30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Nitapambana miradi yote ikamilike haraka – Bonnah

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli amesema atahakikisha miradi yote ya maendeleo iliyopangwa katika jimbo hilo inatekelezwa kwa wakati na kuwapunguzia kero wananchi.

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Kifuru Kata ya Kinyerezi alipokuwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo.

Ameyasema hayo baada ya kufanya ziara katika Kata za Kinyerezi, Buguruni na Tabata kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Mwaka mpya wa Serikali umeshaanza na tuna miradi ya DMDP awamu ya tatu ikiwemo ujenzi wa kingo za Mto Msimbazi. Niwaombe madiwani na wenyeviti tushirikiane tuhakikishe wakandarasi wanaanzia sehemu zenye madhara kwa sababu mto unapita sehemu nyingi na zingine nyumba zimeathiriwa,” amesema Bonnah.

Aidha amemuomba mkandarasi anayejenga mfereji katika Mtaa wa Msimbazi Magharibi amalizie kipande cha mita 100 kilichobaki pamoja na kuweka mifuniko imara ili wananchi wa maeneo hayo waweze kukaa katika mazingira mazuri.

Diwani wa Kata ya Buguruni, Busoro Pazi, akimuonyesha mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli (katikati) maendele ya ujenzi wa mfereji.

Katika ujenzi wa stendi Kinyerezi Msimamizi wa mradi huo kutoka Kampuni ya UWP Consulting, Injinia Mahobe Abdul, amemuhakikishia mbunge huyo kuwa utakamilika Agosti 30,2021.

Mradi wa ujenzi wa stendi hiyo sambamba na barabara ya Gongolamboto hadi Kinyerezi na Daraja la Ulongoni B inagharimu Sh bilioni 17.6.

Katika ziara hiyo Bonnah pia amepata nafasi ya kuzungumza na wananchi mbalimbali ambapo katika Mtaa wa Kifuru Kata ya Kinyerezi wameomba ujenzi wa barabara ya NST Bangulo uharakishwe kwani wamekuwa wakipata adha kubwa hasa wakati wa mvua.

Injinia Mahobe Abdul akimweleza mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, maendeleo ya ujenzi wa stendi hiyo.

Naye Diwani wa Kata ya Kinyerezi, Leah Ng’itu, ameomba wasaidiwe barabara za ndani kwa kuweka vifusi pamoja na kukarabati maeneo korofi kwenye barabara za lami.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Buguruni, Busoro Pazi, amesema ujenzi wa mfereji katika Mtaa wa Mvinjeni utakuwa ni suluhisho la kero ya mafuriko katika eneo hilo.

“Tunamshukuru mbunge wetu kwa juhudi kubwa alizozifanya kuhakikisha katika Mtaa wa Mivinjeni mfereji huu unajengwa, changamoto ya maji kutoka katika Mto Msimbazi kwenda kwenye makazi ya wananchi ilikuwa ni kubwa sana lakini kupitia ujenzi wa mfereji kero hii itaisha kabisa,” amesema Pazi.

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa mfereji katika Mtaa wa Mvinjeni.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mvinjeni, Fadiga Legele, amesema kabla ya ujenzi wa mfereji huo walikuwa wakipata adha kubwa ya mafuriko ambayo yalisababisha wakati mwingine wananchi kuhamishwa kwa ajili ya kuwapatia hifadhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles