33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NJIA 10 ZA KUONGEZA UWEZO WA KUZAA, KUZALISHA

Na JOACHIM MABULA,

KUPATA mtoto ni kitu kinachofurahisha kwa wenzi hasa waliofunga ndoa. Ambao hawakubahatika kupata mtoto wanakabili wakati mgumu mno. Baadhi ya wanawake hushika ujauzito mapema tu baada ya kujamiiana na kwa wengine huchukua muda mrefu hadi kusababisha kukata tamaa kwa wenzi hao.

Iwe unajaribu kupata mtoto wako wa kwanza au wa sita, kuna njia nyepesi unazoweza kuzifuata ili kuongeza uwezo wa kuzaa/kuzalisha. Njia 10 bora za kuongeza uwezo wako wa kuzaa/kuzalisha ni kama ifuatavyo:-

Dumisha uzito unaofaa kiafya

Wanawake wengi wanapenda kuwa na uzito wanaoupenda wao, ingawa si kila uzito unafaa kwa kuwa na hali nzuri ya uzazi. Kuwa na uzito kupita kiasi au kuwa na uzito mdogo kupita kiasi kunaweza kusababisha ugumu katika kushika ujauzito. Uzito unaweza kuathiri udhibiti wa homoni na hivyo kuathiri ovulesheni (yai kutolewa). Kudumisha uzito unaofaa kiafya kunasaidia kudhibiti ovulesheni ya kawaida na kuongeza uwezekano wa kushika mimba.

Weka mbegu za kiume katika afya bora

Nini huanza kwanza, mbegu za kiume au za kike? Wanawake wengi hutilia mkazo afya ya mayai, tarehe za ovulesheni na idadi ya mayai, hata hivyo hupaswi kusahau umuhimu wa mbegu za kiume. Idadi, harakati na umbo la mbegu za kiume ni sehemu muhimu ya afya ya mbegu za kiume, lakini pia kuna vitu vinavyopaswa kufanywa au kutofanywa ili kudhibiti afya bora ya mbegu za kiume. Ili kuwa na mbegu zenye afya, wanaume wanahamasishwa kudumisha uzito unaofaa kiafya, kula mlo bora/kamili, kuzuia magonjwa ya ngono, kudhibiti mkazo (stress) na kufanya mazoezi.

Kuepuka uvutaji wa tumbaku, kudhibiti matumizi ya pombe, kuepuka sumu mbalimbali mfano sumu za kuulia wadudu kwenye mbogamboga, hizi ni kati ya hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kukuza afya ya mbegu za kiume. Ni vyema kuvaa nguo za ndani zisizobana, tumia muda kidogo kukaa, kuepuka joto sehemu za siri mfano kukaa kwenye jakuzi la maji moto, kuweka simu au kompyuta za kupakata (laptops) karibu na makorodani.

Jikinge na magonjwa yanayoambukizwa kwa kujamiana

Kujikinga na magonjwa ya ngono hakutakulinda tu afya yako bali pia uzazi wako. Kisonono na Klamidia (Chlamydia) ni kati ya magonjwa yanayoharibu uzazi kwa wanaume na wanawake. Kuna njia zinazoweza kutumika kupunguza hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa mfano matumizi sahihi ya kondomu na kuwa mwaminifu kwa mpenzi wako.

Fanya tendo la ndoa

Ikiwa mko katika uhusiano wa kike na kiume na mnahitaji kupata mimba, fanyeni tendo la ndoa mara nyingi iwezekanavyo hasa wakati wa siku nzuri kwa mwanamke kushika ujauzito. Kwa wastani, siku nzuri za mwanamke kupata mimba kwenye mzunguko wa hedhi huhusisha siku tano kabla ya ovulesheni (yai kutolewa), siku ya ovulesheni na siku 2-3 kufuatia ovulesheni. Kufanya ngono kila siku au kila baada ya siku mbili kutaongeza uwezekano wa kupata siku nzuri ya kupata mimba tofauti na kufanya ngono mara chache.

Zingatia ni mafuta gani ya kulainisha utatumia

Baadhi ya wenzi hutumia/huhitaji mafuta ya kulainisha wakati wa tendo la ndoa, lakini si kila mafuta yamefanyizwa kwa jinsi ile ile. Ikiwa utanunua mafuta hayo,  fikiria Pre-Seed, mafuta yaliyotengenezwa kulingana na ute wa seviksi (mfuko wa uzazi). Pre-Seed haina Glycerin hivyo huruhusu mbegu kuogelea kwa uhuru kuelekea kwenye yai kwa ajili ya urutubishwaji. Mafuta mengine kama Astroglide, KY Jelly na Touch huzuia mbegu kusafiri vizuri.

Kunywa pombe kistarabu

Wanaume kwa wanawake wanahitaji kuchukua tahadhari pindi wanapochagua vinywaji ili kuongeza uwezekano wa kuzaa/kuzalisha. Kwa wanaume, matumizi ya pombe kupita kiasi hupunguza uzalishaji wa homoni ya testosteroni na kusababisha uume kutosimama sawasawa na kuchangia kupungua kwa mbegu za kiume zinazotengenezwa. Kwa wanawake, matumizi ya pombe kupita kiasi huweza kusababisha matatizo ya ovulesheni na hivyo kuathiri uwezo wa kushika mimba.

Punguza matumizi ya kahawa

Kafeini inayopatikana kwenye kahawa inaweza kuchangia kusababisha utasa ikiwa miligramu 500 au zaidi hutumiwa na mtu, hii ni sawa na vikombe vitano vya kahawa kwa siku. Matatizo ya kafeini yanayopendekezwa kwa siku ni miligramu 200-250.

Usivute tumbaku

Sote tunatambua kuwa uvutaji wa sigara ni mbaya kwa afya zetu kiujumla, lakini unafahamu uvutaji wa sigara unaweza kuathiri uwezo wako wa kupata mimba? Uvutaji wa sigara kwa wanaume unaweza kusababisha uzalishaji mdogo na kasi ndogo ya mbegu za kiume na uharibifu wa DNA wakati kwa wanawake husababisha kutokukomaa kwa ovari.

Acha mazoezi magumu na kwa muda mrefu

Kufanya mazoezi ni vizuri kwa afya yako kiujumla, ukiwa unajaribu kupata mimba mazoezi mazito yanaweza kuwa hatari kwa hali yako ya uzazi. Mazoezi zaidi ya saa tano kwa wiki, mazoezi magumu yanaweza kusababisha matatizo ya uzazi kwa sababu ya kukandamiza ovulesheni na homoni ya projesteroni(homoni inayohusika na mzunguko wa hedhi na utungwaji wa mimba. Ni vizuri kuzungumza au kumwona mtaalamu wa mazoezi ili kuweza kukupangia aina na muda wa mazoezi utakao kufaa kulingana na shughuli zako.

Jihadhari na sumu

Kila mahali, kuna aina fulani ya kemikali unazopaswa kujihadhari nazo kwa kuwa kemikali zingine huchangia utasa kwa wanaume na wanawake. Wanaume na wanawake waliopatwa na sumu za kuulia wadudu mfano kwenye bustani za mbogamboga, mbolea zenye sumu wanaweza kupata matatizo ya uzazi. Baadhi ya kazi kama kazi za viwandani, kilimo, saluni na daktari meno wako katika hatari ya kupatwa na kemikali hatari kwa afya ya uzazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles