NI KWELI JPM UTAWAKUMBUKA WATUMISHI UCHAGUZI UKIKARIBIA?

0
604

UFANYE  mabaya zaidi ya  Hitler au mazuri kupindukia zaidi ya malaika, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba  mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke, hakika hakosi kulalamika.

Ikiwa ni miaka miwili ya  fedha kwa upande wa Bajeti ya Serikali ya  Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli,   watumishi wa umma hawajaongezewa mishahara yao hata senti tano.

Kutoongezeka kwa mishahara kwa wafanyakazi wa Serikali  kama ilivyozoeleka katika awamu za uongozi zilizopita inawezekana inatokana na mambo mbalimbali.

Ikumbukwe kuwa Rais Magufuli mara ya kuapishwa kushika usukani aliibua sakata la wafanyakazi hewa hali iliyomfanya kiongozi huyu kujiongezea umaarufu na kuonekana ni mbunifu kwani wananchi walionekana kumuunga mkono.

Hata hivyo  suala la  watumishi hewa liliwekewa kikomo huku  wafanyakazi wakihamasishwa kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi chote cha kuuzika uchafu huu uliokuwa ukipoteza mabilioni ya fedha za walipa kodi.

Pamoja  na  uchafu  huu kuwekewa kikomo lakini la kushangaza  Serikali imeendelea kuutumia kama fimbo ya  kutowatimizia  wafanyakazi maslahi yao  huku ikiibua sakata jipya la vyeti feki.

Mazingira ya namna hii japo kifalsafa ni ya  kuigwa  lakini kwa kuwa yanafanyika ndani ya watumishi ambao wengi wao wana  pato lisilokidhi  mabadiliko ya kiuchumi,  pameibuka mijadala yenye mitazamo tofauti  baada ya kufanya uchunguzi mdogo.

Wapo watumishi hususani walimu wanasema kuwa wakati  Rais  akiomba kura katika kipindi cha  kampeni alituahidi kuwa ataboresha  maisha yetu kumbe ilikuwa ni gia ya kulifikia  tonge  hivyo anasubiri uchaguzi mkuu mwingine ukikaribia ndipo atupumbaze kama watoto wadogo kwa kutuongezea vijimshahara.

Wengine wanasema Rais wetu anapenda sana misifa  kwani amekimbilia  kununua vitu vya gharama kwa muda mfupi mfano bombadia ilhali  sisi watumishi tukiwa taabani.

Rais amefanya haraka kubadilisha mifumo aliyoikuta hususani usimamizi wa bandari na kukusanya kodi kwa kuwabana wafanyabiashara ambao huenda wameanza kumkimbia na hivyo Serikali haina fedha japo  haitaki kuwa wazi.

Kitendo cha Rais kupuuzia ziara za nje ya nchi katika Serikali ambayo haijawa  na viwanda vya kutosha wala  soko la uhakika la ndani  ni hatari kiuchumi.

Rais Magufuli ni mkali mno na hivyo wasaidizi wake wanaogopa kutumbuliwa mara watakapomgusia hali halisi ya watumishi wa Serikali.

Wakati hao wakiwa  na mtazamo  huo  pia  wapo wenye mawazo tofauti kwa kusema kuwa hatua anazochukua Mheshimiwa Rais ni za kubana matumizi ili kujenga uchumi imara.

Wengine wanasema kiongozi huyu ameamua kwa dhati kufuata nyayo  za Baba wa Taifa Hayati mwalimu Nyerere.

Rais anatimiza ahadi yake ya kuwafanya watumishi wote wawe sawa kwa kuwashusha wale waliokuwa wakiishi utafikiri wako peponi.

Kiongozi wetu ana nia nzuri na nchi yetu kwani kwa kubana matumizi ni dhahiri mfumuko wa bei ambao tumeuzoea utapungua kwa kasi.

Rais Magufuli ni jembe kwani anafanya hivyo ili nchi iwe na utaratibu wa kujitegemea kuliko maisha ya kutembeza kopo nje ya nchi ili kuomba misaada wakati tuna rasilimali za kutosha.

Mheshimiwa ni Mzee wa kazi  kwani anataka watu wafanye kazi ili wapate kipato halali kwani inawezekana  fedha za kulipa mishahara  zimepungua baada ya kudhibiti  madawa ya kulevya na ufisadi.

Yote katika yote Serikali ipunguze masononeko kwa  kuwajali watumishi wake ambao wanaonekana kuogopa kusema waziwazi kwa kuhofia  kumwaga unga. Hata hivyo subira yavuta heri kwani wafanyakazi wa Serikali wasifikiri kuwa wao ndio wenye thamani kuliko Watanzania wengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here