NAIROBI, KENYA
NJAA na gharama za juu za maisha zimefanya wananchi kusahau janga la ufisadi linalolikumba taifa.
Matokeo ya utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Utafiti la Ipsos, yamebainisha idadi kubwa ya Wakenya wanaamini njaa na bei kubwa ya bidhaa muhimu ndiyo matatizo makuu zaidi yanayoikumba nchi, ikilinganishwa na ufisadi.
Utafiti huo uliofanywa kati ya Mei 11 na 23, mwaka huu, unaonyesha asilimia 36 ya Wakenya walitaja gharama kubwa ya maisha kuwa tatizo linaloikumba nchi, huku asilimia 21 wakiamini njaa ndiyo tatizo kuu.
Kwa upande mwingine, ufisadi ulitajwa na asilimia 15 pekee ya Wakenya, wakifuatiwa na asilimia 13 waliosema tatizo kuu ni ukosefu wa ajira.
Hali hiyo ni tofauti na ilivyokuwa Januari, kwamba asilimia 21 walikuwa wanaamini ufisadi ndio tatizo kuu, na asilimia 14 pekee wakati huo walisema njaa inatatiza zaidi.
Hata hivyo, mchambuzi wa utafiti huo, Dk. Tom Wolf, alisema matokeo hayo hayamaanishi Wakenya wamesahau changamoto ya ufisadi unaoikumba nchi.
“Ni kwa vile tu suala hilo halijapewa uzito ikilinganishwa na masuala mengine kama vile ukame na ukosefu wa chakula cha kutosha. Sababu ya hali hiyo huenda ni kutokana na vyombo vya habari kutoangazia zaidi ufisadi wakati huu,” alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Utafiti pia ulionyesha Nairobi inaongoza kwa idadi ya wanaokabiliwa na umasikini (asilimia 52), ikifuatwa na Pwani, Nyanza na Rift Valley kwa asilimia 46 kila eneo.
Asilimia 45 ya waliohojiwa walisema hali hii inaweza kutatuliwa kwa kuongeza nafasi za ajira.