NIAMEY-NIGERERIA
NIGERIA imesaini makubaliano ambayo yanalenga kuongeza biashara kati ya nchi za Afrika (AfCFTA).
Hatua hii sasa inaifanya Eritrea kuwa nchi pekee ya Kiafrika kuachwa nje.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari alisaini makubaliano hayo ya kihistoria katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU), huko Niger.
Hatua ya kwanza chini ya makubaliano hayo ni kupunguza ushuru wa bidhaa kutoka nchi zilizo ndani ya Umoja huo lakini muda wa kufanya hivyo bado haujatangazwa.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la AFP, kwa sasa nchi za Kiafrika zinafanya huduma na biashara kati yao kwa asilimia 16 tu wakati nchi za Ulaya ni asilimia 65.
AU inakadiria kuwa kwa utekelezaji wa Biashara huru kwa Bara la Afrika AfCFTA – utalifanya bara hilo liongoze hadi asilimia 60 ya biashara kati yao kufikia 2022.
Pia wanasema kuwa makubaliano ya AfCFTA yatatengeneza nafasi kubwa zaidi ya biashara huru duniani.
Makubaliano ya AfCFTA yaligonga mwamba mwaka jana wakati Nigeria ilipotangaza kutosaini siku chache kabla ya nchi hiyo kuelekea kusaini makubaliano hayo.
Nigeria ni Taifa kubwa linaloongoza kiuchumi barani Afrika, wakati iliposita kusaini makubaliano hayo hatua hiyo ilizua maswali iwapo makubaliano hayo ya kibiashara yatafikiwa na kutekelezwa na umoja huo.
Rais Muhammadu Buhari alisema alikuwa anahitaji mashauriano zaidi nchini kwake Nigeria.
Tangu wakati huo, Nigeria ilieleza kuwa ilifanya mashauriano na na makundi yapatayo 27, vikiwamo vyama vya wafanyabiashara.
Wachambuzi wanasema uamuzi huo unaifanya Nigeria kuwa na mengi ya kupata kwa kuongeza upatikanaji wa bidhaa na huduma zake kwenye soko pana la Afrika.
Lakini wengi waliofuatwa kwa ajili ya kutoa ushauri juu ya makubaliano hayo walionyesha wasiwasi kwamba kuongezeka kwa ushirikiano huo kungeleta ushindani usio wa haki hasa kwenye eneo la ajira na bidhaa wanazozalisha.
Hatua ya Nigeria kusaini ndoto za kuongeza biashara kupitia AfCFTA, ni hatua ya karibu mbele.
Sasa AfCFTA inaweza kutoa fursa ya soko kubwa la Nigeria, na kama chombo na kwa nafasi yake ipo katika nafasi imara ya kuzungumza na maeneo mengine duniani.
SABABU ZA ERITREA KUACHWA
Kwa mujibu wa Kamishna wa Viwanda na Biashara wa AU, Albert Muchanga, Eritrea haikushiriki katika mazungumzo hayo kwa sababu ya mgogoro wake na Ethiopia.
Aliongeza kuwa sasa nchi hizo mbili hazina mgogoro na Eritrea tayari imeiomba AU kwenda pamoja kwenye makubaliano hayo.
“Kwa hiyo baada ya muda watakuja, tutakwenda nao, ” alisema.
Chini ya makubaliano hayo ushuru utapunguzwa kwa nchi wananchama zilizosaini.
Ushuru ni kama ule wa kodi zikiwamo zile zinazotozwa mipakani.
Pia makubaliano hayo yanalinda bidhaa zinazozalishwa kutoka mataifa ya Afrika.
BBC