27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

NMB kurahisisha udhibiti makusanyo ya mapato Sekta ya Utalii Zanzibar

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

BENKI ya NMB katika kuhakikisha sekta ya utalii visiwani Zanzibar inaimarika, imetimiza ahadi yake kwa kukabidhi vitendea kazi vitakavyosaidia kudhibiti ukusanyaji mapato katika sekta ya utalii.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mashine 50 za malipo, Mkuu wa Idara ya Biashara za Kadi NMB, Philbert Casmir alisema lengo ni kuimarisha na kukuza ukusanyaji wa mapato ili kuwezesha sekta hiyo muhimu visiwani humo.

“Kama mtakumbuka miezi sita iliyopita benki ya NMB pamoja na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, tulisaini makubaliano ya kuimarisha uchumi wa bluu kwa kutoa elimu na kuhamasisha watu kutembelea vivutio vya kitalii.

“Kuchangia shughuli za kitalii kwa kuwekeza kwenye mfumo wa kidijitali Zaidi utakaotumika katika makusanyo ya serikali katika vituo vyote vya utalii Zanzibar,” alisema Casmir.

Aidha, mashine hizo zilizokabidhiwa kwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Dk. Amina Ameir Issa ziliambatana na makabidhiano ya  mfumo wa kupokea malipo kwa njia ya simu, Lipa Mkononi.

“Maana yake NMB tunarahisisha mfumo wa ulipiaji huduma na bidhaa, ukiwa na simu yoyote iwe simu janja au ‘kitochi’ unafanya malipo. Huna haja ya kutembea na fedha taslimu,” alisema Casmir na kuongeza:

“NMB imekuwa ikijikita Zanzibar kwa kuwa tunatambua sekta ya utalii ni uti wa mgongo wa uchumi visiwnai hapa. Tumekuja kufanya mabadiliko kwenye upande wa makusanyo, kuanzia leo (jana) ukienda kwenye vituo vya utalii huna haja ya kubeba fedha taslimu. Uwe Mtanzania au mgeni, unalipia kwa mashine hizi kwa kutumia kadi yako ya benki, ambayo ina pokea mifgumo ya MasterCard, VISA na UnionPay,” amesema.

Alisisitiza kuwa raia wengi wa kigeni kutoka Ulaya Magharibi wanatumia mfumo wa UnionPay, mashine za NMB zinakubali mfumo huo, hivyo wageni hawatapata tabu kufanya miamala kwenye vituo vya utalii watakavyotembelea.

Katika hatua nyingine, NMB kwa kutambua raia wengi wanatumia simu za mkononi kufanya malipo mfumo wa QR Code unawasaidia wale wasio na akaunti za benki kufanya malipo, kwa wenye simu janja na wasio na simu janja, wanaweza kutumia mfumo wa Ku-scan au Lipa Namba kufanya malipo.

“Serikali inaweza kujua kiwango cha fedha kinachoingia kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi au mwaka katika sekta ya utalii,” alisema Casmir.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mali Kale, Dk. Amina Ameir Issa alisema kukabidhiwa mashine hizo na kuimarisha mfumo wa ulipaji wa malipo ni ishara kuwa benki ya NMB imedhamiria kusaidia jamii na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

“Mashine hizi zitaongeza ufanisi wa kazi na kupunguza changamoto za majukumu yetu ya kiutalii, zitaimarisha mfumo wa ukusanyaji mapato katika maeneo ya kutoa huduma za utalii, ufanisi na udhibiti mapato ya serikali,” alisema Dk. Amina na kuongeza:

“Zitaongeza imani ya wapata huduma kwa fedha zao. Tutapunguza gharama za uchapishaji risiti na zaidi ya yote mfumo unaendana na wakati na utakuza ushirikiano baina ya taasisi za serikali na binafsi,” amesema.

Aidha, alibainisha kuwa kutumia mfumo wa kidijitali wa malipo ni miongoni mwa mikakati ya wizara ambapo kwa sasa maeneo yanayotumia mfumo huo ni pamoja na Mvuleni, Kizimkazi, Mapango ya watumwa Manga Pwani, Bi Khole, Mtoni, Rasi ya Kibweni na Maruhubi.

Alifafanua kuwa, mashine hizo 50 walizopewa na benki ya NMB zitaongeza wigo wa maeneo yanayotumia mfumo wa kidijitali kwenye malipo na itasaidia kuongeza mapato ya serikali.

“Makusanyo ya mwaka uliopita wa fedha kwa wizara ya utalii yalikuwa jumla ya Shilingi Milioni 300, lakini fedha nyingi zilivuja kwa kuwa hatukuwa na mfumo mzuri wa kudhidbiti mapato.

“Mfumo huu wa kidijitali utatusaidia kufikia malengo ya mwaka huu wa fedha, ambapo tumewekewa malengo ya kukusanya Shilingi Bilioni Moja,” alisema Dk. Amina.

Kwa upande wake Meneja Mwandamizi Biashara ya Kadi kutoka NMB, David Ngusa alielezea kwa kina juu ya mfumo huo wa malipo unavyofanya kazi na kuwahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa fedha zote zitaingia kwenye mfuko wa wizara.

“Mfumo huu wa njia ya simu ama lipa mkononi, unafanya kazi na kampuni zote za simu ikiwemo Zantel ambapo kwa upande wa Zanzibar watumiaji ni wengi. Pesa inakwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya wizara, mifumo inayotumika huku (Zanzibar) unapokea huku huku kwenye wizara ya Zanzibar bila kuingiliana na Tanzania Bara,” alisema Ngusa.

Awali, Casmir alifafanua kuwa benki ya NMB imejikita katika masuala mengi sit u kwenye utalii. Ambapo hivi karibuni walizindua huduma za Go na NMB pamoja na Teleza Kidijitali pamoja na kupendezesha bustani ya Forodhani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles