Na CHARLES KAYOKA,
NAJUA wanaosoma makala hii kwa leo watashangazwa na hoja yangu ya kuwataka walimu wasome saikolojia. Maana wataniuliza, mbona tulifundishwa saikolojia vyuoni wakati tunasomea ualimu, sasa naisoma tena vipi? Mimi ninachosema ni kwamba elimu haina mwisho, na hupati hasara ukiwa wanafunzi wa kudumu wa saikolojia na kujenga tabia ya kudumu ya kuongeza ufahamu wako kuhusiana na kile unachokihitaji katika kumsaidia mwanafunzi ili aweze kusoma na kujifunza vizuri. Mwalimu bora ni yule aliyejenga uwezo wa hali ya juu katika kumtambua mwanafunzi wake na hivyo kuweza kusimamia mahitaji yake kielimu vizuri zaidi.
Kwanza ufahamu kuwa elimu ya darasani ya saikolojia ina upungufu mkubwa. Sehemu kubwa ya utafiti uliofanyika umefanyika katika mazingira ya watoto ambao si wa Afrika. Kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa mno baadhi ya mambo yakaenda tofauti kidogo. Ukisoma habari za Intelligent Quotient (IQ) kwa mfano, utaambiwa mtoto alivyoweza kukumbuka vitu kadhaa baada ya kuonyeshwa kwa muda mfupi tu. Na wanasema mtoto mwingine alipoambiwa avitaje alishindwa. Kushindwa haina maana kuwa mtoto huyu hana akili, ila kuwa vitu ambavyo anatakiwa kuweka kumbukumbu si sehemu ya utendaji wake wa kila siku – daily repetoire, na si sehemu ya utamaduni wake. Mtoto wa Kimasaia anaweza kukutajia kila aina ya miti, ndege na wanyama. Lakini ukimpatia zoezi hilohilo akifika mjini atapwaya hadi ayazoee mazingira yake kwa muda.
Lakini kasoro ya pili ni kwamba darasani unasoma nadharia, na unaweza kuona tofauti au ukweli wa kile ulichofundishwa kwa kuendelea kujisomea na kulinganisha kile unachojifunza na tabia na mwenendo wa wanafunzi.
Kazi moja ya mwalimu ni kutatua matatizo na ikiwezekana kutatua kwa kudumu ili tatizo lisijirudie tena. Mara nyingi niliona nikiwa mwanafunzi au wakati nilipokuwa mwalimu chuo cha ualimu na baadaye sekondari, walimu walikuwa wakijiingiza kwenye tabia za umbea, uzushi, na kuwasimanga wanafunzi bila hata kulifanyia uchunguzi wa kile wanachokizungumzia. Walimu wanapaswa kutoa matamko dhidi ya mwanafunzi baada ya kuyapima na kusaidiwa na utafiti wa kutosha, au kutokana na kujijengea ufahamu juu ya maana ya matendo ya wanafunzi. Kila kinachofanywa na mwanafunzi aghalabu huwa ni matokeo ya athari fulani kisaikolojia, matendo ni matokeo ya kile kilichoko katika fikra za mwanafunzi. Ni kazi ya mwalimu kuhakikisha anajua. Kwa mfano; mwanafunzi kuvuta bangi, ni matokeo ya kitu fulani kilichoko kwenye akili yake – kutojiamini, kuathirika na ushawishi wa makundi rika, matatizo ya kifamilia na kadhalika. Ukishafhamu kwanini anavuta bangi basi utatafuta namna bora ya kumuachisha badala ya kumtukana tu… mara nyingi walimu humuita mwanavunzi wa namna hiyo kwenye chumba cha walimu – ofisi ya walimu na kumuweka mtu kati na kuanza kumchambua, pengine kumvuta vuta na kuzunzungumza naye kwa kebehi, mzaha na matusi, pengine huishia kwenye kumchapa viboko. Lakini kesho yake wanamuona mwanafunzi huyo anaendelea na tabia ileile. Wanashangaa, watamuita sugu, lakini kumbe namna walimu walivyolifuatilia suala hilo bila kutumia utaalamu wowote, ndiyo inamfanya mwanafunzi awe sugu.
Maarifa ya kisakilojia yanafundisha walimu kufanya utafiti, juu ya mwanafunzi wanayemtaka kumrekebisha, au kwa jamii inayozunguka shule. Saikolojia ni nyenzo, maarifa na ni msaada kwa mwalimu ambaye anataka kujua undani wa matatizo anayokutana nayo akiwa na wanafunzi na wanajamii. Wiki ijayo nitatoa mifano ya matatizo yaliyonikuta wakati nikiwa mwalimu chuo cha ualimu na namna ambavyo nilifanikiwa kuyatatua matatizo. Ninadiriki kusema kuwa moja ya sababu ya kufanikiwa kuyatataua matatizo hayo ni ujuzi wangu wa saikolojia, kwa sababu nilielewa wanafunzi walikuwa wanasumbuliwa na nini na namna gani niweze kuwatatulia matatizo yao. Tuonane wiki ijayo!