29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Nkasi wapata mochwari baada ya miaka 45

Na Gurian Adolf -Nkasi

WILAYA ya Nkasi mkoani Rukwa kwa mara ya kwanza imefungua jengo maalumu la kisasa la kuhifadhia maiti lenye majokofu katika Kituo cha Afya Nkomolo tangu ilipoanzishwa miaka 45 iliyopita.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake jana, Mkuu wa Wilaya hiyo Said Mtanda, alisema tangu Serikali hii iingie madarakani, mambo mengi yamefanyika, lakini mojawapo ni kuwa na chumba maalumu cha kuhifadhia maiti kilichofunguliwa hivi karibuni.

Alisema tangu wilaya hiyo ilipoanzishwa mwaka 1974, haikuwa na chumba maalumu cha kuhifadhia maiti chenye majokofu, lakini sasa kimejengwa katika Kituo cha Afya Nkomolo na tayari kimesaidia kuhifadhi miili ya watu waliofariki wanaosubiri taratibu za maziko.

Mtanda alisema katika hospitali hiyo kimejengwa chumba chenye uwezo wa kuhifadhi miili sita kwa muda mrefu kwa kuwa kina majokofu tofauti na awali.

Alisema mafanikio mengine ni kuwa hivi sasa Serikali imeboresha upatikanaji wa dawa muhimu za binadamu kwa asilimia 90 hivyo kuwaondolea usumbufu wananchi wa kufuata matibabu katika maeneo ya mbali.

“Pia vituo vya afya vya Kirando, Wampembe na Nkomolo vinavyomilikiwa na Serikali vimeanza kutoa huduma za upasuaji na hivyo kuwaondolea usumbufu wakazi wa wilaya hiyo hususani waliopo mwambao wa ziwa Tanganyika waliokuwa wanasafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo katika Hospitali teule ya Namanyere inayomilikiwa na Kanisa Katoliki,” alisema.

Mtanda alisema Serikali inajitahidi kuboresha huduma kila kukicha ambapo hivi sasa imewapeleka madaktari sita katika Kituo cha Afya Nkomolo ambao watasaidia kuongeza idadi ya madaktari katika wilaya hiyo na huduma za matibabu zitakuwa ni za uhakika.

Alisema hayo ni mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi kifupi tangu Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani na kuwaondolea kero wananchi wanaopata huduma katika vituo hivyo.

“Wananchi wanaamua wenyewe kuchagua maeneo ya kupata huduma, ama katika hospitali za misheni au za Serikali kwa sababu Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya na kuwaondolea adha waliyokuwa wanaipata kwa muda mrefu,” alisema.

Aliwasihi watendaji wa idara ya afya wilayani humo kufanya kazi kwa uadilifu na juhudi ili wananchi wanufaike na maboresho ambayo Serikali imekuwa ikiyafanya katika hospitali zake kwa lengo la kuwasogezea huduma wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles