26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NJIA MUHIMU ZA KUFANYA MAZOEZI, KUWA MKAKAMAVU

Dk. Fredirick. L. Mashili, MD,PhD.

UKAKAMAVU au ‘fitness’ si matokeo, bali ni mtindo wa maisha. Hii inamaana kwamba kudumisha ukakamavu mtu anatakiwa kushughulika kila siku kwa kufanya mazoezi. Haitatokea hata siku moja mtu akafikia mwisho na kusema ‘sasa mazoezi basi, nimekwisha kuwa mkakamavu au fit kiasi cha kutosha’ la hasha. Kuwa mkakamavu ni safari inayoendelea kila siku na wala si mahali ambapo ukishafika inakuwa imetosha.

Ziko sababu nyingi za kuwa mkakamavu kwa kufanya mazoezi mara kwa mara–sababu kubwa ikiwa ni ukweli kwamba ukakamavu unahusishwa kwa karibu sana na afya bora. Kutokana na matokeo ya tafiti mbalimbali duniani, ukakamavu (fitness) hukupa kinga ya magonjwa ya moyo, kisukari na hata saratani. Watu wakakamavu huishi maisha marefu zaidi kuliko wale wasio wakakamavu. Wakakamavu pia wanao uwezo mkubwa zaidi wa kufanya kazi yoyote ile ukilinganisha na wale wasio wakakamavu.

Hii ndiyo sababu tunakuletea dondoo hizi ili kukupa ufahamu na ujuzi kuhusu nini cha kufanya ili uwe mkakamavu na mwenye afya njema.

  1. TENGA MUDA MAALUMU KWA AJILI YA KUFANYA MAZOEZI

Kama una muda wa kutosha, tenga muda maalumu kwa ajili ya kufanya mazoezi. Anza kuamini kwamba muda huu hauupotezi, bali unajiongezea siku za kuishi, nguvu ya kufanya kazi na afya bora. Kutokana na shirika la afya duniani (WHO) ni muhimu kujiwekea angalau nusu saa moja kwa ajili ya kufanya mazoezi kila siku. 

  1. TUMIA KILA FURSA INAYOJITOKEZA KUFANYA MAZOEZI

Tunaelewa kwamba si kila mtu anao muda wa kutosha kufanya mazoezi. Kama wewe ni mmojawapo, usiogope, hakuna kilichoharibika. Tumia ngazi kwenda ofisini, tembea pale inapowezekana, paki gari mbali kidogo na ofisi, simama kutafuta na kuchukua mafaili ofisini, tembea kwenda kupata chakula cha mchana na wala usitumie simu kumtafuta mfanyakazi mwenzako, baadala yake mfuate ofisini kwake.

  1. JIUNGE NA KLABU YA MCHAKAMCHAKA ‘JOGGING CLUBS’

Tafiti zinaonyesha kwamba kujumuika kunatoa motisha wa kufanya mazoezi na kutimiza malengo. Hongera kwa Watanzania, kwa kuanzisha na kujumuika katika ‘jogging clubs’ mbalimbali. Unangoja nini–jiunge na mojawapo ya club hizi sasa.

  1. PIMA UKAKAMAVU AU ‘FITNESS LEVEL’ YAKO ANGALAU MARA MOJA KWA MWAKA 

Ndiyo, inawezekana kabisa. Ziko njia rahisi kabisa za kuweza kufahamu kiwango cha ukakamavu au ‘fitness level’ yako. Kama unavyofahamu ukakamavu unaweza kukuambia mengi kuhusu afya yako ya baadaye. Unapopata ufahamu kuhusu ukakamavu unakuwa unafahamu ni kipi cha kufanya kwa wakati gani. Ukipata wasaa, hakikisha unaonana na daktari wa mazoezi ili akupime kiwango cha ukakamavu wako na kukupa ushauri wa jinsi ya kudumisha afya yako.

  1. TEMBEA KWA MIGUU AU TUMIA BAISKELI KWENDA KAZINI AU SEHEMU NYINGINE YOYOTE

Tafiti zinaonyesha kwamba watu wanaotembea kwa miguu au kutumia baiskeli huwa na afya bora kuliko wale wanaotumia vyombo vya moto (magari na pikipiki). Shirika la Afya Duniani (WHO) limeidhinisha kutembea na kuendesha baiskeli kama njia muhimu zinazotoa fursa ya kufanya mazoezi na kudumisha afya.

Kama wewe ni mmoja kati ya watu wenye bahati ya kuwa na mazingira yanayowawezesha kufanya hivi, usiache kuitumia fursa hii. Kuishi karibu na sehemu unayofanyia kazi, kuwa na barabara maalumu kwa waendesha baiskeli ni mojawapo ya vitu vinavyokupa fursa ya kutembea au kuendesha baiskeli.

Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fiziolojia ya Mazoezi na Homoni katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa mawasiliano, www.jamiihealthtz.com au www.jamiiactive.org. Au 0752 25 59 49.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles