Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Timu ya soka ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje Sports Football) imeendeleza ubabe katika bonanza la michezo kwa kuifunga timu ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi mabao 3 – 0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Mao Zedong’s, Zanzibar.
Magoli ya Nje Sports yalifungwa na mshambuliaji Fabian David katika dakika ya 35 na Yacoub Kibiga aliyefunga mabao mawili dakika ya 79 na 86.
Ushindi huo unaifanya timu hiyo kufikisha michezo mitatu bila kufungwa ambapo mchezo kwanza Januari 9, 2024 iliifunga Baraza la Wawakilishi mabao 3-1, mechi ya pili iliichapa timu ya Ofisi ya Rais Ikulu – Zanzibar mabao 8-3 Januari 10,2024.
Akizungumza baada ya mchezo wa jana kumalizika, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ameipongeza Nje Sports kwa ushindi mnono na kuzitaka timu zote mbili kuendeleza michezo kwa kuwa ni afya na inaimarisha ushirikiano baina ya wachezaji na jamii.
Naye Kocha wa Nje Sports, Shaban Maganga amesema pamoja na ushindi walioupata wataendelea kujifua zaidi na kuhakikisha kuwa kikosi chake kinakuwa imara wakati wote.