23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

NINI KINAWAANGUSHA AZAM, BAHATI AU MIPANGO?

NA MARTIN MAZUGWA


BINADAMU wote ni sawa, ukiiangalia  Azam FC ndipo utaweza kugundua hiki ninachokisema na utabaini ni kwanini nimeamua kuanza na msemo huo.

Licha ya kuwa na miundombinu bora kuliko timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini wakali hawa wameshindwa kufurukuta kabisa katika mashindano ya kimataifa hasa Kombe la Shirikisho.

Jambo linaloibua maswali lukuki katika vichwa vya wapenda kandanda si kwamba Azam hawana timu nzuri la hasha, wakali hawa wana kikosi imara na chenye ushindani mkubwa.

Unapata wapi ujasiri wa kusema timu hii mbovu, ambapo inakumbukwa ilifanya usajili wa nguvu kwa kusajili  nyota kutoka Afrika Magharibi, sehemu yenye wachezaji wenye viwango vya juu.

Wana wakali kama vile Yahya Mohamed, Enoch Atta Agyei, Yakub Mohamed moja kati ya nyota wenye uwezo mkubwa kutoka nchini Ghana.

Uwanjani Lambalamba wamekamilika kila idara, lakini licha ya kukamilika huko vijana hawa wanakosa kitu kimoja nacho ni bahati  ya kuwatoa hapo walipo na kuwavusha hatua inayofuata ili kuweka rekodi hapa nchini na nje ya nchi.

Azam FC ambayo ilianzishwa mwaka 2008, tangu kuanzishwa kwake  haijawahi kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho zaidi ya kuishia raundi ya pili.

Zaidi ya makocha watano wamepita katika timu hiyo, lakini wote wameshindwa kutembelewa na malaika wa bahati ambaye ataisaidia timu kuvuka bonde hilo la kifo ambalo linahitaji kocha jasiri mwenye moyo wa simba kufanikisha hilo.

Makocha waliopita katika klabu hii ni pamoja na Neider dos Santos, Itamar Amorin, Stewart Hall, Boris Bunjack, Joseph Omog pamoja na Zeben Hernandez, ambao wote kwa nyakati tofauti walipokuwa wakufunzi wa kikosi hiki, lakini walishindwa kuutafuna mfupa huu.

Sasa ni zamu ya Mromania, Aristica Cioaba, ambaye tayari msimu wake wa kwanza tu amechemsha kuwavusha matajiri hawa hadi hatua ya pili, baada ya kuondolewa na Mbabane Swallows ya Swaziland na kuendelea kufuata mkondo wa watangulizi wake waliopita ndani ya timu hiyo.

Miaka mitatu mfululizo, wakali hawa wa Chamazi wanashindwa kupenyeza hatua ya makundi ya michuano hiyo ya kimataifa, licha ya kuwa na timu iliyojitosheleza kwa kila kitu ndani na nje ya uwanja, huku ikiwa na watendaji wasomi tofauti na klabu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu.

Tatizo linalowatesa Azam linafanana na lile la Atletico Madrid, ambao wanalia kila kukicha kwa kushindwa kubeba taji la UEFA, licha ya kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya mara mbili.

Katika fainali hizo zote mbili wanapoteza mbele ya mahasimu wao wa jiji moja, huku wao mara zote wakianza kuongoza, lakini mwisho wa siku vijana hao wa Diego Simeone, wamekuwa wakiishia kulia na kuwaacha matajiri wa jiji la Madrid wakichekelea na kuwabeza.

Bado naendelea kutafakari kinachowatesa Azam ni mipango yao waliyojiwekea au wanamkosa malaika wa bahati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles