24.1 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

‘Nilikataa kufanyiwa upasuaji ili kuondoa nuksi ndani ya ukoo’

wert
Priska Willison akiwa amempakata mwanawe, Kulia ni mwandishi wa makala haya.

 

* Mtoto alitanguliza makalio badala ya kichwa

Na Pendo Fundisha, Mbeya

ZIPO sababu nyingi na ushahidi wa kisayansi unaonyesha kuwa, ndoa na mimba katika umri mdogo wa chini ya miaka 18 ni hatari kwa afya ya mama na mtoto.

Wasichana katika umri huu nyonga zao huendelea kukua na mara nyingi huwa changa na finyu kiasi kwamba husababisha matatizo mengi ya uzazi wakati wa kujifungua kwa njia ya kawaida.
Wasichana wengi huchelewa kujifungua au huchukua saa nyingi za uchungu kabla ya kujifungua, hali hii inaweza kusababisha kifo cha mama, mtoto au wote wawili kama matibabu ya dharura ya upasuaji hayakufanyika.

Wasichana wanaopata ujauzito na kujifungua katika umri mdogo wengi wao pia hupata tatizo la fisitula na kusababishia kutokwa na haja ndogo au kubwa bila kujizuia.

Tatizo lingine linaloambatana na mimba katika umri mdogo ni pamoja na kutokwa na damu nyingi pale mimba inapoharibika, kupata uambukizo wa bakteria katika njia ya kizazi pamoja au kifafa cha mimba.
Wasichana wadogo mara nyingi huzaa watoto wenye uzito pungufu au njiti, watoto wa namna hii hukabiliwa na hatari pamoja na changamoto nyingi za kiafya katika umri wa chini ya miaka mitano.

Watoto wengi hupata matatizo ya mtindio wa ubongo na hali hii ndio iliyomkuta Fedrick Emmanuel (19) mwenye ulemavu wa viungo na mtindio wa ubongo.

Mama mzazi wa kijana huyo, Priska Willison mkazi wa Kata ya Iganzo Mtaa wa Mwambenja mkoani Mbeya, anasema alizaliwa mwaka 1980 na mwaka 1996 alibahatika kuolewa akiwa na umri wa miaka 16.

Priska ni mama wa watoto wanne ambapo mtoto wake wa kwanza alimzaa mwaka 1997 akiwa na umri wa miaka 17.

Mama huyu anasimulia madhara makubwa yaliyompata kutokana na kuzaa akiwa na umri mdogo.

“Mara tu nilipoolewa kwa kushinikizwa na wazazi wangu nilishika ujauzito na kufanikiwa mwaka 1997 mtoto Fedrick katika Hospitali ya Wazazi ya Meta kwa njia ya kawaida.

“Madaktari walinishauri nifanyiwe upasuaji kutokana na nyonga zangu kuwa ndogo lakini mimi na familia yangu hatukukubaliana na uamuzi huo.

“Tuliamini kwamba tendo hilo litaleta nuksi ndani ya ukoo, hivyo nililazimisha kuzaa kwa njia ya kawaida jambo ambalo hivi sasa linaniumiza roho yangu kwa mateso niliyomsababishia mwanangu,”anasema mama huyu kwa uchungu.

Anasema wakati akijitahidi kumsukuma mtoto atoke nguvu zilimuishia na wakati huo mtoto alikuwa ametanguliza makalio badala ya kichwa.

“Wauguzi walipoona hali hiyo wakaamua kumvuta mtoto. Wakati mwanangu akiendelea kukua ndipo nilipobaini kwamba mbali na ulemavu wa viungo pia alikuwa na tatizo la akili.

“Madaktari walinieleza kwamba tatizo hili lilitokana na kutolewa ndani kwa kuvutwa hivyo hawezi kubadilika na kwmaba hicho ni kilema chake cha maisha,”anasema.

Anasema baada ya kuelezwa kwamba yeye na familia yake ni miongoni mwa watu waliomsababishia matatizo ya ulemavu mtoto huyo aliumia sana na kuamua kumuachia Mungu.

“Licha ya kwamba watoto wangu wengine nilibahatika kuwazaa wakiwa wazima na kwa njia ya kawaida lakini nimejifunza kutokana na makosa,” anasema.

Mama huyo anasema anakutana na changamoto na majaribu mengi kutoka kwa baadhi ya ndugu wa mumewe na jamii inayomzunguka.

“Wapo watu wanadai kwamba mtoto huyu tumeamua kumfanya hivi eti kwa kutafuta utajiri jambo ambalo halina ukweli, na wengine wanadai kuwa tunamfungia ndani bila ya kumtoa nje kwa kuogopa aibu, jamani kama ni hivyo basi tungeweza kumuua akiwa bado mdogo,”anasema mama huyo huku akibubujikwa na machozi.

Anasema maisha yake na mumewe Emmanuel John ni magumu ambayo yanahitaji misaada mbalimbali.

“Lakini kubwa zaidi ni upendo kuliko masimango kwani yanazidi kuniumiza na kuniweka kwenye kundi ambalo halistahili kuishi duniani.

“Uelewa mdogo wa masuala ya afya ya uzazi ndio uliochangia kupatikana kwa kijana Fedrick akiwa hivi, lakini nimejifunza mengi na ninachowaomba Watanzania ni msaada kwani mtoto huyu anahitaji malezi ya karibu zaidi,”anasema mama huyo.

Anasema wakati mwingine analazimika kumuacha mtoto huyo ndani na kwenda kutafuta chakula na fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto wengine ambao wanaendelea na elimu ya msingi na wengine sekondari.

“Sina sababu ya kuficha ukweli wa mtoto wangu, nimemzaa mwenyewe na hao wanaodai kwamba mimi ninamficha ndani waombe hali hii isiwakute.

“Sipendi kumuacha Fredrick ndani peke yake lakini nitafanyaje wakati mimi na mzazi mwenzangu wote kipato chetu ni kidogo,” anasema.

 

Anasema walihangaika sana kutafuta matibabu licha ya madaktari kuwaeleza kwamba ulemavu wa mtoto huyo ni wa maisha yake yote.

 

Anasema kadiri mtoto huyo alivyokuwa akiendelea kukua ndivyo matatizo hayo yalivyokuwa yakizidi kuongezeka na hali ya kuanza kutoa mate ilianza.

 

 

Kijana huyo ambaye anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, tayari baadhi ya wasamaria wema wamejitokeza na kumnunulia baiskeli na nguo.

 

Watanzania kijana huyu anahitaji msaada kwani licha ya kufanikiwa kulelewa na baba na mama lakini wazazi wake wanashindwa kumudu gharama za matunzo yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,699FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles