31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Nini kinasababisha msongo wa mawazo?

CHRISTIAN BWAYA

HIVI karibuni nilishuhudia watu wawili wakirushiana maneno makali kwenye foleni ya mashine ya kutolea fedha (ATM).

Tukiwa tumesimama kusubiri zamu yetu ya kupata huduma, dada mmoja aliyeonekana kuwa na haraka ya kupata huduma mapema kuliko sisi, alivuruga utaratibu wa kusimama kutaka kuwawahi waliokuwa mbele yake.

Labda kwa kukerwa na jitihada hizo za kuvuruga utaratibu, mama mmoja aliyekuwa amesimama nyuma alikosa uvumilivu. “Hivi watu wengine mkoje? Unatuonaje sisi tuliosimama huku nyuma? Unafikiri hatuna haraka kama wewe? Acha dharau” alifoka mama huyo huku akitamka maneno makali yanayoweza kutafsiriwa kama matusi.

Pamoja na kosa la ukosefu wa ustaarabu lililokuwa limefanyika, watu wengi waliokuwa wamesimama kwenye foleni hiyo walifikiri mama yule alizidisha hasira. Kuona watu wanamgeuzia kibao mama alianza kumtukana kila mtu hali iliyokuza mzozo ule usio rasmi.

“Hebu muwe mnatafuta mahali sahihi pa kutolea hiyo misongo ya mawazo mliyonayo,” alipendekeza mzee mmoja kwa kejeli na kusababisha watu kuangua kicheko.

Matukio ya watu kutukanana na kurushiana maneno bila sababu ya msingi, yamekuwa mengi. Unapofuatilia soga kwenye mitandao ya kijamii, vijiweni, katika usafiri wa umma na hata kupitia mazungumzo yanayofanyika kwenye vyombo vya habari, unaona na mna watu wanavyojibizana pasipo kuwa staha.

Aidha, kuna tabia ya ukosoaji mkubwa unaoendelea kuota mizizi katika jamii yetu. Hivi sasa, kwa mfano, ni kawaida watu kumshambulia mtu hata yule wasiyemfahamu kwa sababu tu amejipambanua kuwa na mawazo tofauti na yale waliyonayo wao.

Hali hii ya ukosoaji na matusi ni kiashiria cha kukata tamaa kunakozidi kuota mizizi katika jamii yetu. Ni wazi watu wengi, ingawa wangependa kuwa na furaha, hawana furaha. Kuna hali ya watu kuishi na uchungu mkubwa ndani yao na hawajui wafanye nini kung’oa mizizi hiyo.

Limeibuka wimbi la watu kutafuta majibu ya matatizo yao kupitia njia za mkato. Kuna wanaokwenda kwa waganga wa kienyeji kwa ahadi ya kutatuliwa kwa shida walizonazo.

Kuna wanaokimbilia biashara za kitapeli kwa ahadi ya kupata utajiri wa haraka. Wengine wanakimbia kutoka imani moja kwenye imani nyingine kutafuta majibu ya shida zinazowasumbua. Haya yote ni mifano ya kitu kinachoitwa msongo wa mawazo.

Msongo wa mawazo ni maumivu ya kihisia anayokuwanayo mtu kama matokeo ya kukosa matumaini na kukata tamaa. Maumivu haya na kukosa matumaini, mara nyingi ni matokeo ya kutokufikiwa kwa matarajio. Mtu huyu anayeishia kukata tamaa, hufika mahali akakwama kifikra na hivyo kushindwa kuona njia ya haraka inayoweza kumfanya afikie matarajio aliyonayo.

Chukulia kijana aliyemaliza chuo kwa matumaini ya kupata kazi mara tu baada ya mahafali yake. Mwaka wa kwanza, mwaka wa pili, kijana huyu anatembea na bahasha ya kaki bila mafanikio.

Pamoja na jitihada kubwa anazofanya za kutafuta kazi, kijana huyu anashindwa kufikia ndoto na mipango aliyonayo ndani ya muda fulani. Ikiwa hivyo, taratibu hali ya kukata tamaa huanza kuchukua nafasi yake na hatimaye hukabiliwa na msongo wa mawazo. 

Mfano mwingine ni kuondokewa na mtu wa karibu katika maisha.  Anaweza kuwa mzazi, mwenzi wa maisha, mtoto, ndugu wa damu au hata rafiki wa karibu.

Kwa kawaida, hawa ni watu ambao kwa kiasi kikubwa wanahusika na mipango tunayokuwanayo. Hawa ndio wanaobeba thamani ya maisha yetu. Katika hali isiyotarajiwa, ghafla mtu huyu umpendaye anaondoka.

Kama hujawahi kufiwa na mtu wa karibu, ni vigumu kuelewa maumivu yanayosababishwa na kuondokewa na mtu uliyempenda. Maumivu haya humfanya mtu akapoteza ramani ya maisha na kila akitazama mbele hao ni dalili za mwangaza. Moyo unajaa masononeko na uchungu na hali ya kujihurumia kupita kiasi. Bila kupata msaada wa haraka mtu anaweza kujikuta akipatwa na kichaa tunachoweza kukiita msongo wa mawazo.

Pia kuna matukio mengine kama kuugua au kuuguza mtu kwa muda mrefu; kukosa au kufukuzwa kazi; kukataliwa, kusalitiwa au kuachana na mpenzi au mwenzi wa maisha; kukosa mtoto baada ya kujaribu kwa muda mrefu; kugombana na watu wa karibu kama ndugu au wafanyakazi.

Ipo mifano mingi zaidi ya hii inayochangia kukata tamaa. Hata hivyo, kwa ujumla msongo wa mawazo unachangiwa na ufahamu wa mtu kufika mahali akaona hakuna jibu rahisi tena la matatizo yanayomkabili.

Mtu kama huyu anaweza kujikuta akigombana na kila mtu kwa sababu tu, ndani yake anaishi na hasira ya kushindwa kufikia matarajio aliyokuwanayo. Itaendelea.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano: 0754870815 Twitter @bwaya

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles