23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

NIMR kutoa matokeo ya utafiti wa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi, ebola

Aveline Kitomary -Mwanza

TAASISI ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Bindamu (NIMR) kituo cha Mwanza, wanatarajia kutoa matokeo ya utafiti wa chanjo ya ebola na saratani ya shingo ya kizazi mwanzoni mwa mwaka 2021.

Utafiti wa ugonjwa wa ebola ulianza mwaka 2015 baada ya kutokea mlipuko katika nchi tano za Afrika ya Magharibi, ikiwemo ya Sierra Leone.

Akizungumza wakati wa kampeni ya ‘Tumeboresha Sekta ya Afya’ inayoendeshwa na maafisa habari kutoka Wizara ya Afya na taasisi zilizopo chini yake, Mtafiti Mwandamizi wa kituo hicho, John Changarucha, alisema tafiti hizo zitakuwa na nafasi kubwa ya kuishauri Serikali katika kulinda afya ya jamii.

“Mlipuko huo ulifanya dunia ije pamoja kutafuta chanjo itakayozuia ebola katika nchi hizo, sisi tulihusika na chanjo moja wapo tuliweza kushirikisha watu wazima 25 na wamepewa chanjo, tulivyomaliza chanjo iliweza kuzalisha kinga tulichokifanya ni kuwafuatilia hadi sasa” alisema.

Kwa saratani ya shingo ya mlango wa kizazi, alisema ni tatizo  kubwa kwa kanda ya ziwa kuliko sehemu zingine ila bado Serikali kupitia NIMR inaendelea na zoezi la ukusanyaji takwimu ili kupata uhakika zaidi wa ukubwa wa  tatizo. 

“Tunaamini chanjo ya HPV ikiweza kutolewa kwa walengwa wote, inaweza kupunguza saratani ya mlango wa kizazi ila cha muhimu itachukua muda kwasababu wanaochanjwa ni miaka 14, mwaka kesho tunatoa majibu ya utafiti tuliofanya,”alisema Changarucha.

Kwa mujibu wa Changarucha, utafiti mwingine ni wa chanjo ya mlango wa kizazi ili kuweza kutoa chanjo moja badala ya tatu.

“Kwa kawaida wanatakiwa kupata chanjo tatu, dozi ya kwanza ikitolewa ya pili baada ya miezi sita lakini bado kunachangamoto za utoaji huduma kuna ambao hawajapata chanjo kama inavyotakiwa.

“Nia ya utafiti ni kuwapa wengine chanjo moja, wengine mbili na wengine tatu ili kuona kama chanjo moja inaweza kutosha kukinga, tunafatilia kwa miezi 36 na tunatarajia kukamilisha Januari mwakani na kutoa matokeo kama chanjo moja inatosha tutashauri Serikali kutumia chanjo moja ili kuokoa fedha na muda utakaotumika kutoa chanjo zote,”alibainisha. 

Mtafiti Mwandamizi kutoka kituo hicho Dk Kidola Jeremiah, alisema utafiti mwingine wanaoufanya ni wa kufupisha matumizi ya dawa za kifua kikuu  (TB) ili kukabiliana na tatizo la usugu wa dawa kwa wagonjwa hao.

Alisema Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa yenye kiwango cha juu cha maambukizi cha ugonjwa wa kifua kikuu.

“Utafiti wa kufupisha dawa za kifua kikuu utaweza  kufanya wagonjwa kutumia dawa ipasavyo na kwa wakati, hii itapunguza tatizo la usugu wa vimelea kwa dawa, watatumia dawa kwa muda mfupi.

“Pia itasaidi kupunguza mzigo wa dawa unaoagizwa kwa wagonjwa wa kifua kikuu sasa wanatumia dawa nne kwa muda wa miezi sita, tunataka iwe moja tunayofanyia majaribio itumike kwa miezi minne,”alisema Dk Jeremiah.

Akizungumza mafanikio waliyopata kwa miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano, Mkurugenzi wa NIMR kituo cha Mwanza Dk. Safari Kinung’hi, alisema kituo hicho kimechangia kwa kiasi kikubwa juhudi za kitaifa za kudhibiti na kutokomeza magonjwa ya kichocho, minyoo ya tumbo, Ukimwi na malaria.

 “Tumetekeleza miradi 10 za kitafiti kukabiliana na kichocho na minyoo ya tumbo, tumegawa dawa kwa umma kwenye wilaya saba, tafiti za maji na usafi.

“Pia tulifanya utafiti kuelewa jinsi ambavyo konokono wa aina mbalimbali wanavyoweza kusambaza kichocho na mchango wa ugonjwa wa kichocho katika kueneza maambukizi ya Ukimwi,” Alisema.

Mbali na hayo, utafiti unaonesha maambukizi ya VVU ni tatizo kubwa kwa Mkoa wa Mwanza, huku kiwango cha maambukizi kikiwa asilimia 6.2, ambapo Mwanza ni miongoni mwa mikoa yenye viwango cha juu.

Dk. Safari Kinung’hi alisema NIMR imeendelea kutoa elimu inayolenga kubadilisha tabia, huku ikiendelea kutoa huduma za upimaji wa hiari na ushauri nasaha kwa jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles