30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Njia ya kutatua migogoro ya ardhi yatajwa

migogoro ya ardhiNa JANETH MUSHI, ARUSHA

KILIMO cha mashamba ya nyasi kwa ajili ya mifugo, kimetajwa kuwa ndiyo suluhisho la kumaliza migogoro inayotokea nchini kati ya wakulima na
wafugaji.

Wito huo umetolewa mjini hapa jana na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uzalishaji na Utafiti wa Mbegu ya Kibo Seed, Francis Chege, alipokuwa
akielezea umuhimu wa wakulima na wafugaji kushiriki katika Maonyesho
ya Nane Nane.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake, Chege alisema kilimo hicho
pia kinaweza kuwa ni njia nyingine inayoweza kumaliza migogoro inayojitokeza kati ya wananchi wanaoishi maeneo yaliyoko jirani na hifadhi za Taifa ambako mara nyingi wanyamapori wanaingia katika mashamba ya wananchi na kuharibu mazao.

“Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, nyasi hizo zitasaidia wafugaji
kupata malisho ya wanyama badala ya kuingiliana na wakulima na
kusababisha migogoro ya mara kwa mara.

“Katika hili, Serikali ikishirikiana na wadau wengine na kuwawezesha
wananchi kupata mbegu za nyasi na kuzisambaza, kutakuwa na suluhisho la
migogoro kwani hata Serikali ya  Kenya inasambaza mbegu za nyasi katika maeneo ya mpakani mwa hifadhi za Taifa na wananchi.

“Kwa kuwa sasa tunaingia msimu wa kiangazi, wakulima wakiotesha mbegu hizo ambazo si lazima zipandwe kwani zinaweza kumwagwa na kukua haraka, zitawasaidia kupata chakula cha uhakika cha mifugo yao kwa mwaka mzima,” alisema Chege.

Naye Ofisa Masoko wa Kampuni hiyo, Kanda ya Kaskazini, Hassan
Kimweri, alisema maonyesho ya Nane Nane yana umuhimu kwa wakulima na
wafugaji wanaokosa kanuni bora za kilimo.

Alisema kampuni yake inafanya pia utafiti na kuzalisha mbegu za mahindi, mbogamboga pamoja na nyasi za mifugo na kwamba elimu wanayotoa imesaidia uwepo wa mwamko kwa wafugaji kwa kuwa sasa wanatenga maeneo na kupanda nyasi hizo.

“Tunatoa mafunzo kupitia mashamba darasa kwa wakulima na wafugaji kupitia maonyesho hayo pamoja na Kanda nyingine za Mbeya, Morogoro, Mwanza na Makambako.

“Kutokana na elimu tunayotoa, wafugaji wakubwa wameanza kuwa na mwamko na sasa tunahamasisha wafugaji wadogo wabadilike na kuachana na ufugaji wa mazoea,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles