa walukima wa pamba, korosho, kahawa, katani na mahinzi walioko sehemu mbali mbali nchini.

Mponzi aliwaambia waandishi wa habari kablya ya kutiwa saini za ushirikiano huo kuwa NMB iko mstari wa mbele katika kuhudumia kundi la wakulima na kwa makubaliano hayo mkulima ataweza kujiunga na bima ya afya kwa kulipia gharama kwa mwaka kwa marejesho wakati wa msimu wa mavuno na mauzo bila riba.

“Nia yetu ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha Watanzania wengi wanakuwa na bima ya afya kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza,” alisisitiza.

Pia alisema kwa kutambua tamaduni mbalimbali za Kitanzania, malipo ya huduma hiyo yatazingatia ukubwa wa familia kama ifuatavyo:

“Mkulima mwenyewe Sh 76,800 kwa mwaka; Bima ya mtoto Sh 50,400 kwa kila mtoto kwa mwaka; Familia ya mkulima,  mwenza  wake na watoto wawili Sh 254,400 kwa mwaka na Familia ya mkulima, mwenza wake na watoto wanne Sh  355,200 kwa mwaka.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga, amesema ushirikiano huo na Benki ya NMB utawawezesha wakulima wa mazao mbalimbali nchini walio kwenye vyama vya ushirika kunufaika na huduma za matibabu kupitia bima ya afya bila kuwa na changamoto ya kifedha.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mpango wa Ushirika Afya ulianzishwa rasmi mwaka 2018 lakini ukawa unasuasua kufanikiwa jambo ambalo limepelekea kushirikiana na wadau kama Benki ya NMB ili kuweza kuwahudumia wakulima kikamilifu.

“Mfuko (NHIF) umeazimia kuwafikia Watanzania wote na huduma za bima ya afya ili waweze kupata huduma za matibabu kwa urahisi kama ilivyo azma ya Serikali yetu ya kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya. Ndio maana tumekubaliana na Benki ya NMB ambao ni wadau wakubwa wa wakulima nchini kuwawezesha wakulima kujiunga na bima ya afya bila changamoto ya kifedha,” alisema Konga.

Akizungumzia huduma, Konga amesema kuwa mkulima na familia yake atapata huduma zote za matibabu katika mtandao mpana wa vituo zaidi ya 9,000 Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hospitali ya Rufaa ya Taifa.

Ngeni rasmi katika tukio hilo, Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Udhibiti na Usimamizi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Collins Nyakunga, alipongeza jitihada zinazofanywa na Benki ya NMB na NHIF katika kuwanufaisha wakulima na huduma za bima ya afya. 

Alisema ushirikiano na vyama vya ushirika ni fursa pia kubwa ya biashara kwani mpaka sasa hivi kuna vyama 9,000 vyenye wanachama milioni sita ambapo lengo ni kuwa na idadi ya wanachama milioni 15 ifikapo mwaka 2025 ambalo litakuwa soko kubwa sana kwa taasisi hizo mbili.

“Sote ni mashahidi, ugonjwa huja bila taarifa na mara nyingi magonjwa yamewaacha wakulima kwenye changamoto kwa sababu inawabidi watumie fedha yote waliyonayo na mara nyingine kukopa ili kujitibia au kumtibia mwanafamilia.

“Kwa mpango huu unaoletwa na NHIF na Benki ya NMB, mkulima hana hofu juu ya huduma za matibabu wakati wowote yeye na familia yake,” alisema Nyakunga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles