33.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Njia tano za kujihami na wizi wa benki

Pg jpgNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KUTOKANA na kushamiri kwa matukio ya wizi yanayoelezwa kutokana na mtandao wa majambazi kushirikiana na watumishi wa mabenki nchini, Jeshi la Polisi limelazimika kutaja mbinu za kujihami.

Hatua hiyo inatokana na kuwapo kwa baadhi ya wafanyakazi wa benki, ambao kwa namna moja au nyingine wanashirikiana na majambazi kufanya uhalifu.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Simon Sirro, alisema kutokana na hali hiyo, hivi sasa wanawasiliana na wamiliki wa taasisi za kifedha kujiridhisha uhusika wao na uhalifu wa kutumia silaha.

 

MBINU ZA KUJIHAMI

Kamanda Sirro alisema iwapo kuna mtu yeyote anataka kubeba kiasi kikubwa cha fedha, ni vema akatoa taarifa kwa jeshi hilo kwa kufuata hatua zifuatazo:

  1. Mtu yeyote anayetaka kwenda kuchukua fedha nyingi benki atoe taarifa kwa Jeshi la Polisi ili apate ulinzi.
  2. Unaruhusiwa kulipia Sh 10,000 au Sh 20,000 ambapo utapewa askari mwenye silaha ili akulinde.
  3. Toa taarifa kwa Jeshi la Polisi pindi unapohisi kuna dalili ya tukio la kuvamiwa.
  4. Epuka kupanda bodaboda pindi unapokuwa na kiasi kikubwa cha fedha.
  5. Kutumia njia mbadala ya kuchukua fedha benki ili kuepuka uhalifu huo.

 

MATUKIO YA UJAMBAZI

Uamuzi huo wa Jeshi la Polisi umekuja baada ya hali ya Jiji la Dar es Salaam kuwa ya hatari na kuwafanya wakazi wake kuishi roho mkononi.

Matukio ya ujambazi wa kutumia silaha yamekuwa sugu na kusababisha wananchi wanaopeleka au kutoa fedha benki kuvamiwa, kujeruhiwa au kuuawa mchana kweupe na majambazi wanaotumia pikipiki aina ya Boxer.

Hali hiyo inawafanya watumiaji wa huduma za benki zilizo ndani ya jengo la Mlimani City maisha yao kuwa hatarini, hasa wale wateja wanaotoa fedha nyingi kutokana na kukumbwa na matukio ya kuuawa na kuporwa fedha zote na majambazi wanaotumia pikipiki hizo.

Matukio mengi ambayo yamekuwa yakitokea kwa wateja hao, majambazi wamekuwa wakitumia pikipiki aina ya Boxer ambayo ina uwezo mkubwa wa kukimbia.

Miongoni mwa matukio ya kusikitisha yakihusisha moja ya benki zilizopo katika jengo la Mlimani City, ni lile lililotokea wiki hii ambapo taarifa zake zilizagaa kwenye mitandao ya jamii kwa mtu mmoja kuuawa.

Inaelezwa kuwa mtu huyo aliuawa na majambazi wakati akitoka kwenye moja ya benki zilizoko Mlimani City kuchukua kiasi cha Sh milioni 10 na kuanza safari ya kuelekea eneo la Tegeta Salasala ambako alikuwa akifanya shughuli zake za ujenzi wa nyumba yake.

Taarifa ya gazeti hili iliyotolewa juzi ilimfanya Kamanda Sirro kusema kuwa wameanza kuweka ulinzi mkali katika benki mbalimbali, zikiwamo zilizopo eneo la Mlimani City na kwamba wanakagua pikipiki na watu wanaowatilia shaka.

Alikiri na kusema kwamba wapo baadhi ya wafanyakazi wa benki ambao kwa namna moja ama nyingine wanashirikiana na majambazi kufanya uhalifu, na kutokana na hilo, watawahoji wafanyakazi wa taasisi hizo za fedha ili kubaini ni nani wanaohusika katika njama hizo.

Alisema hiyo ni operesheni maalumu iliyoanza rasmi na kwamba uhalifu wa kutumia silaha unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya jiji unahatarisha maisha ya wakazi wake na unapaswa kudhibitiwa haraka.

Kamanda Sirro alisema wananchi wanapaswa kutumia njia mbadala ya kuchukua fedha benki ili kuepuka uhalifu huo.

Alisisitiza kuwa unyang’anyi huo hufanyika kwa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda na kwamba wameanza operesheni ya kuwakamata wenye bodaboda hizo na kuwahoji.

“Tumeanzisha oparesheni maalumu dhidi ya waendesha pikipiki ambao wanavunja sheria barabarani na wanaojihusisha na masuala ya uhalifu jijini,’’ alisema Kamanda Sirro ambaye ameshika wadhifa huo kuanzia Januari mosi mwaka huu.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuripotiwa kutokea kwa matukio kadhaa ya uhalifu, ambapo baadhi ya wananchi wameporwa fedha zao mara tu baada ya kutoka kuchukua katika benki. Baadhi ya benki zinazohusishwa na zile zilizopo katika eneo la Mlimani City katika Manispaa ya Kinondoni.

MTANZANIA ilipomtafuta Meneja Usimamizi wa Mabenki wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kennedy Nyoni ili kuweza kujua mikakati iliyowekwa na chombo hicho ambacho ndicho kinasimamia mabenki nchini, aliomba atumiwe maswali kwa kuwa yupo kikaoni na juhudi za gazeti hili kuweza kumpata zinaendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles