30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Niyonzima na sababu tano za kurudi Yanga

NA ZAINAB IDDY

HATIMAYE kiungo wa zamani wa Yanga na Simba, Haruna Niyonzima anatarajiwa kuvaa kwa mara nyingine jezi ya Yanga, baada ya klabu hiyo kumsajili wakati huu wa dirisha dogo la usajili.

Niyonzima amejiunga Yanga kwa mara nyingine akitokea As Kigali ya nchini kwao Rwanda, akiwa na kumbukumbu ya kukipiga kwa Wanajangwani kwa mafanikio kwa miaka sita mfululizo.

Kiungo huyo fundi alianza kusakata Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kusajiliwa na Yanga mwaka 2012.

Akiwa bado kijana mdogo, ndani ya muda mfupi, alifanikiwa kuwa staa kuwa mchezaji tegemeo wa kikosi cha Yanga.

Ustaa wake ulikuja baada ya kufanya kazi yake vilivyo ndani ya uwanja. Kwa wakati mmoja  aliweza kufunga, kuwa mpiga faulo mzuri, kutengeneza nafasi za kufunga kwa wachezaji wengine  na kuwa mburudishaji kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuchezea mpira.

Baada ya miaka sita kuvaa uzi wa kijani na njano, Niyonzima aliamua kubadili upepo na kujiunga na Simba iliyompa donge nono linalodaiwa kuwa ni Sh milioni 90 za  Kitanzania na mkataba wa miaka miwili.

Kama ilivyowahi kutokea kwa Emmanuel Okwi  na Ibrahim Ajib walioondoka Simba kabla ya kurejea tena, Niyonzima anaungana tena na familia yake ya zamani Jangwani wakati huu wa dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufungwa Januari 15 mwakani.

Tayari uongozi wa Yanga, umetambulisha nyota huyo kuwa mmoja wa wachezaji iliowasajili wakati huu wa dirisha dogo.

Usajili huo hata hivyo umezua maswali mengi miongoni mwa wadau wa michezo, wapo wanaohoji kipi kinachomrejesha kwa mabosi wake hao wa zamani ambao wakati anaondoka kwenda Simba, wapo waliomdhihaki na kumtusi na wengine wakichukua uamuzi wa kuchoma jezi yenye namba aliyokuwa anaitumia.

Lakini MTANZANIA linakupa sababu tano za nguvu zinazompa uhalali Niyonzima kurejea Yanga kwa mara nyingine .

Rekodi ya kushinda mataji
Ukiangalia kikosi cha Yanga cha sasa, asilimia 80 ya wachezaji wake  hawajashinda mataji na klabu hiyo.

Mwangalie Farouk Shikalo, Metacha Mnacha, Ally Mtoni ‘Sonso’,  Feisal Salum Abdallah,  ‘FeiToto’, Mohamed Issa ‘Mo Banka’, Ally Ally na wengine wengi waliojiunga na Yanga.

Ni wachezaji muhimu  katika kikosi hicho  wakati huu, lakini  hawajahi kushinda mataji ya ligi wala mashindano yoyote ambayo timu yao hiyom imeshiriki.

Lakini hata wakongwe hawa, Deusi Kaseke, Mrisho Ngassa, Rafael Daud, Juma Abdul na Kelvin Yondan ambao wamewahi kushinda mataji na klabu hiyo kwa sasa wameshindwa kufanya kile ambacho mashabiki wengi wa Yanga wanakihitaji ambacho ni ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara walioukosa kwa misimu miwili.

Katika kipindi hicho cha misimu miwili, ubingwa wa ligi hiyo umekuwa ukienda kwa Simba, ambayo ni mshindani mkuu wa Yanga.

Lakini kurejeshwa kwa Niyonzima kunaweza kuchochea vita ya kusaka taji hilo kwani katika kipindi cha miaka sita alichovaa uzi wa kijani na njano, timu hiyo iliweza kuchukua mataji mengi kuanzia ya Ligi Kuu, Kombe la Azam , Ngao ya Jamii, Kombe la Kagame na Kombe la Mapinduzi.

Kiongozi ndani ya uwanja.

Ni ukweli usio na kificho hivi sasa Yanga inakosa mchezaji kiongozi dimbani, kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kinapoteza morali ya wachezaji.

Yondani, Ngassa na Juma Abdul ni wachezaji wakongwe Yanga, lakini hawana kipaji cha uongozi.

Lakini pia kati yao mwenye uhakika wa kuanza kikosi cha wachezaji 11 wa kwanza ni Yondani, Ngassa na Abdul mara nyingi wamekuwa wakianzia benchi.

Sibomana, Mapinduzi Balama, Makame, Sonso na wengine waliosajiliwa msimu huu wanahitaji kufanya kazi na mtu wa aina ya Niyonzima ili waweze kujituma zaidi na kuipa timu yao mafanikio.

Kuibua hofu kwa wapinzani
Baada ya miaka mingi, Yanga ilikubali kupoteza mchezo  Uwanja wa Taifa na timu ndogo ya Ruvu Shooting.

Hii inaonyesha jinsi gani wapinzani wa Yanga hawana hofu tena wanapokutana nayo.

Lakini uwepo wa Niyonzima utasababisha wapinzani wa Yanga kupata hofu ambayo kwa Wanajangwani hao ni faida kubwa kwani wanaweza kuitumia kupata matokeo ya ushindi.

Pia timu nyingi zitapanga mikakati ya kumzuia Niyonzima na kuwasagau wachezaji wengine ambao wanaweza kutumia mwanya huo kuwaletea madhara.

Thamani ya jezi yake

Niyonzima ni mchezaji mkubwa si Tanzania tu bali Afrika Mashariki, hiyo  ni kutokana na rekodi yake katika klabu kadhaa alizozichezea kuanzia APR ya kwao Rwanda.

Kurejea kwake Yanga kunaweza kuwarudisha viwanjani mashabiki wake ambao pengine waliacha kuhudhuria michezo  ya timu hiyo, baada ya kukerwa na hatua yake ya kuhamia Simba.

Hata katika soko la jezi, Yanga inaweza kufanya biashara kwa kutumia ukubwa wa jina lake.

Kurudisha heshima yake

Mnyarwanda huyo anarejea Yanga akiwa na deni kwa Wanajangwani, baada ya kuchuakua uamuzi ya kutimkia Simba kipindi ambacho bado walikuwa wanahitaji huduma yake.

Lakini pia licha ya kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu akiwa na Simba, jina lake limeonekana kushuka umaarufu kwa kiasi fulani.

 Hiyo ilitokana na huko Simba kukutana na majina mengine makubwa zaidi yake akiwemo Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na Clatous Chama. 

Pia inafahamika wazi kuwa Simba ilimtema kutokana na kile ilichodai hakuwa tena na ubora unaoendana na matarajio ya Wekundu hao wa Msimbazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles