28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

NIKIWA MAKONDA, NITAONESHA JEURI YA KUMSAIDIA RAIS

NA ANDREW MSECHU                            |                         


KILA kukicha, tunakutana na mambo mapya. Vituko vya viongozi wa kisiasa na hasa wateule wachache vimeendelea kuwa sehemu ya kujenga tafakari mpya.

Naungana na Watanzania wenzangu kushuhudia mengi, kwa wiki nzima sasa ikiwa ni msigano wa mawazo, fikra, madaraka na mamlaka baina ya mkuu wa mkoa, mkuu wa nchi, kiongozi mstaafu na umma.

Huenda chanzo cha haya yote kimeanzia mbali, wala si suala la ‘makontena ya Makonda’ yanayodaiwa kuwa na vifaa kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam na shinikizo lake la kutaka yasamehewe kodi, bali namna ambavyo mkuu huyu wa mkoa amekuwa akitumia nafasi yake kujipa ‘uungu mtu’.

Hata baada ya mkuu wa nchi kueleza hadharani alipokuwa akizungumza na viongozi huko Chato, akieleza namna mteule wake alivyokengeuka katika suala hilo, bado mteule hakukaa kimya, alihakikisha kwamba anawajibu waliotaka atenguliwe au ajitengue kwa kuwarushia vijembe.

Agosti 30, Rais Dk. John Magufuli, alionekana kumkemea Makonda kwa kitendo chake cha kutaka makontena 20 anayodai yana vifaa vya shule za Dar es Salaam, yatoke bandarini bila kulipiwa kodi ya Sh. bilioni 1.2.

Baada ya kauli hiyo ya Rais, watu kwenye mitandao ya kijamii walionekana kubashiri kuwa, siku za Makonda ofisini zinahesabika na kuwa, wakati wowote Rais angetengua uteuzi wake.

Jumapili, Septemba 2, mwaka huu kiongozi wa muda mrefu ambaye kwa sasa amestaafu shughuli zake serikalini, Prof. Mark Mwandosya naye aliandika katika ukurasa wake wa Twitter, akisema alivyofundishwa misingi ya Utawala Bora, mkuu wa nchi akimkosoa mtumishi hadharani, anapaswa kuandika barua ya kujiuzulu.

Ingawa hakumtaja Makonda moja moja, lakini ni wazi kuwa alimlenga Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa kuwa ni siku chache tu baada ya Rais Magufuli kumkosoa Makonda hadharani na kumtaka alipe kodi hiyo.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Privatus Karugendo pia aliandika mtandaoni akimweleza Prof. Mwandosya kuwa misingi ya uwajibikaji anayoisema haijapitwa na wakati, ila wazee wameshindwa kujenga utamaduni wa kuwajibika.

Alisema kwa namna hiyo, vijana wadogo wanaoingia katika uongozi zama hizi hawana mahala pa kujifunza, kwa kuwa kwa sasa hakuna utamaduni wa kujiuzulu, si kwa kujenga heshima tu, bali pia ni kumsaidia Rais, kufanya uamuzi mgumu na wepesi wa kuliongoza Taifa.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania, Abdul Nondo hakubaki  nyuma, aliandika kwenye mtandao akimjibu Prof. Mwandosya, akisema kwa sasa kiongozi wa umma anaweza kuishi akiwa hajui hata anaongozwa na kanuni zipi za uongozi wa umma au sheria zipi.

Alisema Yeye (kama alivyo Makonda) anafanya kazi anavyojisikia tuu, ilimradi aambiwe ni mbunifu au anayethubutu basi wala hajali kuhusu maadili ya uongozi, hayo sio kipaumbele sasa.

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kupitia barua yake ya wazi kwa Rais Magufuli kutoka Ubelgiji anakoendelea kupata matibabu baada ya shambulio la risasi Septemba, mwaka jana hakubaki nyuma katika hili, alielezea sakata hilo na kuzusha hoja kadhaa.

Alitaka mjadala wa makontena hayo usiishie tu kumtaka kiongozi huyo kuambiwa akalipe kodi, bali uende mbali zaidi kwa kuangalia uwezekano wa kuwapo makosa mengine ya kijinai.

Hatua inayoshangaza ni ule ujasiri alionao Makonda, hakukawia, siku hiyo hiyo aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa wahenga wana methali nyingine kama mvumilivu hula mbivu.

Akaandika tena: “Bado mnasubiri? Wahenga walisema subira yavuta kheri…maisha yanaendelea,”

Anasahau kwamba zipo semi nyingine, ikiwamo ile ya ‘Mtu mzima ukivuliwa taulo, chutama” ili kuficha aibu, hata kama maisha yanaendelea.

Nikakumbuka, huyu huyu ndiye ambaye ameonekana kuwa ‘mtoto mpendwa’ wa mamlaka ya juu ya uteuzi nchini, akiwa na majigambo siku zote kwamba anao uwezo wa kufanya lolote wakati wowote, huku akitajwa mara kadhaa kwa mkoa wake kutofanya vizuri katika ukusanyaji mapato, kisha kutokuwa na utekelezaji mzuri wa Ilani ya chama tawala.

Ninapata nafasi ya kujaribu kutafakari, ninajaribu kujivika nafasi ya Mkuu wa Mkoa, nikiwa nimekabidhiwa dhamana ya kuongoza mkoa huu muhimu katika nchi hii.

Katika nafasi yangu, sitarajii jipya sana, lakini niatarajia kufanya tofauti katika suala la uwajibikaji kwa nafsi yangu, kwa nchi yangu na kwa wananchi.

Uwajibikaji wangu kwa wananchi hauna maana ya kumfurahisha mwenye mamlaka ya uteuzi, bali kuwajibika kuhakikisha ninatekeleza majukumu yangu katika namna ambayo hata mamlaka iliyoniteua inaweza kufurahia namna ninavyochapa kazi.

Ninapokuwa katika nafasi hii, ninapenda kuonesha ni kwa namna gani nitawajibika katika maneno yote, hakika nitafanya tofauti na huyu ambaye amekuwa gumzo katika vinywa vya watu, mitandao ya jamii na hata katika vyombo vya habari.

Katika kutekeleza majukumu yangu, nitahakikisha ninaheshimu sheria, miongozo na taratibu zinazonipa dhamana ya wadhifa wangu.

Nikiwa mkuu wa mkoa ninayejua kwamba ninapendwa na wenye mamlaka ya uteuzi kiasi cha umma kutambua mapenzi yao kwangu, tofauti na ilivyo kwa wengine, nitatumia nafasi hiyo kuwajibika kwa kuheshimu mipaka yangu.

Ninajua, ninaweza kupata ‘bichwa’ na kujiona mimi ni mtoto mpendwa kutokana na baadhi ya sifa zinazotolewa na walionipa nafasi hii hadharani, lakini hii haitakuwa kigezo cha kujiona nimeshamaliza kila kitu na kwamba hakuna maisha baada ya hapa.

Nitafanya tofauti, pale tu mamlaka zilizoniteua zitakapoanza kuniumbua hadharani kwa kuniambia kwamba mkoa wangu umekuwa miongoni mwa mikoa isiyokuwa na ushirikiano mzuri baina ya watumishi, nikiwamo mimi na wasaidizi wangu, nitahitaji kuangalia nilikojikwaa, kuanza kushirikiana upya na wasaidizi wangu.

Itakapotokea kwamba ndani ya muda mfupi ninazidi kutajwa hadharani na wakuu wangu, wakidai kwamba mapato ya mkoa ninaouongoza, ambao ndio wenye vyanzo vingi vya mapato kuliko mikoa yote, yameshuka na kuzidiwa na mikoa isiyo na vyanzo vya maana nitasikitika. Kama si jambo la mkakati baina yangu na wao basi nitaanza kuangalia namna ya kujisaidia.

Ninajua, kuwa ninaweza kuwa nimefanya mkakati kwa ushirikiano kwa ajili ya kujenga picha hasi ya mkoa ninaouongoza ili kuwashughulikia wale ninaodhani kuwa labda wataonekana kuwa mahasimu wangu na kuwa ndio chanzo cha kuporomoka kwa mapato, lakini hii sitakubali iwe aibu yangu, nitafanya tofauti kwa kuwa najua kuna maisha baada ya kesho, hasa katika umri wangu huu mdogo.

Hakika, nitafanya tofauti kwa kuangalia mipaka yangu ya kiutendaji. Hasa kwa kujua kuwa kutiliwa shaka na aliyeniteua na kunitaja hadharani kama mtu niliyekengeuka ni ujumbe mzito kwangu kwamba nafasi hiyo hainifai tena.

Nitafanya tofauti kwa kuhakikisha ninaacha wazi nafasi hiyo kwa kuwa kama ningekuwa nastahili, akiwa mtu wangu wa karibu angeweza kunieleza kwa aidha mawasiliano ya simu, kuniita ofisini na kuzungumza naye, au kunitumia ujumbe kupitia kwa watu wake wa karibu iwapo nimefanya jambo lisilofaa.

Nitafanya tofauti, kwa kuwa si hulka njema kuomba radhi kila mara katika mambo yaliyo chini ya uwezo, bali kuchukua hatua kuonesha kuwa uwezo wangu unatakiwa kutumika katika mambo ya msingi.

Katika hili la kumsaidia Rais, sitachelewa kuonesha namna nilivyo na uwezo na upendo mkubwa kwake, nitafanya tofauti kwa kuchukua hatua ya kujiuzulu, ikiwa ni sehemu ya kumsaidia katika mawazo ambayo tayari nimeshamsababishia na yale ambayo huenda nitamsababishia baadaye, nikiamini kwamba kuna maeneo mengine mengi tunayoweza kushirikiana na nitakayoweza kumsaidia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles