31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

NKAMIA APINGANA NA TANZANIA YA VIWANDA

Na MAREGESI PAUL, DODOMA

MBUNGE wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), amesema Serikali haiwezi kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kama haijajua sababu zilizoua viwanda vilivyokuwapo.

Nkamia aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akichangia taarifa ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, kuanzia Januari 2016 hadi Januari 2017.

Taarifa hiyo iliwasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Peter Kafumu.

Katika maelezo yake, Nkamia alisema badala ya Serikali kusisitiza uanzishwaji wa viwanda vipya, ingeimarisha viwanda vilivyopo  vizalishe kwa mafanikio zaidi kwa sababu baadhi havina malighafi za kutosha.

“Tulikuwa na viwanda vingi   kama Mwatex na Mutex ambavyo sasa vimekufa. Tujiulize viwanda hivyo na vingine vilikufa kwa sababu gani na tukipata majibu, tuanzishe viwanda vipya.

“Serikali inasema inataka kufufua kiwanda cha matairi wakati hatuna hata mashamba ya mpira, hivi tutakifufuaje?

“Tuna viwanda vipatavyo 30 vya pamba, lakini malighafi tuliyonayo haivitoshelezi na bado tunasisitiza kuanzisha viwanda vipya.

“Nashauri tufanye utafiti kwa nini viwanda vyetu vilikufa na tukikamilisha utafiti huo, tuimarishe tulivyonavyo.

“Nayasema haya kwa sababu siku hizi ukionana na Mwijage pale nje (Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekzaji), anakwambia ntakupa kiwanda, ukionana naye pale ‘kantini’, anakwambia nitakupa kiwanda! Hivi, hivi viwanda mtavipataje wakati hamna hata bajeti, au mnatembea navyo mifukoni?

“Lazima tuwaambie ukweli kwa sababu  tusipowaambia tutakuwa hatuitendei haki Serikali,” alisema Nkamia.

  Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM), aliilalamikia Wizara ya Nishati na Madini akisema ndiyo inayochangia viwanda vishindwe kufanya kazi.

Kwa mujibu wa Ghasia, upatikanaji wa umeme mkoani Mtwara ni hafifu na hivyo akamtaka waziri anayehusika aondoe kero hiyo   uzalishaji viwandani uweze kuongezeka.

 Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo (CCM), alisema Serikali ikiimarisha upatikanaji wa umeme Tanzania ya viwanda itafikiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles