22.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

Nigeria kutuma ndege kuokoa raia wake Afrika Kusini

LAGOS, NIGERIA

RAIA wa Nigeria wanaoishi Afrika Kusini wamepewa ofa ya ndege za bure kurejea nyumbani kukwepa vurugu za kibaguzi zinazoendelea nchini Afrika Kusini.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria imesema mmliliki wa Shirika la Ndege la Air Peace yupo tayari kuwasafirisha bure wale wote watakaotaka kurudi nyumbani kwao siku ya Ijumaa.

“Wote watakaotaka huduma hiyo wanashauriwa kuwasiliana na Ubalozi wa Nigeria jijini Pretoria na ofisi ndogo za ubalozi jijini Johannesburg kwa matayarisho muhimu,” taarifa ya wizara imeeleza.

Mashambulizi ya biashara zinazomilikiwa na wageni nchini Afrika Kusini yamepokelewa kwa hasira kali hasa na Wanigeria ambao wanahisi wanalengwa na kuonewa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Geoffrey Onyeama amewaambia wanahabari juzi kuwa kulingana na taarifa zilizowafikia, hakuna raia wa Nigeria aliyepoteza uhai kwenye ghasia zinazoendelea.

Hata hivyo, amesema kuwa serikali inaangalia uwezekano wa kumrejesha nyumbani balozi wake kutoka Afrika Kusini na kudai fidia kwa biashara zote za raia wa nchi hiyo zilizoharibiwa.

Aidha Nigeria imesusia kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaofanyika Afrika Kusini kutokana na ghasia hizo zinazoendelea.

Zaidi imetoa onyo kwa raia wake waliopo Afrika Kusini wakiwataka kutosafiri ama kuelekea kwenye maeneo ambayo ghasia hizo zimeshamiri hadi pale hali itakapotengemaa.

MTN WAFUNGA BIASHARA

Wakati huo huo waandamanaji nchini Nigeria wamevamia biashara za kampuni za Afrika Kusini kama njia ya kulipiza kisasi.

Kampuni hizo zilizoshambuliwa ambazo zimewekeza nchini Nigeria ni pamoja na kampuni kubwa ya mawasiliano ya simu- MTN iliyolazimika kufunga vituo vyake vya biashara kote nchini Nigeria.

Mwanzoni mwa wiki Raisi Muhammadu Buhari alisema kuwa anamtuma mwakilishi wake kwenda Afrika Kusini kueleza ghadhabu zao juu vurugu zinazoendelea.

Kama njia ya kuonyesha kukasirishwa na vitendo vya kibaguzi vinavyofanywa na Waafrika Kusini, juzi Muimbaji wa muziki nchini Nigeria Tiwa Savage alitangaza kujiondoa kwenye tamasha alilokuwa amepanga kushiriki nchini Afrika Kusini baadaye mwezi huu.

Mwanamuziki huyo wa nyota wa mtindo wa Afrobeats alikuwa amepangiwa kufanya shoo katika jukwaa kuu la tamasha la DSTV Delicious Jumamosi ya Septemba 21 mjini Johannesburg, mji ambao kumeshuhudiwa ghasia kubwa na uporaji wa maduka mengi yanayomilikiwa na raia wa kigeni kutoka mataifa ya Afrika.

Kabla yake, msanii Burna Boy pia kutoka nchini Nigeria ameapa kutokanyaga Afrika Kusini baada ya ghasia dhidi ya raia wa kigeni kuzuka upya nchini humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles