NI wakati mwingine kwa mashabiki wa soka duniani kushuhudia uhondo wa mechi kubwa ya Ligi Kuu Hispania kwa miamba Real Madrid na Barcelona kuvaana katika Uwanja wa Santiago Bernabeu saa 2:15 usiku leo.
Mchezo huu utakuwa ni zaidi ya vita kwa timu hizo kutokana na kupishana pointi chache kwenye msimamo wa ligi, Barca ikiwa kileleni kwa pointi 27 na Real ikiwa nazo 24, huku zikifukuziwa kwa karibu na Atletico Madrid iliyojikusanyia 23.
Vita imekolea hapo, kwani kupoteza mchezo kwa Barcelona kutamfanya afikiwe na Real, ambaye naye akifungwa atakuwa amepoteza nafasi ya pili kwa kushuka hadi ya tatu kama Atletico Madrid itainyuka Real Betis keshokutwa.
Itakuwa ni vita kubwa kwa makocha wawili wa timu hizo, Rafael Benitez (Real) na Luis Enrique (Barca), wote wakiwa wanaujua utamaduni wa timu zao kwa kuwa waliwahi kuzifundisha timu za vijana kabla ya kuondoka na kurejea tena walipoanzia.
Zifuatazo ni dondoo mbalimbali kuhusu mechi hiyo;
UREJEO WA MESSI, MAJERUHI
Staa wa Barcelona, Lionel Messi, amefanya mazoezi na timu kubwa tokea juzi, hiyo inamaanisha kuwa atakuwepo kwenye mchezo huo. Hakuna aliyetarajia urejeo huo, hasa kutokana na staa huyo kuwa nje ya dimba kwa takribani siku 54 akiuguza majeraha.
Tofauti na miaka mingine, msimu huu Barca imefanya vema bila hata ya uwepo wa Messi, ikifanikiwa kushinda mechi saba, sare moja na kupoteza moja, ikibebwa sana na Neymar Jr na Luis Suarez, ambao wako kwenye moto hivi sasa.
Hivyo haitashangaza kushuhudia Messi akianzia benchi ili kumlinda kwa kumwepusha na majeraha kutokana na kasi na presha ya mchezo huo, huku staa huyo akiwa amekosa mechi nyingi wakati akiuguza majeraha yake.
Kiungo wa Barca, Rafinha, ataendelea kukosekana, Rakitic naye yupo hatihati ya kucheza mchezo huo, Real Madrid watamkosa kipa wake Keylor Navas, Karim Benzema atarejea, huku beki Sergio Ramos, anayesumbuliwa na majeraha ya bega akitarajia kuchomwa sindano za kuondoa maumivu na kukipiga kwenye mchezo huo muhimu..
MARCELO V ALVES
Moja ya vita itakayokuwa kwenye mchezo huo ni upande wa kulia wa Barcelona, hii itamhusisha beki wa kulia, Dani Alves na beki wa kushoto wa Real, Marcelo.
Marcelo mpaka sasa bado hajapewa heshima yake na baadhi ya watu, lakini ni mmoja wa wachezaji wabunifu ndani ya Real Madrid, hivi sasa amekua, yupo sawa na anafanya kazi kubwa kwenye kushambulia na pia kuzuia.
Beki huyo anatarajia kumpa wakati mgumu Dani Alves, ambaye hivi sasa si yule tena wa miaka miwili au mitatu iliyopita. Amekuwa na makosa kwenye ukabaji, hasa pale mpira unapokuwa upande mwingine na kama amepanda mbele, amekuwa mgumu sana kurejea kwenye eneo lake.
Hivyo kwa mipira yote ya kushambulia ya Marcelo upande wa kushoto akisaidiwa na viungo au Ronaldo, itamfanya Alves kuwa kwenye wakati mgumu katika mchezo huo.
MFUMO, MBINU
Bila Messi, Barca imejaribu mifumo tofauti, ikicheza 4-2-3-1 na 4-4-2, ambayo ilifanya kazi vizuri, kutegemea litakalotokea kwa Rakitic, bado watatumia washambuliaji watatu.
Hiyo inamaanisha kuwa Munir El Haddadi atacheza mbele sambamba na Suarez na Neymar kama Messi ataanzia benchi. Mascherano anarejea, hivyo atacheza na pacha wake, Pique kwenye beki ya kati huku kiungo mkabaji Busquets, akikaa mbele yao na kipa Claudio Bravo akisimama langoni.
Real Madrid, iliyotoka kufungwa 3-2 dhidi Sevilla, ina haja ya kutafuta usawa kati ya washambuliaji ambao hawakabi mara nyingi na viungo, Benzema hayupo fiti asilimia 100, hivyo Benitez ana kazi ya kuwafanya Bale na Ronaldo wacheze pamoja na kufunga mabao tofauti na mechi zilizopita.
Tatizo kubwa la Real ni kocha wao, Benitez, kuifanya timu hiyo icheze soka la ulinzi zaidi kuliko kushambulia, jambo ambalo limepelekea Ronaldo ashindwe kung’ara sana msimu huu.
