27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

NJOO TRAVERTINE HOTEL MAGOMENI LEO TUKUMBUSHANE YA 1984

 

NA JIMMY CHIKA

YALIKUWA ni matukio makubwa ya kimuziki mwaka 1984, ukiacha kadhia mbaya kwa Watanzania ile ya kumpoteza aliyekuwa Waziri Mkuu, hayati Edward Moringe Sokoine.

Tunazidi kumuombea, apate mapumziko mema peponi, Amina. Tunairejea mada ambayo Kijaruba leo kimeikuta katikati ya akiba zake zinazoletwa kwenu kupitia ukurasa huu kila siku ya Jumamosi.

Kwa taarifa tu, ni kwamba ndani ya Kijaruba kuna hazina kubwa isiyokauka, iliyohifadhi mambo mengi yaliyokuwa yakitokea enzi hizo, ambazo pengine ni muhimu kwa wahenga kuzikumbuka na wale ambao miaka hiyo walikuwa bado hawajakanyaga ardhi hii ya Jalali, basi wapate faida ya kujua mambo hayo.

Leo tunayakumbuka matukio mawili ya kimuziki yaliyojiri mwaka 1984 na kuitikisa familia ya tasnia hiyo kiasi cha kuibakisha historia hiyo katika vichwa vya watu mbalimbali.

Kwanza ulishuhudiwa mpasuko wa bendi kubwa mbili, Mlimani Park na Vijana Jazz ambao wanamuziki wake tegemeo walichukuliwa na bendi moja ambayo kabla ya tukio hilo halikuwemo kwenye orodha ya bendi zenye tabia ya kupora wanamuziki wa bendi nyingine.

Tumeikumbuka Bima Lee ambayo kabla ya mwaka huo ilikuwa na staili za muziki wake ukiwapa nafasi kubwa waimbaji mahiri Roy Bashekanako, Jumbe Batamwanya, Belesa Kakere na Kassim Bosanga.

Walifanikiwa kuwateka mashabiki wake vilivyo hasa zile tungo za awali zilizoandaliwa muda mfupi baada ya kuanzishwa bendi hiyo mwaka 1970.

Ilikuwa kazi nzuri ya mpuliza saxafoni, Comson Mkomwa kuachia vibao kama Rafiki karibu ya nyumbani na vingine vingi ambavyo leo siyo mada yake kuvichambua sana.

Tukio kubwa ni pale ilipodhihirika kwamba wanamuziki mashuhuri Tanzania, Joseph Mulenga, Abdalah Gama na Suleyman Mwanyiro ni kweli wamekimbia katika bendi waliyoanzisha mwaka 1978 Orchestra Mlimani Park na kwenda Bima Lee.

Haikuwaingia akilini mashabiki wa muziki kwani umaarufu wa wanamuziki hao kwenda Bima ilionekana kama vile wanakwenda kushusha hadhi yao hasa ikizingatiwa enzi hizo umaarufu wao ulikuwa unamithilika na hawa vijana wanaotamba katika muziki wa kizazi kipya.

Lakini ilikuwa hivyo kwani haikuchukua muda wakali hao wa magitaa walipokea vichwa vingine vya waimbaji waliong’olewa Vijana Jazz, Othman Momba na Jerrys Nashon na kisha viongozi wa Bima wakarudia tena pale Mlimani Park na kumng’oa Shaaban Dede na kuimarisha kikosi chao.

Kwa nini matukio hayo yanafananishwa na leo?

Katika Ukumbi wa Travertine uliopo Magomeni jijini Dar es Salaam, leo kutakuwa na mpambano wa wanamuziki, ambapo bendi kongwe ya Msondo Ngoma iliyoasisiwa tangu mwaka 1964 itavaana na magwiji wa muziki wa dansi.

Kabla ya tukio hilo Watanzania walizoea kusikia bendi za Msondo na Sikinde zikiumana, lakini safari hii watayarishaji wamaunda timu ya Taifa ya Muziki wa dansi na kisha kuipambanisha na Msondo.

Kama ulitamani kuona ilivyowahi kutokea siku hizo, basi unaweza kupata nafasi hiyo adimu ambayo itaweza kukuonyesha ilivyokuwa au itakupa ufahamu wa jinsi ulivyokuwa ushindani wa muziki wa dansi.

Unadhani ni bei mbaya basi? Tsh. 10,000 inatosha au 20,000 kwa VIP. Unakosaje kwa mfano? Uje na washikaji zako.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles