Na HELLEN KIJO BISIMBA,
JULAI 23 mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilifanya mkutano wake mkuu maalumu wa kumchagua mwenyekiti mpya.
Nilipata fursa ya kufuatilia na kusikiliza hotuba ya mwenyekiti huyu mpya wa CCM ambaye pia ndiye Rais wa nchi, ambapo nilivutiwa na baadhi ya mambo nikiwa mtetezi wa haki za mtoto, pale alipowataka wajumbe wa mkutano huo kutafakari uwepo wa watoto wadogo katika siasa kwa jina la chipukizi wa chama.
Alihoji watoto hawa wakiwa kwenye shughuli hizo za chipukizi wanasoma saa ngapi? Pia alionesha wasiwasi kuwa iwapo kila chama kati ya vyama vyote vilivyosajiliwa vikiwa na watoto hao ambao wako kati ya miaka nane hadi kumi na tano wataenda kupata elimu yao wakati gani?
Bila shaka wajumbe wa mkutano mkuu wamemsikia na walichukulie hili kwa makini kwani elimu ya watoto ni muhimu lakini pia kwa umri wao huo si vyema kuhusishwa katika masuala ya siasa.
Nimemsikia mwenyekiti huyu mpya akielezea suala la rushwa ndani ya  chama. Hapa nimemuona amekuwa na ujasiri mkubwa sana kuongea mbele ya wenye chama kuwaonyesha udhaifu mkubwa aliouona na akatolea mfano Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na jinsi alivyoona rushwa ikiwa nje nje.
Alionyesha jinsi katiba na kanuni za chama zinavyokubaliana na katiba ya nchi katika kupinga rushwa. Alinukuu kifungu cha 3 cha katiba ya CCM kuwa rushwa ni adui wa haki.
Mwenyekiti huyu wa CCM amesema kuwa yeye aliweza kuwania nafasi hiyo kubwa na akaweza kuipata bila kutumia rushwa. Napenda kumwamini na kumpongeza kwa hilo.
Tukumbuke jinsi ambavyo suala hili lilivyoota mizizi kiasi hata Bunge ambalo huwa na wabunge wengi kutoka CCM waliwahi kupitisha sheria iliyojulikana kama sheria ya Takrima ambayo kwa uhakika ilikuwa inahalalisha rushwa.
Kwa mwenyekiti mpya kusimama mbele ya mkutano uliomchagua na kuwaonyesha udhaifu huu na kuwa atapambana nao ni jambo la kutia moyo sana, tunaamini inawezekana kama mwenyewe alivyosema.
Mwenyekiti mpya huyu pia ameelezea  kuwa nchi yetu ni ya  amani, inayofuata demokrasia. Katika hili kuna ukweli kiasi. Nchi yetu haina vita kwa hiyo ina amani. Lakini nchi yetu kuna watu wasio na amani.
Utafiti uliofanyika mwaka uliopita kupima kiasi cha furaha ya watu katika nchi ilionekana Watanzania ni watu wasio na furaha na wengi wana manung’uniko, hivyo hapa tunaona amani iko shakani kutokana na masuala mbalimbali.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimetoa taarifa ya nusu mwaka ya hali ya haki za binadamu nchini. Taarifa  inaonyesha jinsi gani nchi hii ya amani ilivyo na watu wengi wasio na amani. Suala la ukatili wa kijinsia, wanawake wapatao 7,475 walifanyiwa ukatili wa aina mbalimbali na kutoa ripoti polisi katika miezi sita tu.
Kati yao 2,850 walibakwa. Watoto 1,491 nao walibakwa. Wapo wazee waliouawa kwa sababu za kishirikina wapatao 394.
Wapo watu waliouawa na watu waliojichukulia sheria mkononi wapatao 135. Watu wenye ualbino wameendelea kuishi na wasiwasi na wanne kati yao walifanyiwa vitendo vya ukatili vya kunyofolewa viungo vyao. Hii si amani. Naamini mwenyekiti wa chama kinachotawala ataangalia dawa.
Pia tukumbuke hata polisi ambao ndio walinzi wetu waliuawa na kuumizwa na vituo vitano vya polisi kushambuliwa, hapa amani iko shakani iwapo hata walinzi wetu nao wanauawa na kuvamiwa.
Kwenye demokrasia Katiba ya Tanzania ibara ya tatu inatamka kuwa ni nchi ya  demokrasia, tena demokrasia ya vyama vingi.
John Cheyo alipoongea katika mkutano huo alitoa ufafanuzi kuwa si kweli kuwa Rais Magufuli amekataza mikutano ya hadhara au siasa bali amekataza ile yenye shari. Eneo hili linatakiwa kufanyiwa kazi na Rais akiwa ni mwenyekiti wa chama kuhakikisha vyama vyote vya siasa vinapata nafasi sawa katika kukua na kuendeleza vyama vyao vya siasa ili demokrasia ya vyama vingi nchini iweze kuendelea na kukua kwa mujibu wa katiba.
Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).