Hata mashabiki wamemlalamikia Mhispania huyo, wakidai anawachosha wachezaji kutokana na soka wanalocheza, Ronaldo inadaiwa tayari amemueleza bosi wa timu hiyo, Florentino Perez, kuwa hawawezi kushinda taji lolote chini ya kocha huyo.
Barca ni timu iliyokuwa na kiwango bora mpaka sasa, hata rekodi zinaibeba, kwani kwenye mechi sita zilizopita imeruhusu wavu wake kuguswa mara moja tu. Neymar na Suarez, wameonyesha kuwa hawajammisi Messi, Busquets naye yupo vizuri sana.
WAFUNGAJI MAHIRI
Licha ya Messi kuwa ndiyo mchezaji kinara wa El Clasico, mchezo huo utakutanisha nyota watatu wanaoongoza kwa mabao La Liga Neymar, Suarez na Ronaldo, ambao wataingia dimbani kusaka ushindi ili kuzibeba timu zao.
Mpaka sasa kuelekea raundi ya 12, Barca ndiyo yenye safu kali ya ushambuliaji zaidi ya Real, Neymar akiwa amefunga mabao 11, akifuatiwa na Suarez aliyefunga tisa na Ronaldo wa Real akiwa anajikongoja kwa kutupia nane.
Hivyo linaweza likawa pambano litakalokuwa na mabao kwa pande zote mbili kutokana na rekodi kuonyesha kuwa hakuna timu iliyoweza kushinda bila wavu wake kuguswa na kwa aina hiyo ya washambuliaji inadhihirisha hilo.
REKODI ZAO
Msimu uliopita zilipokutana kwenye uwanja huo, wenyeji Real walishinda 3-1, mabao yaliyofungwa na Ronaldo, Pepe na Benzema.
Katika michezo 58 waliyokutana Barcelona imeshinda mara 25, Real 17 na mechi 16 zimekwisha kwa sare na mechi nane zao zilizopita zimekwisha kwa pande zote mbili kufunga mabao.
Real Madrid haijafungwa nyumbani kwenye mechi 22 zilizopita, ikishinda 19 na sare tatu, huku Barcelona ikitupia mabao 41 katika mechi zao za mwisho 15, ukiwa ni wastani wa mabao 2.7 kwa mchezo.
Kocha wa Real Madrid, Benitez, ataingia uwanjani kwenye mchezo wake wa 12 dhidi ya Barcelona, kuanzia alipokuwa kocha wa Valladolid, Extremadura, Valencia na Liverpool, akishinda saba, sare 1 na vipigo vinne.
Messi anakaribia rekodi nyingine ya kuwa mfungaji bora kwenye mechi za El Clasico, kwenye mechi zake 18 za La Liga dhidi ya Real, amefunga mabao 14, sawa na Alfredo Di Stefano, nane kati ya hayo amefunga kwenye jiji la Madrid.
MAN CITY VS LIVERPOOL
Kimbembe kingine kitakuwa kwenye Ligi Kuu England, kwa wenyeji Manchester City kuvaana na Liverpool iliyojengwa upya chini ya Mjerumani Jurgen Klopp, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Etihad, saa 2:30 usiku.
Klopp aliiongoza Liverpool kupata kipigo cha kwanza dhidi ya Crystal Palace (2-1) tokea akabidhiwe mikoba hiyo, atakuwa na mtihani wa kurejesha tena makali kwa kuichapa Man City, ambayo itaongezewa nguvu kwa kurejea kikosini kwa nyota wake, Sergio Aguero na David Silva.
Urejeo wa nyota hao unatarajia kuipa wakati mgumu Liverpool kutokana na ubora wao na namna walivyohusika kuibeba City kwenye mechi zilizopita kabla ya kupata majeraha.
Klopp atakuwa akijipa matumaini ya kuiharibia Man City ugenini, kama alivyoifanyizia Chelsea kwao kwa kuidunga mabao 3-1, lakini City iliyo kileleni ndiyo timu inayopewa nafasi kubwa ya kuchukua taji msimu huu.
Beki wa Liverpool, Mamadou Sakho, atakosekana baada ya kupata majeraha, lakini Klopp anatarajia kumpa nafasi Dejan Lovren, ili kuonyesha thamani yake ya pauni milioni 20 iliyotumika kumsajili ya msimu uliopita.
Vita kubwa inatarajiwa kuwa kati ya viungo washambuliaji, Kevin De Bruyne wa Man City na Philippe Coutinho wa Liverpool, kutokana na nyota hao kuwa watengenezaji wa mabao ya timu zao na vilevile wafungaji.
REKODI ZAO
Man City imeshinda mechi nne na kutopoteza hata mmoja kati ya sita za Ligi Kuu England zilizopita dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Etihad, pia imefungwa mchezo mmoja kati ya sita iliyopita ya ugenini, ikifungwa na Man United (ikishinda miwili, sare tatu na kupoteza mmoja).
Coutinho amefunga mabao matatu kwenye mechi tatu zilizopita dhidi ya Man City, ambayo kipa wake, Joe Hart, amedaka mechi nyingi bila kufungwa bao (mara 14) mwaka huu dhidi ya kipa wa Liverpool, Simon Mignolet aliyefanya hivyo katika michezo 13.